Lipumba ‘asulubiwa’

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

Lakini pia, nawaomba wabunge msome Katiba ya nchi kwani inaeleza namna ya kuwapata wabunge na nawahakikishia wabunge hawa wapya wamepatikana baada ya taratibu zote kukamilika.

WABUNGE wa majimbo wa Chama Cha Wananchi–CUF wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Malim Seif Shariff Hamad wameonesha dhamira ya kumsulubu ndani ya Bunge Mwenyekiti wao anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba (pichani). RAI linachambua.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkubwa wa kiuongozi ndani ya CUF unaomuhusisha Prof. Lipumba na Maalim Seif.

Mvutano huo unadaiwa kukiathiri chama hicho hasa kwa upande wa Maalim Seif kutokana na hoja kuwa upande wa Prof. Lipumba unasaidiwa kwa karibu na Serikali.

Hoja hiyo inahalalishwa na uamuzi wa haraka uliofanywa na Bunge na Msajili wa vyama vya Siasa nchini baada ya kuridhia kwa haraka kutimuliwa kwa wabunge nane wa viti maalum wa chama hicho waliokuwa upande wa Maalim Seif.

Mara baada ya Bunge kuridhia uamuzi huo, ofisi ya Msajili ilipitisha majina manane ya wabunge wa viti maalumu yaliyodaiwa kupelekwa na upande wa Prof. Lipumba, wabunge hao waliapishwa juzi ndani ya Bunge.

Kuapishwa kwa wabunge hao kuliibua hasira ya wabunge wa CUF wanaomuunga mkono Malim Seif kwa kushirikiana na wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kuwasusa na kuahidi kutowapa ushirikiano wenzao kwa kile walichodai kuwa hawakustahili.

Mbunge wa Momba, David Silinde ambaye pia ni Katibu wa Kambi ya Upinzani bungeni, alisema waliamua kutoingia wakati wa zoezi la kuwaapisha wenzao likiendelea kwa sababu hawakubaliani na uamuzi uliochukuliwa dhidi ya chama hicho.

“Sababu kubwa ya kutoingia wakati wakiapishwa wabunge baadhi, tunapinga Bunge kutumika na Serikali kwa kukandamiza upinzani pamoja na kutofuata sheria za nchi, lakini kubwa zaidi ni kuwaunga mkono wabunge wote walioondolewa.

“Hatuko tayari kufurahia hatua ya Serikali kufurahia chama chenye migogoro kwa kupendelea upande mmoja na kukandamiza upande mwingine.

“Hii ndio tumekuwa tukionesha siku zote, hatutaki kuona Bunge liendelee kutumika, tunataka Bunge liwe imara, waone kama ilivyotokea kule Kenya kwa mahakama kusimama peke yake na sisi tunataka Bunge lisimame peke yake.

“Tunauona udhaifu mkubwa katika Bunge na tutaendelea kupinga siku zote tukiendeelea kukaa hapa bungeni na hilo ndilo jambo kubwa ambalo Watanzania wanatakiwa kufahamu na sisi hatutashirikiana na wabunge hawa hadi pale kesi ya msingi itakapoisha mahakamani,”alisema Silinde.

Kwa upande wake Mbunge Juma Kombo Hamad ambaye pia ni Katibu wa wabunge wa CUF alisema wanalalamikia kutofuatwa kwa misingi ya sheria katika mchakato wa kuwasimamisha wabunge wenzao nane.

“Kimsingi tumejumuika kwa pamoja kama kambi ya Ukawa, lengo letu ni moja tu kupaza sauti zetu kwa kudai haki kwa sababu mchakato wa kuwafukuza wenzetu umekwenda kinyume kwa sababu bado kuna kesi za msingi zinaendelea na kwamba ingekuwa jambo la busara kusubiri kesi ziishe ndipo maamuzi yachukuliwe.”

Kombo aliahidi kutoshirikiana kabisa na wabunge walioapishwa na kwamba hawatafanya hivyo hadi pale haki ya kisheria itakapopatikana.

Uamuzi huo wa kuwasusia wabunge wa CUF ya upande wa Prof. Lipumba umekuja ikiwa ni wiki moja imepita baada ya wabunge 19 wa chama hicho kufungua shauri Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam wakimzuia mwenyekiti wao asiwachukulie hatua za kinidhamu wabunge, madiwani na viongozi wengine hadi mashauri yaliyopo Mahakamani juu ya uhalali wa uongozi wa chama yatakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Katika kikao cha kwanza cha mkutano wa nane wa Bunge, wapinzani hawakuingia ndani ya ukumbi wa Bunge isipokuwa wabunge watatu wa CUF wanaomuunga mkono Lipumba.

Katika kikao hicho wabunge wa upinzani wanaounda Ukawa walivalia nguo nyeusi wakimaanisha masikitiko kwa yanayoendelea bungeni.

SAKAYA: HAWAJUI WALITENDALO

Kufuatia kadhia hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho ambaye pia anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Magdalena Sakaya alisema amewashangaa wabunge hao na kuongeza kuwa hawajui wanalolifanya.

