YA GADDAF,

LUMUMBA YANA KITU CHA KUMFUNZA MAGUFULI

Rai - - MBELE - Na Mwandishi wetu

FEBRUARY22, mwaka 2002 ndipo ulipokoma ubabe wa vita wa Joseph Savimbi uliodumu kwa zaidi ya miaka 30. Savimbi akiwa kiongozi mkuu wa kundi la UnitaAngola, alihusika na mauaji, utekaji na kila aina ya ukatili.

Swali lililokuwa likiulizwa na wengi, nani alikuwa nyuma ya Savimbi? Kwa zaidi ya miaka 30 ya ubabe wake wa vita ni nani alikuwa mfadhili wake? Dhamira ya Savimbi katika kupigana ilikuwa ni demokrasia kama alivyojipambanua ama kulikuwa na lengo lingine nyuma ya pazia?

Baada ya mengi kuzungumzwa na mengi kuandikwa baadaye ilikuja kujulikana Savimbi alikuwa hapigani kwa ajili ya demokrasia ama uhuru wa Angola kama alivyopenda ijulikane. Alikuwa anapigana ili madini ya dhahabu, almasi na mafuta yaweze kwenda vizuri. Nyuma ya Savimbi na UNITA yake kulikuwa na Marekani, Uingereza na mabeberu wengine.

Hawa walikuwa tayari kutoa fedha, mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya askari pamoja na fadhila nyingine ili vita isikome.

Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa sana rasilimali. Tafiti zinaonesha kati ya simu tano basi nne zinatengenezwa na madini kutoka Kongo.

Muda mchache baada ya kupata uhuru, 1960, Patrice Lumumba akateuliwa kuwa Waziri Mkuu. Akiwa kijana mdogo, mzalendo halisi, akaonesha nia na dhamira ya kutaka Congo ifaidike na rasilimali zilizotapakaa katika ardhi hiyo.

Dhamira hii haikuwapendeza mabwana wakubwa. Kwa kushirikina na Wacongo wajinga, mabeberu wakiongozwa na Ubelgiji wakaanza hila juu ya kijana huyu.

January 7, 1961, akiwa na miaka 34 Patrice Lumumba alitoweka gerezani alipokamatwa na serikali dhalimu ya Joseph Kasa Vubu akishirikina na kiongozi mwezie Joseph Desire Mobutu.

Hamu yake ya kutaka kuifanya Congo kufaidika na rasilimali, ikamfanya atoweke na baadaye kusadikika kuuawa na vikosi vya serikali mpya.

Kwa miaka mingi Muhamar Gaddaf alikuwa mkali kwa rasilimali za Libya. Alihakikisha kila rasilimali ya taifa hilo inakuwa na faida na tija kwa wananchi wa kawaida wa taifa hilo.

Kuhakikisha suala hilo linawezekana, Gaddaf aliweka sheria madhubuti ili mafuta yanayopatikana katika taifa hilo yaweze kuwa msaada wa Walibya wote. Kupitia sheria zake makini, mafuta yalileta neema na baraka katika taifa hilo na sio laana kama mataifa mengine. Wananchi walipata huduma zote muhimu na kufurahia maisha. Hakukuwa na mgawo wa umeme, shida ya barabara, pamoja na nchi hiyo kuwa jangwani ila wananchi hawakuwa na shida na maji safi na salama kutokana mauzo ya mafuta kuwapa gawio kubwa na wao kulitumia katika kuijenga nchi yao na kuboresha maisha ya Walibya. Kicheko hiki kwa walibya kilikuwa kilio kikubwa sana kwa mabeberu wa magharibi.

Kwa miaka mingi waliandaa mipango ya kummaliza Gaddaf na serikali yake. Bahati mbaya kwao, nzuri kwa Walibya na Gaddaf mwenyewe majaribio mengi yalishindwa kufanikiwa.

Baada ya kuona majaribio yao ya moja kwa moja yanashindwa, wakaamua kuwatumia Walibya wenyewe. Wakachukua baadhi ya walibya wenye uroho wa madaraka na uchu wa utajiri, wakawamezesha wimbo wa demokrasia kisha wakawapa mbinu za kijasusi na kuwarudisha Libya.

