Takukuru iondoke Ikulu, iwe taasisi huru ya kujitegemea KUTOKOMEZA UFISADI NCHINI:

Rai - - MAKALA - NA HILAL K SUED

A

KIMWAPISHA Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wiki iliyopita, Rais John Magufuli amesema iwapo Tanzania itafanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi itafanikiwa kutatua matatizo yake mengi.

Aidha, Rais Magufuli aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

Brigedia Jenerali John Mbungo anakuwa Naibu wa SSP Valentine Mlowola ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru. Bado ni mapema mno kufahamu iwapo kuongozwa na watu waliotoka vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi hiyo inaweza kupata mafanikio makubwa.

Hata hivyo, hakuna ubishi katika kauli hiyo ya Magufuli, pengine labda tu angeongezea kwamba ufisadi pia huweza hata kuleta uvunjifu wa amani na hali ya utulivu. Athari hii imeandikwa, si mahali pengine bali katika sentensi ya kwanza kabisa ya utangulizi (Preamble) ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB Act) ya mwaka 2007.

Hivyo sote wananchi twalifahamu hili, hususani watawala wetu waliotunga sheria hiyo. Lakini cha ajabu ni kwamba ilikuwa desturi kila wanapofanya vitendo vyao vya ufisadi unaosababisha mtikisiko na wananchi kuanza kuja juu na hata kuonyesha kutishia amani iliyopo (kama vile kutaka kufanya maandamano nchi nzima nk), basi watawala hao hao, badala ya kuchukua hatua thabiti ya kuwashughulikia mafisadi, basi huanza kuwatuliza wananchi na kuwahamasisha wafanye ibada kuiombea nchi amani!

Aidha, tafsiri ya ‘ufisadi’ bado inaleta utata kwa sababu sheria hiyo katika kichwa chake cha maneno kinataja ‘rushwa’ (yaani kutoa au kuchukua hongo) na si ufisadi, ingawa huenda ni suala la tafsiri tu. Na tunapozungumzia tafsiri, sheria hiyo haitoi tafsiri (definition) halisi ya neno ‘ufisadi’ (corruption) katika utangulizi wake wa tafsiri ya maneno na vifungu mbalimbali vya maneno.

Ufisadi na changamoto za kupambana na kansa hiyo hapa nchini vilianza tangu wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 70.

Mwaka 1971 Serikali ilipitisha Sheria ya Kuzuia Rushwa (Anti Corruption Act, 1971) lakini sheria hii ilikuja kuanza kutumika miaka mitano baadaye; mwaka 1976 baada ya kuundwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa (Anti Corruption Squad-ACS). Haikueleweka ni kwanini ilichukua muda mrefu kuanza kutumika.

Hata hivyo, ingawa sheria hiyo ilikuwa kali na yenye meno, lakini haikuuma sana, kwa maana kwamba haikuwahi kuibua kesi iliyotikisa nchi; sanasana ilikuwa inakimbizana na ‘vidagaa’ tu vya rushwa kama ilivyo tu katika miongo iliyofuatia.

Mfano mmoja wa ukali wa meno wa sheria ile ni pale ambapo mtumishi wa umma anayetuhumiwa kumiliki mali nyingi, yeye ndiye alikuwa na jukumu la kuieleza mahakama uhalali wa kumiliki mali hizo, huku ikitiliwa maanani kipato chake halali akiwa mtumishi wa umma.

Mwishoni mwa miaka ya 70, kikosi hicho kilihamishwa kutoka Jeshi la Polisi kilichokuwa kama moja ya taasisi chini yake na kupelekwa kuwa chini ya ofisi ya rais.

Hatua hii ilisababisha watu kuinua kope zao na kuibua maswali na kuhoji lengo lilikuwa nini hasa, huku wachunguzi wa mambo wakiona kwamba ni njia ya kuinyima taasisi hiyo uhuru, hasa kutokana na ukweli kwamba mafisadi wakubwa wako katika Nguzo ya Utawala (Executive Branch).

Lakini binafsi siamini iwapo Nyerere alikuwa akiwalinda mafisadi ila tu nadhani walianza kuwa werevu mno katika kuinyamazisha taasisi hiyo, yaani kutoa milungula kwa watendaji wa chombo hicho na vingine vya dola husika kama vile Polisi na Idara ya Mahakama.

