Mahakama zafungua milango ya haki kwa wapinzani

Rai - - MBELE - NA HILAL K SUED

Wiki iliyopita mahakama za juu katika nchi mbili tofauti Barani Afrika zilitoa maamuzi mawili ya kihistoria yanayoelezwa kuwa iwapo yatatekelezwa na kuigwa na nchi nyingine yatakuwa hatua muhimu ya kuimarisha demokrasia – hususan katika uendeshaji wa uchaguzi na upigaji kura na uwajibikaji wa viongozi kwa ujumla.

Kwanza Mahakama ya Katiba ya Afrika ya Kusini (Constitutional Court) ilitoa uamuzi kwamba Spika wa Bunge la nchi hiyo, Baleka Mbete kikatiba anao uwezo wa kuamua iwapo kura ya siri itumike kuhusu upigaji kura wa ombi la kutokuwa na imani na Rais.

Katika uamuzi wa wengi katika jopo la majaji waliosikiliza shauri lilopelekwa na vyama vya upinzani, Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng alisema kwamba si kweli kwamba Spika Mbete, kama anavyodai, hana madaraka kikatiba ya kuamua upigwaji wa kura ya siri.

Uamuzi huu una maana kwamba iwapo wapinzani wataomba ipigwe kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma, Spika Mbete hataweza tena kutoa hoja kwamba anafungwa kikatiba kuruhusu kura ya siri. Wapinzani wamekuwa wakidai kwamba iwapo kura ya wazi itapigwa, Wabunge wengi wa chama tawala cha ANC watamtosa rais wao.

Uamuzi wa pili wa mahakama (ambao ndiyo ntauzungumzia katika makala hii) ni ule uliotolewa na Mahakama ya Rufaa ya Kenya kuhusu shauri la awali lililopelekwa na muungano wa vyama vya upinzani wa National Super Alliance (NASA) unaoongozwa na Raila Odinga.

Awali shauri hilo lililoanzia Mahakama Kuu ya nchi hiyo liliomba mahakama hiyo itamke kwamba Kituo cha Kitaifa cha Majumuisho ya Kura (National Tallying Centre) kuhusu matokeo ya upigaji kura katika uchaguzi ni batili, kiharamishwe, na badala yake matokeo yote yanayotangazwa katika kila kituo, katika nafasi zote za ugombea, ndiyo yawe ya mwisho.

Katika uamuzi wake mapema mwezi uliopita (Mei) Mahakama Kuu hiyo ilikubaliana na ombi la muungano wa NASA lakini Serikali, kupitia Mwanasheria wake Mkuu pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zilikata Rufaa Mahakama ya Rufaa ambayo wiki iliyopita jopo lake la majaji watano lilitoa uamuzi wa kukubaliana na Mahakama ya chini yake – (Mahakama Kuu) kwamba matokeo yanayotangazwa vituoni ndiyo yawe ya mwisho.

Jopo hilo la majaji Judges Asike Makhandia, Kathurima M’Inoti, Patrick Kiage, William Ouko na Agnes Murgor lilijadili shauri hilo kwa masaa manne na nusu kabla ya kuja na maamuzi kwamba matokeo katika vituo hayawezi kamwe kubadilishwa na mtu yoyote isipokuwa tu iwapo yatakatiwa rufaa mahakamani.

Wadadisi wa mambo wanasema huu ni ushindi wa pili mkubwa wa wapinzani nchini Kenya, baada ya ule ulioing’oa tume nzima ya zamani ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wake Ahmed Isaac Hassan na wakurugenzi wake kwa madai ya upendeleo katika uchaguzi wa 2013 na pia ufisadi kutokana na kashfa ya manunuzi ya vifaa vya Hata hivyo wanasheria wa upande wa serikali na wale wa IEBC walipigania kidete mahakamani kulinda utaratibu uliokuwapo wakidai kwamba Mwenyekiti wa IEBC ndiyo wa mwisho katika kutangaza matokeo yanayokusanywa kutoka vituoni na kuletwa kwake.

Utaratibu wa zamani ulikuwa unakiuka sheria na kanuni za IEBC yenyewe – kwamba mwenyekiti wa tume hiyo ndiyo msimamizi pekee wa uchaguzi katika matokeo ya uchaguzi kwa ngazi ya urais (sole Returning Officer of Presidential results) na kwamba matokeo ya vituoni yanayotangazwa huwa ni “ya muda tu” (provisional).

Katika maamuzi yake Mahakama ya Rufaa ilisema ni “unafiki tu na kitu kisichoingia akilini” kwamba IEBC inahoji usahihi wa matokeo inayopelekewa na maafisa wake wenyewe waliowaweka vituoni. Walisema utangazaji wa matokeo usiwe kama ‘onyesho la mtu mmoja” (one man show) kwani kunabeba viashiria vya kuwa uchochoro wa wizi wa kura.

Isitoshe Mahakama hiyo iliona kuna kinga za kutosha dhidi ya wizi wa kura katika ngazi za vituo ambako kuna mawakala wa vyama vya siasa, watazamaji huru na vyombo vya habari vilivyoruhusiwa.

Mawakili wa upinzani walitoa hoja kwamba kwa kuwa ofisi ya mwenyekiti wa IEBC iko Nairobi ikisubiri matokeo kutoka nchi nzima, kunakuwepo mwanya wa kuyachokonoa matokeo kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba wakati mwenyekiti huyo anayapokea, tarakimu zinakuwa zimebadilishwa mara kadha kupitia njama baina ya vyombo vya serikali na wasimamizi wa vituo wasio waaminifu. Inadaiwa watu hawa wasio na uaminifu ghafla hutoweka, na kuibuka miezi kadha baadaye.

Wadadisi wa mambo wanasema maamuzi haya ya Mahakama ya Rufaa ni ya kihistoria iwapo yataigwa katika uendeshaji wa chaguzi katika nchi nyingi barani Afrika ambako katika utamaduni wa sasa Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi kwa muda mfupi hujifanya ‘mungu mtu’ kwa kuwaweka wananchi katika shauku kubwa kungojea kumtangaza mshindi wa kiti cha urais, kwani mshindi anaweza kujulikana hata kabla ya kura zote kuhesabiwa.

Hili hutokea Marekani na nchi nyingine za magharibi. Marekani kwa mfano, haina Tume ya Uchaguzi kama ilivyo hapa kwetu na nchi nyingine nyingi.

Usimamizi wa chaguzi zote hufanywa na mamlaka za serikali za majimbo ambako kila kituo hutangaza matokeo ambayo vyama vya siasa, watu wa vyombo vya habari na taasisi zingine huzikusanya na kuzijumlisha kwa uwazi na kuonyeshwa katika runninga na sehemu nyingine ili wapigakura waweze kufuatilia mwenendo wa wagombea wao.

Kinachofuatia ni kwa mgombea anayeonekana atashindwa kumpigia simu mshindi na kumpongeza kwa ushindi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.