Kitovu cha kesi ya uchaguzi Kenya kiko katika maeneo haya

Rai - - MAKALA - NAIROBI, KENYA

“Jukumu la Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya kuendesha uchaguzi wa kuaminika ni muhimu sana na lina changamoto nyingi hivyo lazima litimizwe kwa weledi, uadilifu, na haki na ujasiri. Na pamoja na yote hayo lazima IEBC isipatikane na doa lolote la kutia shaka kutoka kwa wananchi ambao ndiyo inawahudumia. Mengi yanategemewa kutoka IEBC, hususan kuhusu hali ya sasa na ya baadaye ya amani ya Kenya.”

Kauli hii ya kinabii inayogusa myoyo mingi ya wananchi wa Kenya ilitolewa na Mahakama ya Rufaa ya Kenya Juni 23 mwaka huu wakati ilipoamua kwamba Mwenyekiti wa IEBC hana mamlaka yoyote kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa Rais.

Jukumu kubwa la mkuu huyo wa IEBC linaishia katika kupokea matokeo kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi (Returning Officers) kutoka majimbo ya uchaguzi 290, kuyajumuisha, na kumtangaza mshindi.

Hivyo uamuzi huu wa Mahakama ya Rufaa sasa ndiyo umejikita katika kitovu cha kesi iliyopo sasa hivi katika Mahakama Kuu ya Kenya ya kupinga matokeo yaliyotangazwa na IEBC kumpa ushindi Uhuru Kenyatta.

Kulikuwapo vituo 40,833 vya kupiga kura nchini kote. Kufuatana na IEBC, wasimamizi wa uchaguzi katika vituo hivi walikuwa na jukumu la kutuma matokeo, kupitia Fomu 34A kwenda kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo (constituency returning officers) yote 290.

Na hawa wasimamizi wa majimbo 290 walitakiwa kuzipokea hizo Fomu 34A kutoka kwa wasimamizi wa vituo. Na kutokana na IEBC, mchakato huu wa kutuma matokeo kupitia Fomu 34A kwenda kwa wasimamizi wa majimbo hayo 290 haukutakiwa uwe wa kielektroniki. Na katika hali yoyote ile, mchakato huu haukuweza kuwa wa kielektroniki kwa vituo vyote vya kupiga kura kutokana na changamoto za mitandao katika asilimia 25 ya vituo vya kupigia kura.

Na tena kufuatana na IEBC, wasimamizi wa majimbo (Constituency Returning Officers) walitakiwa kuhamisha taarifa kupitia Fomu 34A kwenda kwenye Fomu moja ya 34B. Baadaye walitakiwa kuzihakiki taarifa, kuzijumuisha na kutangaza matokeo ya kila mgombea wa urais alivyopata katika majimbo husika.

Wasimamizi wa majimbo baadaye walitakiwa kutuma taarifa za Fomu 34B kwa njia ya kielektroniki kwenda kwa Kituo Kikuu cha Majumuisho (National Tallying Centre – NTC) kilichopo Nairobi). Kwa hali ya kawaida mchakato huo ni rahisi tu. Kanuni ya 39 (1)(A)(a) ya Kanuni Kuu za Uchaguzi (Election General Regulations) inasema kwamba “kuhusu uchaguzi wa Rais, IEBC itatuma kwa njia ya kielektroniki, kupitia fomu rasmi, majumuisho ya matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka kituo cha kupigia kura kwenda kituo cha jimbo na hatimaye National Tallying Centre (NTC).”

Hivyo “fomu rasmi” kwa ajili ya matokeo yanayotolewa na msimamizi wa kituo ni Fomu 34A. Fomu hii 34A lazima itumwe kielektroniki na kila msimamizi wa kituo kwenda kwa msimamizi wa jimbo na hatimaye kwa NTC.

Kifungu 138(3)(c) cha Katiba ya Kenya kinasema kwamba “katika uchaguzi wa Rais, baada ya kuhesabu kura kwenye kituo cha kupigia kura, IEBC itafanya majumuisho na kuhakiki mahesabu na kuyatangaza matokeo hayo.”

Mahakama ya Rufaa, kupitia kifungu hiki cha Katiba ya Kenya iliamua kwamba “kituo cha chini kabisa cha kupigia kura na hatua ya kwanza katika kuyatangaza matokeo ni kituo cha kupigia kura. Fomu ya kutangaza matokeo hayo ni hati ya kwanza iliyo muhimu, na hati nyingine zote baada ya hii ni majumuisho ya hati hii ya awali iliyoandikwa na msimamizi wa kituo cha kupigia kura.

IEBC imekiri kutokana na hati zilizowasilishwa mahakamani kwamba matokeo ya tarakimu zilizokuwa zikitolewa kielektroniki kupitia mtandao wake uliokuwa ukionyeshwa kwa wananchi yalikuwa ni ya muda tu (provisional) na yalikuwa yamebeba makosa kadha.

Mfano mmoja ni jumla ya mwisho ya kura zilizokataliwa (rejected votes) katika uchaguzi wa rais. Kufuatana na matokeo yaliyokuwa yanatolewa kwa wananchi kupitia mtandao wa IEBC wa kielectroniki, jumla ya kura zilizokataliwa zilikuwa 400,000. Lakini katika matokeo ya mwisho kabisa yaliyotangazwa na IEBC katika Fomu 34C jumla ya kura zilizokataliwa zilikuwa 80,000 tu.

Je, usafirishaji wa matokeo katika kura za urais ulitimiza matakwa ya kisheria? Je namna ya usafirishaji wa matokeo ya urais iliathiri matokeo ya uchaguzi mzima?

Haya na maswali mengine yataamuliwa na jopo la Majaji saba wanaosikiliza kesi hii ya kupinga matokeo iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita na Umoja wa NASA.

Jopo la majaji saba wa Mahakama ya Juu (Supreme Court) linalosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.