Kuingiza sukari nchini kinyemela ni kuhujumu uchumi

Rai - - MAONI/KATUNI -

HABARI za kufurika kwa sukari kutoka nje kwenye maduka, ni habari mbaya kwa Serikali ya Tanzania.

Rais John Magufuli ameazimia kuwa anataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, sio tu kwa ajili ya kupunguza tatizo la ajira nchini, bali pia kutimiza azma ya kitaifa ya kutakaka nchi inayo elekea kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ndiyo maana jitihada zinafanyika sasa hivi ama kuongeza nguvu na uzalishaji wa bidhaa katika viwanda vilivyopo, au kufufua viwanda vilivyobinafsishwa na kutelekezwa, ili vijana wanaokaa vijiweni bila kazi, wapate ajira.

Sukari ni bidhaa ambayo kwa miaka mingi imekuwa inasumbua kwa kuwa upatikanaji wake umekuwa mgumu kutokana na uzalishaji wa viwanda vya ndani kushindwa kutosheleza soko. Lakini viwanda vya sukari vimeitikia wito wa Serikali na kuahidi kupanua ukubwa wa mashamba ya miwa ili kuzalisha sukari zaidi.

Haikuishia hapo. Serikali iliahidi kuagiza sukari kutoka nje, ili kufidia pengo la upungufu wa sukari. Sasa wazalishaji wa sukari — kampuni ya TPC (Tanganyika Planiting Company) ya Arusha Chini, Moshi imetaarifu kwamba katika kipindi kifupi imepoteza soko kwa asilimi 30 kutoka na kuenea kwa sukari iliyoingizwa nchini kimagendo.

Ingawaje bado haijathibitishwa, lakini upo uwezekano kwamba sukari hiyo imeingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Kenya ambayo iliagiza tani 250,000 ikiwa ni mkakati wa kuzima hoja ya ukosefu wa sukari nchini humo — hasa hasa kwa vile suala hili lilifanywa hoja ya uchaguzi mkuu nchini humo uliofanyika mapema mwezi huu.

Tunawaunga mkono wanachama wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari (Tanzania Sugar Producers) ambao wameiomba Bodi ya Sukari nchini (SBT), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufanya uchunguzi na kutoa majibu—sukari hiyo iliyofurika madukani mikoa ya Kaskazini, imeingiaje nchini.

Mchezo huu unaofanywa na wafanyabiashara kutoka Kenya na kushirikiana na Watanzania wanaharibu mipango ya Serikali ya Tanzania na ustawi wa Watanzania kwa vile wanakwepa kulipa kodi.

Tunashauri kwamba viongozi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mara, washirikiane na kuhakikisha kwamba njia zote za uchochoroni kutoka na kwenda Kenya zinadhibitiwa na wafanya magendo watakaokamatwa, wafunguliwe mashitaka ya kuhujumu uchumi wa nchi yetu.

Haiwezekani viongozi wetu wanafanya juhudi za kuipaisha Tanzania kiuchumi, halafu watu wachache — kutokana na uroho wa kujitajirisha haraka haraka, wao wanahujumu jitihada hizo.

Hata kama itajulikana kwamba sukari hiyo iliingizwa kihalali na kulipiwa kodi, itakuwa imekiuka makubaliano ya Jumuia ya Afrika Mashariki(EAC)ambayoyanatamka wazi kwamba bidhaa zitakazouzwa kwenye soko la pamoja, zitakuwa bidhaa zilizozalishwa katika nchi wanachama — sio bidhaa zinazo agizwa na nchi mwanachama kutoka nchi za nje.

Kama wafanyabiashara wa nchi zetu hizi watashindwa kufuata utaratibu huu, ni wazi Afrika Mashariki itaendelea kuwa soko huria la nchi za nje. Nchi wanachama wa EAC zikatae kutumika kwa kusitawisha viwanda vya nje na kuviminya viwanda vya ndani — kama Jumuia hatutaweza kustawi kiuchumi na kijamii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.