Nakulilia Muhingo Rweyemamu

Rai - - MBELE -

ASUBUHI ya Septemba 2, mwaka huu nilijulishwa juu ya kifo cha gwiji wa habari, Mhariri nguli na Mkuu wa Wilaya wa zamani wa Handeni (Tanga), Makete (Iringa) na Morogoro Mjini (Morogoro), Muhingo Rweyemamu. Tangu nilipofahamishwa kifo chake asubuhi hiyo,

ASUBUHI ya Septemba 2, mwaka huu nilijulishwa juu ya kifo cha gwiji wa habari, Mhariri nguli na Mkuu wa Wilaya wa zamani wa Handeni (Tanga), Makete (Iringa) na Morogoro Mjini (Morogoro), Muhingo Rweyemamu.

Tangu nilipofahamishwa kifo chake asubuhi hiyo, nilibabaika kidogo kana kwamba nilikuwa ninaota njozi. Nilipatwa na mshtuko ambao kwa hakika nashindwa kuelezea. Zilipita saa 5 kuamini habari ile kuwa Muhingo hatunaye duniani. Nilijiuliza kuugua sawa, mbona mambo yamekwenda kwa kasi namna hii?

Baadaye nikakumbuka maandiko yake yaliyopo kwenye maktaba yangu. Nikakumbuka siku niliyomtumia picha ya makala aliyowahi kuandika huko nyuma. Jawabu lake lilikuwa fupi tu, “Mpangala, asante kwa kunikumbusha. Kwa kweli ni mengi yamepita.”

Mathalani nilikumbuka maandiko yake aliyowahi kuyachapa katika safu ya Fikra Pevu. Miongoni mwake ni ‘Tulianza kuwa wajinga tulipopelekwa shule’, ‘Mbuzi wa tatu yuko wapi?, ‘Niache Niseme kama Mwendawazimu’ na yale maandiko maridadi ya “Ubongo wa Mjusi”.

Kwenye maandiko yako ya ‘Mbuzi wa Tatu yuko wapi’, Muhingo Rweyemamu uliandika hivi: “Leo nawapa mfano wa Mbuzi namba tatu. Mfano huu kwangu huwa ni somo kubwa kwa mahusiano ya kikazi na kimaisha.

“Hebu nikueleze kidogo na wewe kwani linaweza pia kuwa darasa kwako. Je, umewahi kuhangaikia jambo ambalo huna na ukapuuza kile ulicho nacho?

“Katika shule moja ya sekondari Jumapili moja jioni, vijana wawili watukutu waliwazingira mbuzi watatu toka katika banda la jirani. Kisha wakawapaka rangi kwa kuwatia namba 1--2--4. Vijana hao wakawakimbizia mbuzi hao kati eneo la shule.

“Kesho yake asubuhi wakati viongozi wa shule walipoingia shuleni walisikia harufu isiyo ya kawaida. Baadaye wakaona kinyesi cha mbuzi kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo lao na hivyo wakahisi kuna mbuzi kwenye jengo hilo.

“Uchunguzi ukaanza na mara wakafanikiwa kuwakuta mbuzi watatu. Uongozi wa shule ukasema mbona mbuzi ni watatu badala ya wanne. Wakaulizana yuko wapi mbuzi namba tatu? Walitumia siku nzima wakimsaka mbuzi namba tatu.

“Watu wote tangu walimu, wanafunzi, wapishi, makarani na wote shuleni wakatoka kutafuta mbuzi namba tatu ambayo haikupatikana na kimsingi hakuwepo.

“Hivi ndivyo tulivyo. Inawezekana tunayo malengo yetu ya kutimiza lakini tuko obsessively looking for the elusive missing, non-existing goat number three.

“Badala ya kutumia vipawa au vitu tulivyo navyo tunabaki tukihangaikia vitu au sifa ambazo hatuna.

“Kama wafanyakazi iwe katika shirika, taasisi binafsi, ya umma au kwingineko ina frustrate mkiwa na kiongozi anayetafuta mbuzi namba tatu muda wote.

“Kwa mawazo yangu mafanikio yanakuja pale tu tunapojitahidi kutumia vile tulivyo navyo na tukaacha kuhangaika na vile ambavyo hatuna na wala hatuwezi kuvipata. Alamsiki.”Namzungumzia mtu niliyemfahamu katika nyakati za makuzi yangu ya fani ya uandishi wa habari. Kwa hakika yapo maandiko mengi, lakini binafsi ninavutiwa zaidi na hayo kiasi kwamba yamenitawala.

