Magufuli anapodhihakiwa na machinga mh!

Rai - - HABARI/TANGAZO -

HIVI karibuni Rais Dk. John Magufuli aliagiza kuwa wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kwa machinga, wasibughudhiwe na wasiondolewe katika maeneo ya katikati ya miji wanayofanyia biashara.

Kisa? Eti hakuna sheria inayowazuia wasifanye biashara sehemu hizo. Rais Dk. Magufuli alimwagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa kuwaondoa wafanyabiashara hao.

Rais akiwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, alitoa agizo hilo Ikulu na kuonya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kulitekeleza aachie ngazi. Du!

Lakini Rais Dk. Magufuli alitoa hadhari kuwa hapendi machinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara japo hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au machinga hatakiwi kufanya biashara katikati ya miji.

Kwamba Kigamboni, Dar es Salaam kulikuwa na machinga ambao walihama vizuri kweli, wakatengenezewa miundombinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na viongozi wa machinga walishirikishwa.

Kwamba machinga wajengewe mazingira ya kufanya biashara na wasizagae. Kwamba wakitaka kuwahamisha wazungumze nao kwa utaratibu mzuri na watakapopelekwa liwe ni eneo rafiki kwao na wafaidike kufanya biashara.

Hata hivyo Rais Dk. Magufuli alitoa onyo kuwa amri yake isiwe chanzo cha wamachinga kufanya biashara na kujenga mabanda kila mahali kwa sababu yanachafua mandhari ya miji.

Hata hivyo, baada ya onyo hilo, sasa hali imekuwa vurugu katika baadhi ya mitaa katika miji ya makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini ambayo imefurika machinga.

Katika miji mikuu ya mikoa sasa machinga wanaonekana wakiendelea kujenga vibanda na wengine wakipanga bidhaa zao chini tofauti na onyo la Rais.

Mitaa kadhaa, mfano, ya Kariakoo, Dar es Salaam wafanyabiashara hao wameweka shehena kubwa za bidhaa, huku wakiendelea kuzitandaza pembezoni na hata katikati ya barabara bila kujali wapitanjia wengine, hususan wanaotumia vyombo vya moto.

Mitaa iliyosheheni wafanyabiashara hao ni Kongo, Nyamwezi, Swahili, Sikukuu, Narung’ombe na Mchikichi.

Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka wanaonekana nao wakihaha kutafuta nafasi za kutandaza bidhaa zao nje ili nao wasilipe kodi.

Wamachinga wengine wanapanga bidhaa zao katikati ya barabara na kufanya magari yashindwe kupita.

Hali ni ya namna hii sasa katika miji yote mikoani nchini.

Aidha, sasa machinga wameongeza staili ya kufanya biashara kwa kupanga bidhaa zao juu ya magari yanayoegeshwa kandokando ya barabara katika mitaa mbalimbali Dar es Salaam.

Wanatundika nguo zao katika magari yanayoegeshwa katika mitaa kadhaa, hususan Mtaa wa Kongo.

Kwa hakika machinga sasa wanafanya biashara yao popote kwa jeuri, wengine wakiwa wamepamba nakala za habari iliyokuwa inamnukukuu Rais Dk. Magufuli alipowaruhusu kufanya biashara katikati ya miji, nakala hizo zikiwa zimezungukwa na nguo zao wanazoziuza.

Wengine wanatundika nguo kwenye transforma za umeme bila kujali kuwa sehemu hizo ni hatari kwa maisha yao, na kwamba wanaweza kuleta hitilafu katika mtiririko wa umeme.

Rais Dk. Magufuli alisema machinga wasisumbuliwe, na viongozi wanaogopa kufanya chochote sasa. Itakuwapo shida kubwa mbele ya safari kama Rais asipotoa kauli au amri ya kuwafanya wafanye biashara kwa adabu na nidhamu.

Rais Dk. Magufuli amesema machinga wafanye bishara popote, na wao wanafanya biashara kwa mzaha popote!

Rais Dk. Magufuli alitoa onyo kuwa amri yake isiwe chanzo cha wamachinga kufanya biashara na kujenga mabanda kila mahali kwa sababu yanachafua mandhari ya miji.

Lakini sasa hali imekuwa hivyo baada ya baadhi ya mitaa katika miji ya makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini kufurika machinga.

Katika miji mikuu ya mikoa tangu Dk. Mugufuli atoe ruhusa, machinga wanaonekana wakiendelea kujenga vibanda na wengine wakipanga bidhaa zao chini.

Mitaa kadhaa Dar es Salaam wafanyabiashara hao wameweka shehena kubwa za bidhaa, huku wakiendelea kuzitandaza katikati ya barabara bila kujali wapitanjia wengine.

Mwenyewe Rais Dk. Magufuli alisema kuwa amri yake haina maana kuwa machinga waendeshe shughuli zao ovyo. Na hii haina maana kuwa hakueleweka.

Hivi sasa machinga wananunua chakula na kukila katika mazingira hatarisha yenye kila shaka ya afya.

Kama alivyosema Rais, hawana budi wazingatie sheria, wasipange bidhaa zao ovyo mitaani na kuchafua mazingira.

Ingekuwa vizuri kama pia watatengewa baadhi ya mitaa huku wakiweka meza kwa mpangilio pembezoni mwa barabara, kuweka mapipa ya taka na kuacha nafasi za watu kuingia madukani.

Mpango huu utawezesha kutolewa kwa mashine za kukusanya ushuru na kukagua risiti za wafanyabiashara ili Serikali ipate mapato yake pia.

Lakini kilichotokea baada ruhusa ya Rais Dk. Magufuli, ni machinga kuwa na kiburi na kufanya mizaha inayodhihaki ruhusa iliyotolewa na Rais wa nchi! Mh!

Machinga wakiwa wamepanga bidhaa katikati ya barabara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.