ASKOFU DK. SHOO:

WANAOMPINGA JPM KWENYE VITA YA UCHUMI HAWAJUI WATENDALO

Rai - - MBELE - NA FRANCIS GODWIN, IRINGA 0754026299

WIKI hii ilikuwa ya shamrashamra za sikukuu ya Idd el Fitr ambapo katika mhubiri ya viongozi mbalimbali wa dini walitumia jukwaa hilo kuonya, kushauri na kutoa maoni yao kuhusu mambo kadha wa kadha yanayoihusu jamii na serikali kwa ujumla.

Mkoani Iringa, viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo pia hawaku nyuma katika hilo ambapo pamoja na mambo mengine walielezea kufurahishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli hasa katika nyanja ya kupambana na mafisadi au wanyonya na kurudisha rasilimali za Taifa.

Viongozi hao hao walielezea bayana kufurahishwa na vita aliyoianzisha Rais Magufuli kwa kupambana na wanyonyaji.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo alisema mtu anayempinga Rais Magufuli kwa kazi ya kuwawajibisha wezi wa rasilimali za Taifa hana mapenzi mema na Taifa hili hao watakuwa mpumbavu.

Askofu Dk. Shoo alisema wao kama kanisa wanapongeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli ya kuwashughulikia wale wote waliokuwa wakishirikiana na mabepari wazungu kutaifisha madini ya Tanzania.

“Wapo viongozi ambao muda wote walikuwa wakisafiri kwenda kusaini mikataba ya madini na mikataba mingine nje ya nchi na wakikireja nchini kazi yao ni kujisifu kuwa safari zilikuwa za mafanikio makubwa kumbe walikuwa wametoka kujinufaisha kwa kusaini mikataba na mabepari hao ili kuiba mali za Watanzania …nasema hivi kwa watanzania wenye uelewa na wasio na uelewa tunampongeza sana Rais wetu na kama wapo wanaopinga nasema hao ni watakuwa ni wapumbavu “alisema Askofu Dk. Shoo.

Alisema kazi kubwa anayoifanya Rais kanisa lake linaheshimu na kutambua na kuendelea kumpongeza pamoja na kumuombea zaidi azidi kuwatumikia watanzania bila kuchoka .

Mbali na hayo, pia alizipongeza kamati mbili za madini zilizoundwa na Rais Magufuli akisema zimewaaumbua baadhi ya watanzania waliodhani ni sifa kusaini mikataba ya madini inayonya haki ya watanzania.

“Kama hao watu waliosaini hiyo mikataba walidhani wanaisadia nchi huku wakijua mikataba hiyo inalenga kuiibia nchi, wajue hayo ni mambo ya aibu na ni upumbavu mkubwa kufanya mambo kama hayo kwa ajili ya matumbo yao binafsi,” alisema.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Abubakar Chalamila alisisitiza watanzania kuendelea kumuombea ili Taifa lishinde vita ya uchumi inayofanywa na mafisadi wachache.

“Vita hii ambayo Rais wetu anayoifanya ni vita kubwa na ni vita inayowagusa wakubwa na matajiri wakubwa duniani hii ni vita ya kiuchumi kweli tunampongeza kwa kazi hii nzuri.

“Kwa sababu ni dhahiri utendaji kazi wa Rais Magufuli unaofanana na ule wa baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na kuwa kazi kubwa inayopaswa kufanywa na watanzania ni kuendelea kumpa ushirikiano na kumuombea zaidi.

“Tunadhani makosa yalifanyika awali kwa kutotoa kipaumbele katika maelezi bora ya hofu ya Mungu kwani chimbuko la ufisadi, wezi wa mali za umma na uadilifu usio mzuri miongoni mwa viongozi wa umma ni kutokana na kupuuza kipaumbele cha hofu ya Mungu na wengi wanafikiri kwao kipaumbele kikubwa kwa mtoto ni elimu pekee pasipo kumpa Mungu nafasi “alisema.

Waililia Katiba mpya

Mbali na hayo hawakuacha suala la Katiba mpya, ambapo ha Askofu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville alimuomba Rais Magufuli kuumalizia mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.

Alisema wakristo na watanzania kwa ujumla wao wana imani kubwa na serikali ya awamu ya tano na ni matarajio yao kwamba mchakato wa kuandika katiba utamalizwa kama lengo lilivyokuwa.

“Dayosisi ya Iringa inatoa mwaliko kwa vyama vyote vya kisiasa na jamii nzima ya watanzania tuendeleze kukuza tunu ya ushirikiano na moyo wa kizalendo ili kuwa na maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Kwa sababu tunatiwa moyo na jitihada zinazoendelea kufanywa na Rais Magufuli katika kufufua uchumi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya watanzania wote na kuwa wa kuendelea kufanya hivyo ni faraja kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, aliiomba serikali iangalie upya suala la kodi kwa mashirika ya dini akisema baadhi ya kodi wanazolipa ikiwepo ya kuendeleza vyuo vya ufundi na ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi zimekuwa mzigo mkubwa kwao.

Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa Zainabu Mwamwindi (CCM) alisema iwapo muswada wa katiba utakaotaka rais Magufuli kuongezewa muda wa kuongoza ukitua bungeni hata kesho utapitishwa kwani hakuna mwanasiasa ambae yupo tofauti na utendaji kazi wa rais .

Mwamwindi alisema kuwa mataifa ya nje yanaitazama Tanzania mpya kutokana na utendaji kazi wa Rais na kuwa itapendeza kuona Rais anaendelea kuungwa mkono na kuwataka wapinzani wasiopenda kazi nzuri ya kuliletea taifa maendeleo kufunga midomo na kuwa wao uwezekano wa kuiondoa CCM madarakani haupo kwa sasa.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini ili kufikia malengo yake ya kimaendeleo.

William alizungumzia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo mkoani Iringa na akawaomba watanzania na wawekezaji kuzitumia ipasavyo kuunga mkono jitihada za Rais za kuifanya nchi kuwa ya viwanda.

Askofu mstaafu wa dayosisi hiyo Dkt Owdenburg Mdegela alisema kuwa imani ya watanzania kwa Rais Magufuli ni kubwa na kuwataka wanazuoni wanaopinga utendaji wake kukutana katika mdahalo wa wazi ili kupingana kwa hoja.

Alisema anashangazwa kuona wapo baadhi ya wanazuoni ambao wanapinga kazi ya Rais na baadhi yao ni wanasheria hivyo alisema kama yupo mwanazuoni aliyetayari kupinga kwa hoja wakutane katika madahalo wa wazi.

Rais Dk. Magufuli akisalimiana na Askofu Dk. Shoo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.