Mwanzo wakaanza kwa gia ya maandamano. Wananchi wengi wa mataifa ya nje wakadhani kweli wale walikuwa wanadai kitu cha msingi. Wasiojua ni kwamba nyuma ya maandamano yale, kulikuwa kuna hila za Wamarekani na washirika wake. Uchungu wa kubaniwa kubwia mafuta wa miaka mingi ulizaa mbinu muafaka na kukubalika kwa wengi bila kujulikana.

Baada ya maandamano kugeuka uasi. Marekani na washirika wake wakatumia upenyo huo kuanza kumshambulia Gaddafi na vikosi vyake. Ilipofika Oktoba 20, 2011 shujaa huyu wa walibya aliuawa.

Gaddaf aliuawa sio kwa sababu alikuwa akichukia demokrasia. Kwa wasiojua ukweli wanaweza kuamini uongo mwepesi huo. Ila ukweli ni kwamba Gaddaf aliuawa akiwa analinda na kutetea rasilimali za walibya. Aliuawa baada ya kukataa nchi yake kufanywa ghala la mataifa ya magharibi na kunyonywa.

Sasa habari kubwa ni Rais Magufuli kuanzisha kile kinachojulikana kama vita ya uchumi. Wananchi wa kawaida wanafurahia. Wazalendo wanapongeza. Viongozi wa dini mbalimbali wameonesha kuunga mkono na kusema watazidi kumuombea kama ambavyo amekuwa akiomba. Ila je, Rais Magufuli kajipanga kweli kukabiliana na wabadhirifu wote wa uchumi wetu?

Katika sakata la ACACIA kuna mengi yanazungumzwa. Kubwa ni kwamba katika bodi ya wakurugenzi ya kampuni hiyo kuna watu wakubwa mno katika serikali nyingi duniani ambapo bila shaka wamekuwa wakifaidi faida na magawiwo yanayotokana na uwekezaji wao sehemu mbali mbali duniani, Tanzania ikiwemo. Rais Magufuli kupitia mamlaka zake, amejipanga madhubuti katika kuzuia mchezo huu usibadilishwe? Kajipanga kuzuia usifanyike ujanja wa kuonekana wao ndio mashujaa badala ya yeye?

Rais Magufuli kajipanga kwa dhati ili mabwana hawa na wenzao wasijipange na kuamua kumchafua na kachafuka kama ilivyotokea kwa wengine duniani waliotaka kuzuia mirija ya wakubwa katika kunyonya utajiri wa baadhi ya nchi?

Katika sakata la Congo, Libya na Angola, Magufuli kajifunza nini? Anajua nchi hizo zinapigana sio kwa sababu ya kitu kingine ila utajiri wao wa rasilimali. Yeye baada ya kuona kuna ulazima wa kuzuia kuibiwa na kutaka rasilimali za taifa hili ziwasaidie watanzania. Anadhani mabwana hawa kuja Ikulu na kusema watajadili na kuyamaliza, wataishia hapo? Magufuli hajioni kama kageuka mwiba kwao hivyo ili wale chakula vizuri watakuwa hawana budi kutumia laghai na janja zao zozote ili kumtoa? Washauri na mamlaka za ujasusi za Rais Magufuli zimeliona hili kwa makini? Zimejipanga vipi kukabiliana na suala hili?

Wakati tukiendelea kusifu na kupongeza juhudi zote zinazofanywa na Rais Magufuli katika kutetea mali ya umma na rasilimali, ni muda mufaka pia kujiuliza kama Watanzania kwa umoja wao watakuwa na uelewa wa kuzijua hila za waathirika wa masuala haya katika kutaka kugeuza ukweli. Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania.

Kuhakikisha suala hilo linawezekana, Gaddaf aliweka sheria madhubuti ili mafuta yanayopatikana katika taifa hilo yaweze kuwa msaada wa Walibya wote. Kupitia sheria zake makini, mafuta yalileta neema na baraka katika taifa hilo na sio laana kama mataifa mengine.

Muhamar Gaddaf

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.