Mtu aliyewahi kunipa jukumu la kuhakikisha tunakuwa na habari za kipekee kuhusu bara la Afrika kila wiki. Mtu ambaye aliwahi kunihoji kwanini wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waligoma (mwaka 2008). Na kuanzia hapo ndipo tukafanya mazungumzo juu ya Kamati iliyowahi kuundwa kuhusu kuangalia kiini cha migogoro ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vingine.

Ninakumbuka mojawapo ya misingi yake juu ya uandishi wa habari dhidi ya uandishi wa raia. Hakuwahi kuogopa uandishi wa raia (Citizen Journalism) ambayo sasa imekuwa na nguvu kuliko miaka 10 iliyopita.

Muhingo alikuwa mwalimu halisi. Mwalimu wa fani ya uandishi wa habari. Ni Mwalimu kama taaluma aliyoanza nayo kabla ya kuingia ya habari. Pengine ualimu ndiyo ulimfanya azidi kukipenda kilimo ambacho wakati wote alisisitiza. “Kuwa mkulima ni kuchagua amani ya moyo,” alisema.

Nakulilia sana Muhingo. Nakulilia kwa sababu nyingi mno kitaaluma na maisha ya kawaida. Hukuchosha kuelimisha ingawa ulichagua kupumzika kuandika mara kwa mara.

Nakumbuka mjadala wetu mkali tuliowahi kufanya ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, ulikuwa juu ya “Mshahara wa Rais wa nchi”. Ulinipinga kuwa hakuna sababu za kuweka bayana mshahara wa rais wa nchi. Ukanihoji: “Hivi Markus ukiujua mshahara wangu utakusaidiaje?

Ninakumbuka nilikwambia, nchi yetu hii isiendeshwe kana kwamba mshahara ni suala la siri sana (hata kama makubaliano yanasemwa kuwa ni ya siri). Nikasema kwangu haina madhara yoyote isipokuwa tumezoea hivyo. Mwishowe ukaniambia saidia jamii kuinuka katika mazingira duni kwenda juu ila mshahara wa rais hauleti chochote mezani.” Nilitii.

Nakulilia nikikumbuka falsafa yako ya kutochukua wanafunzi waliofaulu sana ambao walikataa kwenda shule walizopangiwa serikalini ili ajiunge na shule yako. Ulitaka wale wenye ufaulu hafifu wajiunge na Hope Schools. Ulileta mapinduzi na maajabu.

Kifo chako kimenihuzunisha Muhingo Rweyemamu. Nimesononeka mno. Nimetafakari mengi tuliyopita na kupanga. Nathamini mafunzo yako katika mapito yangu kwenye fani hii. Uliniita na kunisahihisha. Ulinikemea na kuniadhibu.

Ulinipitisha kwenye changamoto kubwa sana kuwahi kutokea maishani mwangu. Natanguliza kukuomba msamaha kwa pale niliposumbua juu ya mpango wetu wenye masilahi ya kizazi chetu na kijacho. Hatukutekeleza tulichopanga baada ya rais mstaafu Jakaya Kikwete kukupa jukumu huko mkoani Tanga. Nilikuuliza sasa, tunafanyaje umetwishwa mzigo mwingine? Jawabu lako lilikuwa rahisi: “Kwanza nimeanza kuwakusanya wakuu wenzangu ambao ni wanataaluma. Nimewashawishi. Wameafiki, ingawa wengine bado. Tutakamilisha tu bwana mdogo.”

Majukumu yaliyokuwepo yalipunguza muda wa kufikiria tulilopanga. Lakini nilitambua kuwa ni kwa masilahi ya nchi yetu. Leo hii hadi umeaga dunia hatukuweza kutekeleza suala lenyewe. Sikulaumu, ulilitumikia taifa lako vilevile.

Nakumbuka maandiko yako yalivyozusha mjadala baada ya mgomo wa UDSM mwaka 2008 kupitia safu ya ‘NILONGE NISILONGE’. Bahati mbaya siku hizi hakuna mijadala hiyo, tumebakiwa na ‘Itikadi’ za vyama vyetu tu. Nimefilisika maneno. Umetangulia mwaka huu, kama nilivyomtanguliza mama yangu hapo Februari. Ninaamini mtakutana huko, mwambie ‘natekeleza, sirudi nyuma.’

Pumzika kwa amani Muhingo. Nikimwona Kambi Mbwana huwa nakuona. Pole sana Shilengile. Poleni akina Rweyemamu.

Nakulilia nikikumbuka falsafa yako ya kutochukua wanafunzi waliofaulu sana ambao walikataa kwenda shule walizopangiwa serikalini ili ajiunge na shule yako. Ulitaka wale wenye ufaulu hafifu wajiunge na Hope Schools. Ulileta mapinduzi na maajabu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.