January Makamba: Tusiogope

Rai - - MBELE - NA OSCAR ASSENGA, TANGA.

Watu wanataka mabadiliko lakini wanaogopa kubadilika, hiyo si sawa, tusiogope, hatupaswi kuyaogopa mabadiliko, badala yake wote tunapaswa kuondokana na hali hiyo kwa kujipanga upya ili kuendana na jambo hilo kwa vitendo kwani hiyo ndio njia inayoweza kuwafikisha mbali kimaendeleo.

WAZIRI wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira January Makamba amesema hakuna sababu ya kuogopa mabadiliko ya kweli.

Alisema hakuna nchi yoyote dunia inayofanya mabadiliko bila kupitia kwenye kipindi kigumu kwa sababu jambo hilo si lele mama kama watu wengi wanavyofikiria.

Aliitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki hii jijini Tanga, wakati akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu kwenye baraza la Eid lililofanyika kimkoa katika shule ya Sekondari Jumuiya.

Alisema ni lazima watu wayakubali mabadiliko ya kweli na kuwa na utayari wa kubadilika na kuendana nayo kuliko kuanza kuogopa, hatua mbayo inaweza kukwamisha mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

“Niwaambie kitu… watu wanataka mabadiliko lakini wanaogopa kubadilika, hiyo si sawa, tusiogope, hatupaswi kuyaogopa mabadiliko, badala yake wote tunapaswa kuondokana na hali hiyo kwa kujipanga upya ili kuendana na jambo hilo kwa vitendo kwani hiyo ndio njia inayoweza kuwafikisha mbali kimaendeleo.

“Tunapaswa kufikiri fikra tofauti, ni lazima tubadilike kuendana na kasi kubwa iliyopo sasa, lengo ni kupata maendeleo, hatupaswi kuyaogopa mabadiliko yaliyopo sasa,” alisema.

Akimzungumzia Rais Dk. John Magufuli, Makamba alisema ni kiongozi mwenye nia njema na nchi ya Tanzania anayehakikisha Watanzania wanapata maendeleo makubwa na kwamba ni vema tukamuunga mkono kwa vitendo na kwa kumuombea.

“Niwaambieni, mkitaka Rais wetu ajikwae na nchi itajikwaa, lakini pia tukitaka Rais afeli nchi nayo itafeli, tumtakie mema Rais wetu ili afanikiwe kuiletea mema.”

DAWA ZA KULEVYA

Katika hadhara hiyo Makamba pia alizungumzia suala la dawa za kulevya, ambapo alisema jambo hilo ni janga kubwa hasa katika ukanda wa Pwani ambako vijana wengi wamejiingiza kwenye ulevi huo.

Alisema maeneo yaliyoathiriwa zaidi na dawa za kulevya hasa kwa vijana ni Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani.

Makamba alitoa rai kwa viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kukemea suala hilo kila mmoja kwenye eneo lake.

“Jambo hilo ni tatizo kubwa sana kwenye ukanda wa Pwani, niwaombe viongozi wa dini kuona namna bora ya kulikemea hili ili kuliondosha katika maeneo yenu, hitaji letu ni kuwaondoa vijana kwenye janga hili.”

KUUNDA MAKUNDI

Katika kuukaribisha umoja na mshikamano kwa waislamu, Makamba alitoa wito kwa Taasisi inayowaongoza waislamu wote wa Mkoa wa Tanga, kuanzisha kundi la WhatsApp litakalowajumuisha vijana wasomi wa dini kuweza kujadili masuala yao.

Alisema taasisi hiyo ina changamoto kubwa ya kuwafikia vijana wengi waliopo kwenye sekta binafsi na umma hivyo suala hilo lingewezesha kurahisisha upatikanaji wao.

Aidha, alisema jambo ambalo linafanywa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi ni kuimarisha Bakwata.

“Katika jambo hilo tutaomba msaada kwa waislamu wengine waliopo nje ya nchi kwa lengo la kufanikisha mambo hayo muhimu kwa ajili ya kupata maendeleo,” alisema.

MAADILI KWA VIJANA WA KIISLAM

Alisema katika dini ya uislam kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili hasa kwa vijana waliopo maeneo ya mijini kwa kupenda kwenda kwenye kumbi za starehe.

Aliongeza katika hilo lazima kuundwe mwongozo mzuri wa kuwalea vijana hao kwani wanaweza kupotosha kizazi kikubwa siku zijazo.

“Hakikisheni tunawaweka vijana wetu kwenye muundo mzuri wa dini kwani Tukikiacha hakitakuwa na upendo wa dini, tunaweza kupoteza msingi wa mambo yote mema na amani ya dunia.”

UMOJA NA MSHIKAMANO

Alitoa wito kwa Waislam nchini kuwa na umoja utakaosaidia kuwepo kwa mshikamano imara, ambapo pia alimpongeza Mufti kwa kuimarisha umoja wa Waislam.

Alisema waislam wanakabiliwa na changamoto ya dini hiyo kuhusishwa na ugaidi, jambo ambalo si jema kwa waislam wote duniani.

“Dini ya uislam kuhusishwa na suala hilo hili tusilichukulie kiwepesi sana kutokana na teknolojia, huko tunapokwenda tunapaswa kuuona umuhimu wa dini zetu,”alisema.

Hata hivyo, aliwataka waislam waendelee kuihubiria dini hiyo kwa nia nzuri na kwamba wanaofanya vitendo viovu si wenzao.

SHIGELA AMPONGEZA

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amempongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuupigania mkoa huo kwenye suala zima la maendeleo.

Shigella alimpongeza Rais Magufuli kwa kuupigania mkoa huo kupata mradi wa bomba la mafuta jambo ambalo limesaidia kupanua wigo mpana wa fursa mkoani hapa.

Alisema kutokana na mradi huo zipo taasisi kadhaa zimekwishafika mkoani hapa kwa nia ya kutafuta maeneo ya uwekezaji.

“Mradi huu ni mkubwa na ajira za moja moja zitapatikana hivyo niwasihi wananchi wajipange vizuri kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayokuja mkoani hapa, lakini pia kuongeza uzalishaji ni vema tukawa na mshikamano na tuendeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya.”

Kwa upande wake Shekh wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu aliwataka waislam kuendelea kutenda mambo mema waliokuwa wakiyatenda wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhani ikiwemo kuweka mshikamano kwenye kila jambo la maendeleo.

Alisema mshikamano huo ndio utakuwa chachu ya kuweza kufikia mafanikio makubwa ikiwemo pia kuhakikisha wanatunza mazingira na rasilimali za Taifa zinazowazunguka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.