Inasemekana iwapo kulikuwapo mtuhumiwa wa ufisadi ambaye alionekana ana uwezo mkubwa wa kifedha, basi Nyerere alikuwa anaomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu iwapo Serikali inaweza kushinda kesi hiyo kama itapelekwa mahakamani. Na baada ya uchunguzi iwapo Mwanasheria Mkuu atasema kuna uwezekano Serikali kushindwa kesi, basi Nyerere humweka mtuhumiwa huyo kizuizini kwa kutumia Sheria ya Kuweka watu Kizuizini (Preventive Detention Act).

Aidha, inasemekana changamoto dhidi ya kupambana na ufisadi kipindi kile ndizo zilizomsukuma Mwalimu Nyerere mapema miaka ya 80, kuanzisha sheria ya Bunge mahakama maalumu ya wahujumu uchumi nje ya mfumo wa mahakama rasmi uliopo Kikatiba.

Alilaumiwa sana na wanasheria wakiwamo majaji, makundi mbalimbali ya wanaharakati wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi, hasa pale sheria hiyo ilipopitishwa baada ya watuhumiwa kutiwa mbaroni sehemu mbalimbali nchini.

Na hata taasisi iliyorithi ACS katika miaka ya 90 yaani Takukuru ilibakia kuwa chini ya ofisi ya rais hadi leo hii, hali ambayo bado imekuwa ikiibua manung’uniko hayo hayo ya kukosa uhuru kamili pamoja na kuwepo kwa sheria mpya iliyopitishwa mwaka 2007.

Na hiki ni kitu kimekuwa kinajionyesha wazi kabisa hasa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya tuhuma ya ufisadi dhidi ya maofisa wakuu wa utawala na kwa Takukuru kuonekana iko katika likizo ndefu isiyoisha.

Kwa maoni yangu tatizo kubwa la taasisi hii si kukosa meno, bali ni kukosa uhuru. Ingefaa Rais Magufuli aliangalie suala hili na kuiondoa kutoka Ikulu na kuwa taasisi ya kujitegemea, isiingiliwe na chombo chochote kile. Bila ya hivyo tutaendelea kuzilea changamoto zile zile.

Majukumu ya taasisi hii huwa yanachanganya sana wananchi, hasa katika mwenendo wake ule wa ‘kutenda’ na ‘kutotenda’ (acts of commission and omission).

Tukiachia mbali ule udhaifu wake unaoeleweka na uliowahi kuanikwa kwa shukrani ya mtandao wa Wikilileaks wa kushindwa kuwafikisha vigogo wa ufisadi mahakamani (kutotenda), kuna hili la taasisi hiyo muhimu mara kadhaa kukubali kutumiwa katika malengo ya kisiasa (kutenda).

Mara kadhaa Chama tawala CCM kimekuwa kikitumia chombo hiki katika kuwekana sawa katika safu zake za uongozi hasa katika chaguzi zake za ndani. Kwa mfano zipo chaguzi za ndani katika chama hicho mwaka 2007 mkoani Arusha na pia katika chaguzi za kuteua wagombea ubunge wa chama hicho kule Tabora, Iringa na kwingineko mwaka 2010). Kadhalika katika chaguzi za ndani za chama hicho mwaka 2012.

Cha kujiuliza ni kwamba kwanini Takukuru huwa haijishughulishi na michakato ya uteuzi wa wagombea, nafasi kama hizo na katika kampeni

za vyama vya upinzani, hususan

katika chama kikuu-Chadema? Inawezekana kweli huwa hakuna rushwa zinazotembea katika michakato yao?

Lakini pengine Tanzania si pekee barani Afrika kwa maudhi yatokanayo na taasisi muhimu za aina hii mbele ya macho ya jamii; kimakusudi kuzifanya kuwa dhaifu na hivyo kutoweza kusimamia haki. Afrika ya Kusini, nchi ambayo baada ya kujikomboa ilichukuliwa kama mfano bora barani Afrika katika kuonyesha uta wala bora baada ya miongo mingi ya ukandamizaji, ilijikuta inaitokomeza taasisi yao ya kupigana na rushwa iliyoitwa Scorpions (yaani ‘nge’) kutokana na matakwa ya wanasiasa walio madarakani kwa lengo la kulinda masilahi yao, pengine kuokoa shingo zao pia.