Akizungumza na RAI juzi, Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua alisema wabunge wa CUF walioteuliwa kuingia bungeni hawakuja kutafuta ushirikiano kwa mtu bali wamekuja kwa ajili ya taifa.

“Kwa hiyo hawakuja ili wamnufaishe yeyote wala chama chochote, jukumu walilopewa ni heshima ya kuwa mbunge wa chama, kwanza atumike kwa ajili ya taifa, wananchi waliowatuma na chama ndani ya bunge.

“Kitendo cha kutoka nje ya Bunge wakiwa wamevaa nguo nyeusi na kusema, ‘eti hatutatoa ushirikiano’ kwani wao ni spika kwamba watawanyima nafasi ya kujibiwa maswali yao bungeni au serikali! sioni wanalolisema kwa sababu unapofika bungeni pale unakuja kutetea wananchi na kuhoji serikali juu ya maendeleo ya wananchi waliokutuma.

“Unayemhoji ni serikali hauwezi kumhoji mbunge yeyote CCM wala Chadema. Lakini pia unakuja pale unahitaji Spika afuate kanuni kama ni muswada, ni sheria, ni maswali au hoja iliyopo mezani. Kwa hiyo huhitaji mtu yeyote kujenga hoja yako. Kama wewe mwenyewe umejipanga unajua unazungumzia nini.

“Kwangu mimi nawaona kama hamna kitu kwa sababu tangu mwaka jana walisema ‘Sakaya ameamua kutetea katiba ya chama chake tunamtenga’, licha ya kunitenga tangu mwaka jana sasa wamenufaika nini au mimi nimefaidika nini kunitenga kwao?. Hamna kitu hawajui wakifanyacho ni uwezo tu wa kufikiri na kuchanganua mambo” alisema Sakaya.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alisema wabunge hao saba walikula kiapo baada ya taratibu zote kukamilika.

“Kwanza kabisa, napenda kuwapongeza wabunge wote wapya ambao awali mlikuwa wabunge wateule na sasa mmekuwa wabunge kamili. Bunge litawapa ushirikiano wote na naomba wapewe fomu za kuchagua kamati wanazotaka ili waanze kazi leo leo.

“Lakini pia, nawaomba wabunge msome Katiba ya nchi kwani inaeleza namna ya kuwapata wabunge na nawahakikishia wabunge hawa wapya wamepatikana baada ya taratibu zote kukamilika,” alisema Ndugai.

Habari kutoka katika viunga vya Bunge zilibainisha kuwa Profesa Lipumba amedhamiria kuwaandikia barua za onyo kali wabunge wote walioshiriki kususa kuingia bungeni pindi wenzao walipokuwa wakila kiapo.

“Bwana anakusudia kuwaandikia barua za onyo kali wabunge wote wa CUF waliotoka nje ya Bunge juzi (leo) wakiungana na wenzao wa UKAWA kwa kile walichodai kutowatambua wabunge wa Profesa wanaoapishwa,” alisema mmoja wa watoa taarifa.

MAHAKAMA KUMNYIMA LIPUMBA NGUVU?

Hata hivyo, lengo hilo la Lipumba kuwaandikia barua ya onyo kali wabunge hao linaweza kukwama kutokana na shauri ambalo wabunge 19 wa CUF wamefungua Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam wakimzuia Mwenyekiti wao asiwachukulie hatua za kinidhamu.

Wabunge hao 19 wanaodaiwa kuwa upande wa Maalim Seif, mapema wiki iliyopita waliiomba mahakama itoe nafuu kwa kuwalinda na kuwaacha watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi mpaka hapo mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi na kumalizika.

Akizungumza na RAI juzi, Msemaji wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande alisema shauri hilo namba 69/2017 linatarajiwa kutajwa kesho mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera.

Wabunge wa CUF walioapishwa mapema juzi ni Alfredina Kahigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.

Wabunge hao ndani ya Bunge mbali ya kushangiliwa na wabunge wa CCM pia waliungwa mkono na Sakaya, Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma.

UAMUZI WA LIPUMBA

Julai 24, Lipumba alitangaza kuwavua uanachama wabunge hao na Julai 25, Spika ndugai akatangaza kupokea barua ya Lipumba, Julai 26, akatoa taarifa iliyoeleza kuridhia kufutwa uanachama kwa wabunge hao na ilivyofika Julai 27, Tume ya Tiafa ya Uchaguzi (Nec), kitangaza majina nane ya wabunge wapya kuziba za waliondolewa.

Wabunge nane waliotangazwa kuvuliwa uanachama na Profesa Lipumba ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally AlQassmy na Halima Ali Mohamed. Madiwani ni Elizabeth Sakala na Layla Madiba.

Miongoni mwa makosa yaliyofanya wabunge hao kufukuzwa, ni pamoja na kukihujumu chama katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa Januari 22, 2017 na kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho (Lipumba).

Makosa mengine ni kumkashifu Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na wakurugenzi wa chama hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.