Marekani yaitosa Israel Umoja wa Mataifa

Rai - - SIASA KIMATAIFA - NA HILAL K SUED

Alhamisi iliyopita, na kwa mara ya kwanza kabisa tangu suala la ujenzi wa makazi ya Wayahudi katika maeneo wanayokalia ya Kingo za Magharibi za Mto Jordan lilianza kupelekwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani iliruhusu Azimio (Na. 2334) la kulaani ukaliwaji huo kimabavu.

Marekani iliruhusu Azimio hilo kupita katika Baraza hilo kwa kutopiga kura ya veto. Azimio hilo pamoja na mengine lilisema makazi ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalestina inayokalia ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.

Marekani ilkiacha kupiga kura katika Azmio hilo ambalo lilipigiwa kura na nchi nyingine 14 wajumbe wa Baraza hilo zikiwemo zile zenye uanachama wa kudumu – yaani Uingereza, Ufaransa, Russia na China. Nchi nyingine wanachama ambao siyo wa kudumu (kwa wakati huu) ni Venezuela, New Zealand, Misri, Malaysia, Senegal, Ukraine, Angola, Uruguay na Spain, na Canada.

Hatua hii ya Marekani imeikasirisha sana serikali ya Israel inayoongazwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ambaye amesema kwamba ni chuki kubwa inayoonyeshwa na Umoja wa Mataifa kwa taifa la Israel na kwambakamwe halazimiki kulitekeleza.

Aidha Azimio hilo linaonyesha jinsi taifa hilo la Kiyahudi linavyozidi kutengwa hata na maswahiba wake wa miaka yote – nchi za Magharibi ambazo ukiacha Marekani ambayo haikupiga kura, zingine kama Uingereza, Canada, Ufaransa, Hispania zilipiga kura kupitisha Azimio hilo.

Azimio hilo liliandaliwa na nchi nne wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – New Zealand, Venezuela, Malaysia na Senegal. Awali kabisa Misri ndiyo ilikuwa iwasilishe rasimu ya Azimio hilo mapema wiki iliyopita lakini baadaye ilitangaza kuliondoa mnamo dakika za mwisho kabla ya upigaji kura. Vyombo vya habari vilitangaza kwamba kuondolewa kwa rasimu hiyo kulitokana na msukumo wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa kumuomba rais-mteule wa Marekani, Donald Trump kuingilia kati kuhakikisha rasimu hiyo inaondolewa.

Naye Trump inadaiwa alimpigia simu Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi kumuomba nchi yake isiiwasilishe rasimu hiyo hadi yeye (Trump) atakapoingia rasmi madarakani baadaye mwezi ujao – January 2017.

Hata hivyo hatua hiyo ya Misri ilipingwa na nchi nyingine wanachana kama vile New Zeaand na Malaysia ambazo zilisema wao wataiwasilisha rasimu hiyo kwa upigwaji kura – na ndicho kilichofanyika.

Kulikuwapo ushangiliaji mkubwa na vifijo baada ya matokeo ya kura yalipotangazwa na wachunguzi wa mambo walisema hii ilikuwa ni kama hitimisho la mahusiano yasiyokuwa mazuri baina ya utawala wa rais Barack Obama wa Marekani na serikali ya Benjamin Netanyahu.

Marekani ilishatangaza tangu awali kwamba safari hii itaacha kulipigia kura Azimio hilo ambalo huko nyuma nchi hiyo ilikuwa ikipiga kura ya veto kila mara linapoibuka na hivyo kukwamisha. Na siku mbili kabla ya kupiga kura afisa mmoja wa cheo cha juu wa serikali ya Israel aliutuhumu utawala wa Obama kwa kulitosa taifa la Israel kwa kukataa kupiga kura ya veto.

Kwa miaka mingi Marekani imekuwa ikipiga kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuilinda Israel kutokana na maazimio mbali mbali yanayoituhumu.

Na kwa upande wake Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kwamba nchi yake itauangalia upya uhusiano wake na Umoja wa Mataifa. Israel ni taifa lililoasisiwa na kutambuliwa na Umoja wa mataifa mwaka 1948.

Netanyahu alisema: “Nimeiagiza Wizara yangu ya mambo ya Nchi za Nje, katika kipindi cha mwezi mmoja kufanya tathmini ya mahusiano yetu yote na Umoja wa Mataifa pamoja na uchangiaji fedha kwa wawakilishi wa Umoja huo nchini Israel.”

Katika hatua nyingine, Israel ilitangaza kuitwa nyumbani kwa mashauriano kwa mabalozi wake walioko New Zealand na Senegal na kwamba mara moja inasitisha misaada yote kwa Senegal. Israel haina uhusiano wa kibalozi na Malaysia na Venezuela

Kwa ujumla Azimio Na. 2334 linaitaka Israel “mara moja isitishe shughuli zote za ujenzi wa makazi katika ardhi ya Wapalestina inayoikalia kinyume na sheria, ikiwemo Jerusalem ya Mashariki.”

Azimio linasema makazi hayo ni ‘ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na ni kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa amani ya kudumu katika eneo hilo itakayoletwa tu na kuwepo kwa mataifa mawili – yaani Israel na Palestina.’

Takriban Wayahudi 500,000 wanaishi katika makazi 140 yaliyojengwa katika maeneo ya Kingo za Magharibi za Mto Jordan na Jerusalem ya Mashariki tangu Israel ilipoanza kuyakalia maeneo hayo baada ya vita ya 1967.

Kwa upande wake Kiongozi wa Wapalestina Mahamoud Abbas kaunga mkono azimio hilo na kusema ni pigo kubwa kwa sera za Israel za ukaliaji kimabavu katika ardhi za watu wengine.

Kuanza kutoswa kwa Israel na maswahiba wake wa siku zote zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kulianzia mwishoni mwa mwaka 2012 pale (Novemba 29 mwaka huo) Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kutambuliwa Palestina kama ni nchi kamili. Mataifa 138 kati ya jumla ya mataifa 193 yanaounda Umoja huo yalilikubali Azimio hilo, nchi nane zilipinga (zikiwemo Marekani na Israel) na 41 hazikupiga kura.

Ingawa Ufaransa iliunga mkono azimio hilo, Uingereza na Ujerumani hazikupiga kura. Kwa kawaida katika maazimio kuhusu mgogoro wa Palestina na Israel nchi hizi mbili hupiga kura upande wa Marekani.

Tusisahau kwamba nchi hizi za Ulaya ni miongoni mwa nchi nne zilizochaguliwa katika Mkutano wa Madrid, Hispania mwaka 2002 kushughulikia mchakato wa kufikia mapatano ya amani kati ya Israel na Palestina.

Aidha tusisahau kwamba nchi za Umoja wa Ulaya (EU) ni wafadhili wakubwa wa misaada kwa taasisi za kiserikali na kijamii katika Mamlaka ya Palestina.

Balozi wa Marekani Umoja wa Mataifa Samantha Power akizungumza baada ya nchi yake kuamua kutopiga kura katika kupitisha Azimio Na 2334 liliitaka Israel kusitisha makazi ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalestina.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.