Inakumbukwa jinsi Scorpions ilivyokuwa inawatetemesha viongozi na maofisa wengine wa Serikali nchini humo bila kujali nafasi zao. Kwa mfano iliweza kumuita, kumhoji na kumfunguliamashtaka aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma (ambaye sasa ni rais wa nchi hiyo) kutokana na tuhuma za kupokea milungula. Lakini pamoja na nuru hii ya utawala bora nauwajibikaji wa nchi hiyo ambayo ilikuwa na kila dalili ya kuchukuliwa kama mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine zilizojikomboa

miaka 40 kabla yake, siasa kama kawaida ziliingilia kati na mashtaka hayo yakafutwa.

Mambo hayakuishia hapo tu, baadaye mizengewe ya kisiasa ilisukwa na kukiandama kitengo hicho hadi nacho kikafutwa na kuundwa kingine ambacho sasa hivi hakina uhuru wala meno, kama ile kawaida wanayopenda watawala wa nchi za Afrika. Iwapo Scorpions ingeachwa kufanya kazi yake bila kuingiliwa na wanasiasa, Zuma asingekuwa rais wa nchi hiyo. Leo hii anatawala huku akibeba tuhuma kebekebe za ufisadi, huku chombo hicho kipo lakini hujikuta kinaingiliwa na siasa.

Si Zuma peke yake, ni wakuu wengi tu barani Afrika (na kwingineko duniani) wangeondolewa madarakani na hata kutinga gerezani kutokana na rushwa na uporaji mali za Taifa iwapo taasisi zao za kupambana na ufisadi zingekuwa na nguvu na kuachiwa kufanya kazi kwa uhuru kabisa.

Hata hivyo, kumetokea wale tunaoweza kusema mashujaa wa vita dhidi ya ufisadi barani humu; wakuu wa taasisi za kupambana na jinai hiyo. Hawa ni John Githongo wa Kenya na Nuhu Ribadu wa Nigeria. Wawili hawa walizikimbia nchi zao kutokana na mikwara na vitisho kutoka kwa viongozi wakuu pamoja na watawala waliokuwa chini ya chunguzi zake na wao kukosa kulindwa na Serikali.

Taasisi yetu iliyopewa kazi hiyo (Takukuru), nikisema kwamba kwa muda mrefu ilikuwa imekwenda likizo ndefu, pengine itakuwa ni kusema kidogo sana. Pamoja na kwamba taasisi hiyo hujigamba kuwa karibu kila wilaya hapa nchini katika ofisi za kisasa, lakini haina habari na ufisadi mkubwa unaoendelea katika maeneo yao isipokuwa kama nilivyosema hapo juu, ni kukimbizana na vidagaa tu vya ufisadi yaani rushwa ndogo ndogo.

Mfano; wiki mbili zilizopita akiwa ziarani Mkoa wa Mbeya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliiagiza Takukuru mara moja kuwakamata na kuwafungulia mashtaka ya ufisadi waliokuwa maofisa na watendaji wa ngazi za juu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuhusiana na gharama za ujenzi wa Soko jipya la Mwanjelwa. Hapa utadhani taasisi hiyo haikuwa na ofisi pale Mbeya.

Na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa waziri wa Serikali anayekwenda kuhutubia mikutano maeneo ya wilayani, hupata tabu pale wananchi wanapotoa vilio vyao kuhusu ufisadi uliokithiri wa watendaji wa halmashauri yao (mkurugenzi na maofisa wengine) na kwamba wanaiomba Serikali iwaondoe.

Swali kubwa ni je, hivi maofisa wa Takukuru katika wilaya hizo wanafanya kazi gani hasa? Tuache huko wilayani na turudi Dar es Salaam ambayo ni makao makuu ya Takukuru.

Miaka minne iliyopita kabla ya ujio wa kimbiza-kimbiza ya Rais John Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aligundua madudu katika Mamlaka ya Bandari (PTA), yaliyosemekana kuwa ni wizi na ufisadi wa kutisha hadi kupelekea maofisa wengine kusimamishwa na baadaye kufukuzwa kazi. Huyo ni mtu mmoja tu aliyefanya kazi hiyo kubwa.

Takukuru walikuwa wapi? Si hapa hapa Dar es Salaam? Bado kuna ubishi hawakuwa likizo ndefu? Itashangaza kusikia kwamba taasisi kubwa kama hiyo hawana watu wanaowabonyeza (informers) kuhusu madudu yanayoendelea kule bandarini.

