Nyanyaso Polisi inaiumiza CCM kwa kuinyanyasa Chadema

Rai - - MAONI/KATUNI - NA BALINAGWE MWAMBUNGU

WAKO viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hawapendi jinsi Jeshi la Polisi nchini linavyowaandama wanachama na viongozi wa chama kikuu cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuwakingia kifua walioleta figisufigisu ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Wanacha hao hawawezi kutamka hadharani kwa sababu wamejawa na hofu kwa kuwa kuna uchaguzi wa ndani wa CCM na tayari uongozi wa juu wa chama hicho umekwishatamka kwamba waliokisaliti na kushabikia upinzani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015, wasipewe nafasi ya uongozi.

Lakini ukweli ni kwamba kuna viongozi wenye kuona mbali, wanajua kwamba hata ndani ya chama chao, kuna makundi chanya na makundi hasi ambayo yametokana na mabadiliko yaliyofanywa baada ya Dk. John Magufuli kuukwaa uwenyekiti wa CCM kitaifa.

Magufuli aliamua kuuvunja mfumo uliozoeleka wa namna ya kuwapata viongozi ndani ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya viongozi katika ngazi ya kitaifa, yaani Halmashuri Kuu na Kamati Kuu za chama. Kwa waliofuatilia kikao cha Mkutano Mkuu Maalumu uliomwingiza madarakani mwenyekiti mpya, ilionekana wazi kwamba wajumbe walijawa na woga. Hakuna aliyenyosha kidole na kupinga mabadiliko yaliyoletwa mezani kwa wajumbe.

Si hivyo tu, baadhi ya vigogo wa chama hicho katika ngazi mbalimbali; ama walipewa onyo au walifukuzwa uwanachama moja kwa moja kwa kuwa walitamka hadharani kwamba hawakuridhika jinsi mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi ya urais ulivyofanyika, wengine wakawa wananung’unika chini chini.

Vigogo wa CCM walioadhibiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msatavangu, wenyeviti wengine ni Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara).

Ukilitazama hili kijuu juu utadhani wameondoka bila kuacha makovu ndani ya chama. Kulipuuza hilo na kudhani kwamba ‘CCM kina wenyewe’ ni kujinasibu bila kutafakari. Kuwafukuza viongozi walioongoza chama au jumuiya ya UWT kwa muda mrefu, halafu ukaridhika kwamba mambo ni shwari, ni sawa na mbuni ambaye akiona tufani linavuma, huchimbia kichwa chake mchangani.

Kama kwamba hiyo haikutosha, CCM pia iliwafukuza wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Ally Khera Sumaye (Babati), Mathias Manga (Arumeru), Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk.Emmanuel Nchimbi, alitakiwa kuomba radhi na Adam Kimbisa (Mjumbe wa Kamati Kuu) alisamehewa. Kimbisa alifanya kazi nzuri ya kuendesha kampeni mkoani Dodoma, ambazo zilikiwezesha chama hicho kuchukua viti vyote vya ubunge.

Wenyeviti wa wilaya waliofukuzwa kwa madai ya kukisaliti chama ni pamoja na Wilfred Soilel Mollel (Arusha Mjini), Salum Madenge (Kinondoni), Makollo Laiser (Longido) na Ally S. Msuya (Babati Mjini).

Assa Simba Haroun (Ilala) aliachishwa uongozi pamoja na Abed Kiponza (Iringa Mjini). Wengine ni Hassan Mzaha (Singida Mkoa), Valerian Buretta (Kibaha Vijijini) na Ajili Kalolo (Tunduru).

