Chadema kwafukuta

Rai - - MBELE - NA FRANCIS GODWIN, IRINGA

BUNDI ametua ndaniChama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoani Iringa baada ya madiwani watatu kujiuzulu nafasi zao kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukosekana kwa demokrasia ndani ya chama hicho.

Madiwani hao ambao wanatoka katika jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa ni Baraka Kimata wa kata ya Kitwiru na madiwani wenzake wawili wa viti maalum Leah Mlelewa na Husna Ngasi.

Wakitangaza dhamira hiyo ya kujiuzulu wiki iliyopita madiwani hao walisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na mwenendo wa chama hicho jimbo la Iringa mjini na hivyo wameamua kuachia nafasi zao na kubaki bila kuwa wanachama wa chama chochote.

Kimata ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa Chadema jimbo la Iringa Mjini na Mwenyekiti wa madiwani jimbomi humo alisema nafasi zake zote ameziacha na sasa ataendelea na shughuli zake nyingine nje ya siasa kwani siasa kwa ujumla wake imemshinda.

Alisema ingawa Chadema ni chama cha kidemokrasia ila katika jimbo la Iringa mjini demokrasia imekuwa ikivurugwa na baadhi ya viongozi na hata kupelekea madiwani kuona chama hicho ni kichungu hivyo hatua yao ya kujiuzulu ni kilelezo tosha kuwa ndani ya chama hicho Iringa mjini hakuna usalama.

Alisema mbali ya sababu nyingine zilizosababisha kujiuzulu kwake na wenzake bado amekuwa akikosa ushirikiano kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Mch. Peter Msigwa ambaye toka amechaguliwa mwaka 2015, katika kata yake hajawahi kufanya ziara ya aina yeyote hivyo kutokana na kubaguliwa huko pamoja na kuendelea kudidimizwa haki yake wakati wa kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo ya umeya na unaibu meya ameona ni vema kutojihusisha na masula ya siasa.

“Kumekuwepo na maneno kutokana kwa watu kuwa tumenunuliwa… ila ukweli utabaki palepale kuwa tumeondoka kwa kukwepa demokrasia mbaya ndani ya chama chetu na tutakuwa huru kujiunga na chama chochote kama ACT Wazalendo ama chama kingine chochote chenye demokrasia nzuri kwani mbunge Msigwa anaendesha chama hiki kidkteka,” alisema.

Naye Leah Mlelewa ambae alikuwa Afisa Habari wa Jimbo la Iringa mjini, Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA ) na katibu wa madiwani alisema ameachia ngazi nafasi zote ikiwemo ya udiwani kama wenzake kutokana na ubabe unaofanywa ndani ya chama hicho.

Wakati Husna Ngasi alisema ameachia ngazi kutokana na kubaguliwa kwa misingi ya itikadi zake za dini hivyo kuamua kukaa pembeni.

Duru za siasa kuhusu mgogoro huo wa madiwani unaokua siku hadi siku ndani ya chama hicho zimebainisha kuwa Mbunge wa jimbo hilo, Peter Msigwa ambae ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa amekuwa akijaribu kuficha ukweli wa mambo kwa kudai kuwa mambo ni salama ilihali ni tofauti.

Aidha akizungumzia maamuzi hayo ya madiwani, Mchungaji Msigwa alisema hana muda wa kujibizana na Kimata, kama ameamua kundoka Chadema aomdokee salama na asitafute umaarufu kupitia jina lake.

“Huo udikteka ameanza kuuona baada ya kununuliwa na kujiuzulu mbona siku zote alikuwepo ndani ya Chadema hakusema hayo?.

“Ameondoka kwa kuwa Msigwa ni dikteta ila atambue ni jana tu siku ambayo anajitoa ndipo katibu mkuu wa chama chetu alikuwepo Iringa hivyo kama mimi ni dikteta huo udkteta wa Msigwa ndio angeueleza kwa katibu mkuu ... kwa sasa kuna udikteta na mabavu hivyo anataka kusema heri udikteta wa viongozi wa CCM kuliko wa Msigwa?

“Suala hili nawaachia wananchi wa Iringa na ninyi waandishi wa habari mnanifahamu vizuri kama kweli Kimata anasema mimi ni dikteta kuliko mtu mwingine basi Mungu ndiye anajua na mna haki ya kunipima -- hebu nipimeni kazi zangu kwa kipindi cha kwanza na hiki cha pili – utanilinganisha na mbunge yupi hapa Iringa!

“Amezungumza kuwa ndani ya chama hakuna demokrasia, hakuna chama chochote ambacho kinaenda bila maadili wala nidhamu,” alisema Msigwa.

Aidha alisema Katiba ya Chadema inawaonya na kukataza kutoa mambo ya chama nje, yaani hadharani na kama kulikuwa na uchaguzi ambao hukuridhika nao alitakiwa kukata rufaa ngazi ya juu ila Kimata hajafanya hivyo zaidi ya kulalamika.

Alisema mbinu ya kuua upinzani imekuwa ikitumika kwa kuwanunua madiwani ila hawataweza kwani upinzani ukifa na CCM itakufa na kwamba hata yeye wamekuwa wakitaka kumnunua kwa pesa kubwa zaidi ila wameshindwa kufanya hivyo.

“Wapo watu wanatumika kutaka kutuuza na wapo wengine ambao wapo nyuma wanataka kutoka ndio maana nasema wanaotoka watoke salama watuache na Chadema chetu, sikuingia Chadema kwa ajili ya njaa… na tuhuma nilizopewa na kimata ambazo kanituhumu kupitia radio nitakwenda mahakamani, walinitukana mwaka 2010 hawakuweza na wamerudia mwaka 2015 wameshindwa, nasema hawawezi,” alisema.

Aliongeza: “Kuna watu hapo wakikaona ka-msigwa kana mwili mdogo wanaona kama hakatoshi. Mwili huu usiwape shida mimi ndiyo mwenyekiti wa kanda nilishasema wapo madiwani watakaonunuliwa ila hamkuamini ila leo mmeamini .... ila nawaomba sana eleweni hata kwenye treni wapo wanaopanda na kushuka, na kuna wimbo kanisani unaimbwa wengi wanapanda milima wengine wanashuk. Hicho ndicho chama cha siasa wengine wanatoka wengine wanaingia kama Kimata alikuwepo leo ametoka.”

Akizungumzia kuhusu kutotembelea kata ya Kitwiru tangu achaguliwe alisema ni uzushi wa Kimata kwani alishafanya mikutano zaidi ya miwili Nyamhanga, Uyole na amekaa vikao vya akina mama.

“Ni akili za kitoto kuhama Chadema kwa kuwa eti mbunge hajafanya ziara kwenye kata yako. Mbona Rais John Magufuli hajafanya ziara Iringa ndiyoo kusema wabunge na madiwani wajiuzulu?

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.