WENZETU WANAKWENDA SAYARI NYINGINE, SISI TWENDE VIJIJINI (1)

Rai - - MBELE - Itaendelea wiki ijayo….0717 809 933

NEIL Armstrong mwana anga mahiri wa Kimarekani, kwa kutumia chombo cha Apolo11, alitua mwenzini salama na kusambaza picha za mwanadamu wa kwanza akiwa mwezini Julai 20, 1969. Hii ilikuwa ni hatua kubwa mno iliyofikiwa na mwanadamu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia katika uchunguzi wa anga za juu.

Baada ya hapo majaribio mengi ya kisayansi katika nchi za Bara la Amerika, Ulaya na Asia yameendelea kufanyika. Kwa upande wa Marekani, wanasayansi nchini humo wapo mbioni kuwapeleka binadamu Sayari ya Mass katika kipindi cha miaka michache ijayo. Hayo ndiyo maendeleo ya kisayansi ambayo nchi za ulimwengi wa kwanza na pili zimeyafikia. Wamefikia hatua hizo baada ya kuboresha hali za maisha za wananchi wao vijijini na mijini. Nchi zetu za ulimwengu wa tatu hususani zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hatujaanza kuota ndoto kufika huko. Sisi bado tunapambana na hali zetu. Naam, bado tunapambana na maadui watatu, Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Wakati Neil Amstrong alipokwenda mwezini na kurudi salama katika ardhi ya dunia, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanganyika huru alitakiwa kutoa maoni yake kuhusu hatua hiyo kubwa ya Marekani iliyofikia katika sayansi ya uchunguzi wa anga. Mwalimu Nyerere alijibu kwa kifupi kabisa. Naye alisema: “Wakati wenzetu wanakwenda mwezini, sisi twende vijijini.” Hiyo ilikuwa mwaka 1969 Taifa letu likiwa na umri wa miaka tisa tu tangu kuanza kujitawala kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.

Ni miaka 48 sasa tangu Mwalimu Julius Kambarange Nyerere atoe kauli na azimio hilo. Mwalimu Nyerere sina shaka kuwa aliona jinsi gani vijiji na miji yetu ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo utatuzi wake ulihitaji mkakati wa dhati uliopangiliwa na kupaniwa na wananchi kwa kushirikiana bega kwa bega na viongozi shupavu katika kutatua kero zinazowakabili wananchi walio wengi.

Aliona kuwa Tanzania hatukuwa na wazo wala uwezo wa kuwekeza katika sayansi na teknolojia kubwa kubwa zisizogusa maisha ya wananchi hususani waishio vijijini, isipokuwa tulichotakiwa ni kuhakikisha tunawekeza katika sayansi za kilimo na viwanda vidogo vidogo zinazohusiana na ukuaji na uondoaji wa umasikini wa kipato wa wananchi waishio vijijini.

Yapo maswali mengi ya kujiuliza; je Tanzania maendeleo yamefika vijijini? Hali za maisha za wananchi waishio vijijini zikoje? Je, viongozi wetu bado wana utashi aliokuwa nao Mwalimu wa kwenda vijijini kuboresha hali za maisha za wananchi?

Ukweli ulivyo ni kwamba, bado kuna hali mbaya sana na tungali tunakabiliwa na changamoto nyingi mno zinazowakabili wananchi waishio vijijini. Nachelea kusema kuwa safari ya kuelekea vijijini imeishia katika stendi za majiji na miji. Pamoja na kuwa na dhamira njema tangu awamu ya kwanza ya utawala, uliodhamiria kuboresha hali za maisha ya wakazi waishio vijijini, dhamira hiyo bado haijatekelezwa kikamilifu hata sasa ikiwa ni zaidi ya miaka 55 tangu tuupate uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yetu kwa kuzingatia vipaumbele vyetu.

HALI HALISI ILIVYO VIJIJINI

Ni ukweli usiopingika kuwa kuna hali duni ya maisha katika vijiji vilivyo vingi nchini kwetu. Wakazi waishio vijijini wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na hali duni za maisha. Wale maadui wakuu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini wana makazi ya kudumu vijijini na wameng’ang’ania mithili ya mdudu ruba ang’ang’aniavyo kwenye ngozi.

Vijijini bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu ya usafiri, maji safi na salama, pembejeo za kilimo, huduma za afya, shule, mabweni ya wanafunzi hususani wasichana, wahudumu wa afya, walimu, manesi na madaktari. Upatikanaji wa bidhaa na hudumu ni shida kubwa.