Katika mkutadha kama huo, utakuwa mjinga kama utadhani fukuto hilo limekwisha, hasa ukitazama msukosuko wa ndani uliokikumba chama hicho. CCM kimetikisika, hamkani si shwari tena. Kuna fukuto la chini chini ambalo halikufurahishwa na halifurahii jinsi Mwenyekiti Magufuli alivyo kifuma chama na kuwaondoa viongozi wenye ushawishi mkubwa na wenye uzoevu wa uongozi. Pili, hatua ya Rais Magufuli kupiga mikutano ya vyama vya siasa, chama chake ndio kimeathirika zaidi; kwa kuwa dhana ya CCM ina wenyewe, imeonekana si ya kweli. Mtu mmoja tu mwenye madaraka amesema hakuna kiongozi wa CCM atakayeruhusiwa kushika nyadhifa mbili, iwe serikalini au katika chama. Lakini hakuna anayenyoosha kidole na kuhoji: mbona yeye ni Mwenyekiti na pia rais wa nchi? Ingelifaa Magufuli aende mbali zaidi na kuweka bayana kwamba anatakiwa abaki na cheo kimoja tu cha urais ambacho alipewa na Watanzania.

Maneno aliyoyasema Rais Jakaya Kikwete alipohutubia Mkutano wa Jukwaa la Masuala ya Uongozi Afrika (African Leadership Forum) uliofanyika Afrika Kusini wiki iliyopita, yaliendana na hali halisi ya kisiasa ilivyo nchini Tanzania na hapana shaka yamesemwa kwa wakati mwafaka.

Kikwete alitamka bayana kwamba vyama tawala barani Afrika visivibane vyama pinzani kwa kuwa vyama hivyo si adui wao, bali ni mbia muhimu katika kuendesha na kuimarisha demokrasia na utawala bora.

Ni bahati mbaya kwamba kauli hiyo ya rais mstaafu, ameitoa akiwa nje ya nchi, angekuwa ameyatamka akiwa hapa nyumbani, angeeleweka vizuri zaidi. Viongozi mbalimbali wamekuwa wakiwataka viongozi wastaafu kutoa kauli kuhusiana na mustakabali wa kisiasa wa Tanzania, kutokana na ukweli kwamba Jeshi la Polisi limekuwa linawaandama na kuwavuruga viongozi na wanachama wa Chadema, kana kwamba hawana haki yoyote kisheria na Kikatiba kufanya siasa nchini.

Jeshi la Polisi limekuwa likiwanyanyasa wabunge na viongozi wengine wa Chadema na kila uchao utasikia, mbunge fulani au kiongozi wa chama hicho amekamatwa, ameitwa polisi, ameswekwa rumande kutokana na sababu za kipuuzi tu. Mfano halisi ni hatua ya Jehi la Polisi kumuweka rumande Mbunge wa Bunda Mjin, Esther Bulaya (Chadema), kwa kile kilichoitwa kutotii amri ya kutohudhuria mkutano wa siasa wa Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiku ambaye alimwalika mbunge mwezake kumuunga mkono katika kuhamasisha ujenzi wa bweni la wasichana jimboni kwake.

Pamoja na kushindwa kesi kadhaa dhidi ya viongozi wa upinzani, Jeshi la Polisi limekomaa na kuwavuruga wapinzani kana kawamba ni maadui zao. Kila kukicha utasikia kiongozi fulani wa Chadema amefanyiwa hivi, hata hivi juzi Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alikamatwa eti kwa kuzidisha muda wa mkutano kwa dakika saba!

Lakini kwa upande wa chama tawala, mambo ni poa. Hata wabunge wa CCM wakiitana kupeana nguvu katika majimbo tofauti, hakuna shida. Polisi na wakuu wa wilaya, wanashindana kutoa amri dhidi ya viongozi na wanachama wa Chadema, kana kwamba wametangaziwa zawadi kwamba atakayewaadhibu Chadema mara nyingi atapandishwa cheo au kupewa zawadi nono.

Polisi wanadhani wanaibeba CCM, kuumbe wanakiangamiza machoni mwa wananchi ambao wanajiuliza kunani?

Polisi akizungumza na baadhi ya wafuasi wa Chadema

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.