Na hata baada ya tukio hilo, Takukuru ilirejea usingizini kwani iliona suala la ufisadi kule bandarini ama si lake au limeshatatuliwa na hivyo halipo tena.

Mara kwa mara Takukuru imekuwa inaumbuka katika kashfa kadhaa, kama vile ile ya Wizara ya Maliasili ya utoroshaji wa twiga, ya ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini iliyomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wake, David Jairo, ile ya ufisadi iliyotetemesha Bunge hadi ikapelekea mawaziri kadhaa kuondolewa katika nafasi zao, akiwemo Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na pia ya ununuzi wa mafuta ya Tanesco.

Kashfa zote hizi hazikugunduliwa na Takukuru, bali na taasisi au watu wengine hususan wabunge. Miaka minne iliyopita ilishangaza wengi kuona mbunge tu wa kawaida akipeperusha bungeni nyaraka (barua) iliyoonyesha ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini miaka mitatu iliyopita.

Barua hiyo iliandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, ikiomba ‘michango’ ya fedha (yaani milungula) kutoka taasisi zilizokuwa chini yake kwa ajili ya ‘kuwalainisha’ wabunge ili wapitishe bajeti ya Wizara yake bila dodosa nyingi.

Takukuru ilikuwa haina barua hiyo pamoja na kwamba taasisi hiyo ilikuwa na bajeti yake mahsusi, wachunguzi kila wilaya na maofisa wengine na ‘manusanusa’ kila kona na katika ofisi za umma walishindwa kuipata hati kama hiyo na kuifanyia kazi.

Isitoshe Takukuru inawezeshwa na sheria, ambapo maofisa wake wana uwezo wa kuomba na kupewa mara moja nyaraka yoyote wanayotaka kutoka wizara na ofisi za Serikali.

Lakini hakuna wakati ambapo kauli ile ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Hosea ya kusema taasisi yake ilikuwa ‘huru’ katika shughuli zake, ilipokuja kumsuta sana mwenyewe kama wakati mtandao wa Wikileaks ulipomnukuu akimwambia ofisa mmoja wa ngazi ya juu kutoka Ubalozi wa Marekani hapa nchini, kwamba alikuwa anapata vizingiti ‘kutoka juu’ kuhusu azma yake ya kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wa ufisadi ambao ni vigogo wa Serikali.

Lakini changamoto nyingine kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi ni kule kutupiana mpira kati ya taasisi hiyo na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP).

Utupianaji huu wa mpira mara nyingi umekuwa ukileta tafsiri kwamba lao ni moja tu la kulinda wakubwa katika tuhuma za ufisadi. Lakini cha kujiuliza ni kwamba hawa watendaji si wana mkuu wao aliyowateua, mbona huwa kimya?

Kwa upande mwingine, Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 ina mapungufu muhimu; inatoa ulaini wa adhabu kwa watakaopatikana na hatia, kwani imeweka chaguo (option) la faini kwa mahakimu na majaji, kwamba wanaweza kutozwa faini au kwenda jela wasipoweza kulipa faini au vyote viwili. Mtu kafisadi mabilioni halafu anapigwa faini, si atatumia sehemu ya fedha hizo hizo alizofisadi kulipa hiyo faini?

Hii haiwezi kumaliza ufisadi nchini, kwani haweki ukali (deterrence) wowote. Wanaokumbuka, mwaka 1972 utawala wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ulipitisha sheria iliyoitwa Minimum Sentences Act.

Sheria hii ilitamka kwamba iwapo mtuhumiwa wa makosa ya rushwa na wizi wa mali ya umma atapatikana na hatia, basi hakimu au jaji anayesikiliza kesi hiyo analazimishwa kumpeleka jela kwa kipindi kisichopungua miaka miwili bila ya faini yoyote.

Kwa kumalizia tu hakuna haja ya kutaja hapa kwamba katika kimbiza kimbiza yake hii dhidi ya mafisadi, Rais Magufuli anayafahamu yote haya na hivyo twatarajia atakuwa anachukua hatua stahiki, tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi ya kupambana na rushwa Kenya, John Githongo

Aliyekuwa mkuu wa taasisi ya kupambana na rushwa Nigeria, Nuhu Ribadu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.