Vikwazo kama vile miundombinu ya barabara ni moja ya sababu zinazodunisha ukuaji wa maisha ya wakazi wa vijijini. Barabara nyingi za vijijini hazipitiki katika misimu yote ya mwaka. Nyingi ya barabara hizo ni za vumbi na hujaa maji na kuharibika vibaya wakati wa masika. Hii imepeleka hata baadhi ya watumishi muhimu wa Serikiali kama vile walimu, madaktari, manesi, mahakimu na watumishi wa kada nyingine kukwepa kwenda kufanya kazi na kuishi vijijini wakihofia kuwa watapata shida na dhiki kuu pindi wanapotaka kusafiri na ama kupata bidhaa na huduma nyinginezo muhimu.

Miundombinu mibovu ya barabara hupelekea baadhi ya wagonjwa kufia njiani wanapozidiwa na kuhitaji kufikishwa katika vituo vikubwa vya afya. Nina mfano wa kilichotokea katika msimu wa mvua uliopita. Tafarani Milimba, wilayani Kilombero mkoani Morogoro, kulikuwa na dhahama kubwa. Barabara yenye urefu wa kilomita 70 kutoka Mlimba mpaka Ifakara, ili kuharibika vibaya msimu wa masika iliyopita.

Mlimba kuna kituo cha afya, wagonjwa wanaozidiwa na kushindwa kuhudumiwa katika kituo hicho cha afya hukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis ya Ifakara ambako pia palipo na hospitali ya wilaya na makao makuu ya Wilaya ya Kilombero. Kwa kuwa barabara ilikuwa haipitiki au kupitika kwa shida mno wagonjwa wengi walikuwa wakikumbwa na adha kubwa pindi wanapohitaji kupatiwa huduma za afya. Huu ni mfano mmoja tu katika mifano mingi ya ubovu wa miundombinu unavyoathiri maisha ya wananchi maeneo mengi nchini petu. Athari hizo ni za kiafya na hata za kiuchumi ambazo kimsingi zinadumaza ustawi na ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi.

Mathalani, ifahamike kuwa wakulima wengi kama si wote wanaishi vijijini. Pamoja na kwamba wengi wao hutumia jembe la mkono na pembejeo duni za kilimo bado wangali wanakabiliwa na tatizo sugu la bei duni ya mazao yao.

Wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini kwa kuwa sehemu kubwa ya bei ambayo ingelikuwa ni stahiki kwao inatumia kugharamia usafiri kupeleka kwenye masoko makubwa. Kumbe kama kungelikuwa na miundombinu mizuri katika vijiji vyetu wananchi wa vijijini ambao ni wakulima hali zao za maisha zingestawi kwa kuwa wangekuwa na uhakika wa kuuza mazao yao ya kilimo kwa bei yenye tija.

Vijiji vingi wananchi wake kuishi makazi duni, nyumba za tembe na mbavu za mbwa. Si kwamba hawataki kuishi maisha mazuri na katika makazi mazuri, lah hasha, ni kwa sababu kufikia hatua hizo kunahitaji uwezeshaji wa Serikali ambapo uboreshwaji wa miundombinu vijijini, ambao ungepunguza bei ya bidhaa na huduma, pembejeo za kilimo na wataalamu wa fani husika ingekuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa maisha ya wakazi wa vijijini.

ATHARI ZITOKANAZO NA UDUNI WA MAISHA VIJIJINI

Ukipita mitaani kwenye miji na majiji utashangazwa na wingi wa watu. Maelfu ya vijana wamejazana katika miji na majiji yetu. Wengi wao wanafanya biashara za uchuuzi wa bidhaa za viwandani usio na tija.

Vijana hao ambao kimsingi ni nguvu kazi ya Taifa kwanza wangali na uwezo wa kuzalisha, wengi wao wamekimbia ugumu wa maisha vijijini na kukimbilia mjini wakidhani kupata unafuu wa maisha. Kinyume chake wameendelea kuishi maisha duni kwa kuuza pipi na soksi na vijiko shughuli ambazo kimsingi zinawapatia pesa ya kula tu na kuzidi kudunisha hali zao. Kule vijijini wamebaki wazee tu ambao nguvu na uwezo wa kuzalisha umekwisha hivyo Taifa letu kukumbwa na uhaba wa chakula si kwa sababu hatuna ardhi inayofaa kwa uzalishaji wa chakula. Ardhi tunayo tena ni ya kutosha kabisa, tuna maelfu ya hekari zifaazo kwa kilimo, tuna mito, mabwawa na maziwa ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Tatizo ni nini sasa….

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.