Rais Lungu naye aungana na Kikwete

Rai - - MBELE - LUSAKA, ZAMBIA

RAIS wa Zambia Edgar Lungu ameunga mkono kauli ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuhusu kutowachukulia wapinzani kama maadui baada ya kulegeza msimamo wake kuhusu vyama vya upinzani nchini humo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Ikulu ya Zambia kuwashutumu polisi wa nchi hiyo kwa hatua yao ya kusitisha mkutano wa sala ambapo kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani (UPND), Hakainde Hichilema alitarajiwa kuhudhuria.

Alhamisi iliyopita polisi wakiwa wamebeba silaha nzito waliziba lango kuu la kuingilia Kanisa Kuu la Anglikan jijini Lusaka ambako Hichilema angeonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu atoke gerezani wiki moja kabla.

“Tumesikitishwa kwa hatua ya kuzuiliwa mkutano wa sala,” alisema Amos Chanda, msemaji wa Rais Edgar Lungu alipozungumza na waandishi wa habari mjini Lusaka.

Hichilema aliachiliwa baada ya kukaa miezi minne gerezani kwa tuhuma za uhaini. Kuzuia kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza kuliashiria uendelezaji wa hatua za kupambana na upinzani unaofanywa na vyombo vya dola vya Rais Lungu.

Hichilema, au “HH” kwa wafuasi wake alikuwa anakabiliwa na tuhuma za uhaini kutokana na madai kwamba msafara wake ulishindwa kuupisha ule wa Rais Lungu mapema mwezi Aprili.

Aidha, Hichilema hadi sasa anapinga ushindi mwembamba alioupata Rais Lungu katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana nadi sasa anakataa kumtambua Lungu kama ni Rais.

Mwezi uliopita Rais Lungu alitangaza hali ya hatari ya siku 90, huku akiwapa polisi nguvu zaidi za kukamata watu na kuwaweka kizuizini akidai kwamba vyama vya upinzani vilikuwa vinahusika katika matukio ya uchomaji moto nyumba kadhaa kwa lengo la kuzusha hali ya vitisho na sintofahamu kwa wananchi.

Msemaji wa Rais alisema “hata katika hali hii ya hatari iliyotangazwa, polisi wanapaswa kuonyesha subira kubwa. Polisi wahakikishe haki za raia haziingiliwi.”

Kwa upande wao maafisa wa polisi walisimamia hatua yao wakidai kwamba waratibu wa ule mkutano wa sala walishindwa kutoa taarifa ya mkusanyiko huo.

Kutokana na hali hiyo, Msemaji hiyo wa Rais alisema hafla nyingine za vyama vya upinzani pamoja na mikutano iendelee kama kawaida.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.