Madiwani Chadema, CCM waungana

Rai - - MBELE - NA WAANDISHI WETU

KATIKA hali isiyo ya kawaida madiwani 32 wanaounda Baraza la madiwani Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wameungana ili kumng’oa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Peter Maloda. RAI linaripoti.

Uamuzi wa madiwani hao kuunganisha nguvu ili kumng’oa Maloda unatokana na tuhuma za ubadhirifu, ubabe na matumizi mabaya ya madaraka ya kiongozi huyo.

Tayari madiwani 32 kati ya 50 wanaounda baraza la Madiwani wamedhamiria kumng’oa Maloda. Muungano huo unajumuisha madiwani 29 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na watatu kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Madiwani hao wameshamwandikia barua Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Revocutus Kuuli kuomba kikao cha kumjadili Mwenyekiti wao kwa lengo la kumwondoa katika nafasi yake.

Hoja ya wanaotaka Maloda ang’oke ni kwamba utendaji wake haufuati kanuni na taratibu za uongozi.

Akizungumza na RAI mmoja wa madiwani hao ambaye pia ni Mbunge wa Manonga wilayani Igunga, Seif Gulamali alikiri kutokubaliana na utendaji wa mwenyekiti huyo kwa kuwa ni mbabe, anadharau na mbadhirifu hali iliyochangia kuibuka kwa migogoro ndani ya halmashauri hiyo.

“Mwenyekiti ameshindwa kusimamia kiasi cha Sh milioni 40 ambazo zilipitishwa na baraza

la madiwani April 29 mwaka jana kwa ajili ya ukarabati wa bwawa la Bulenya ambao imeonekana wazi kazi iliyofanyika hailingani na thamani ya pesa hivyo kuzua hofu kuwa huenda kiasi kikubwa cha pesa kimetafunwa. Pia ametumia kiasi cha Sh milioni 23 kwenda kufuata madawati yaliyotolewa na Bunge pasipo fedha hizo kuidhinishwa matumizi yake na Baraza la Madiwani kupitia kamati ya fedha.

“Ameshindwa kusimamia na kufuata mwongozo wa Wizara ya Elimu wa matumizi ya kiasi sh cha milioni 198 za ujenzi na ukarabati wa shule ya msingi Chipukizi. Ameshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ndani katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba,” alisema.

Aidha, madiwani hao walisema kuwa Mkurugenzi halmashauri hiyo anamlinda Mwenyekiti huyo kwa kuwa licha ya kumwandikia barua ya kumtaka kuitisha kikao cha kumjadili mwenyekiti, hadi sasa hajatekeleza wito huo.

Akizungumzia tuhuma hizo mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Peter Maloda, alisema tuhuma zote zinatokana na hila za kisiasa hivyo hakuna ukweli wowote.

“Ni kweli Baraza la madiwani ninaloliongoza limegawanyika vibaya mno. Tumekosa sauti ya pamoja. Tumebaki kutuhumiana tu mambo yasiyo ya kweli. Haya yote ni mambo ya kisiasa tu na uchu wa madaraka, yupo mtu anataka nafasi yangu au anataka kuniondoa ili amsimike mtu wake.

“Tena ni huyu Mbunge wa jimbo la Manonga, Seif Gulamali. Yeye anataka mimi niharibikiwe ili ampandikize mtu wake katika nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri. Nasikitika kuona Chama chetu CCM, hakioneshi utashi wa kushughulikia mgogoro huu” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Revocutus Kuuli naye alikiri kuwepo na mgogoro huo katika Halmashauri yake na kukitaka CCM kuingilia kati.

“Mgogoro upo. Madiwani wamegawanyika kabisa. Unajua hata katika uchaguzi wa kumpata makamu mwenyekiti wa Halamashauri, kura 21 zilipigwa za hapana na kura 3 ziliharibika, hii ni kwa kuwa hawa madiwani licha ya kuwa ni wa chama kimoja CCM, lakini wamegawanyika mno.

“Lakini hayo ni mambo ya kisasa tu. Kubwa zaidi mimi nipo imara na ninachapa kazi. Tuhuma ambazo wananituhumu kuwa ninamlinda Mwenyekiti hazina mashiko ya kisheria. Waaambie wasome sheria na kanuni zinasemaje. Wasibaki kunituhumu bila kusoma kanuni na kuzielewa,” alisema.

RC MBEYA AWASHUKIA

Wakati hali ikiwa hivyo Mkoani Tabora, kwa upande wa mkoani Mbeya mambo ni tofauti kwani Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla amewanyooshea kidole madiwani na watendaji wa halmashauri mkoani huo kwa kushindwa kutambua wajibu wao na kukubali kurubuniwa kwa posho ndogondogo.

Makala pia amepiga marufuku wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutoka nje ya mkoa kwenda kushiriki mafunzo mbalimbali zikiwemo warsha, semina na makongamano hadi pale mkakati huo wa uwezeshaji wananchi kiuchumi utakapokamilika.

Alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Mji wa Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine pia alitishia kwenda kuwashtaki madiwani hao kwa wananchi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Alisema madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi wamekubali kununuliwa na watendaji kwa posho ndogondogo za vikao na kuwasahau wananchi wanaowatumikia wakiendelea kuteseka kutokana na kushindwa kusimamia shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo miradi ya maendeleo.

Aliwataka madiwani hao kufanya kazi na kutimiza wajibu wao kwa wananchi badala ya kuendekeza siasa za kimasilahi.

“Serikali ipo katika harakati za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuanzisha na kuviendeleza viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na wakati, lakini jitihada hizo zinaweza kugonga mwamba kutokana na uzembe wa madiwani.

“Diwani anapaswa kujiuliza kwamba tangu ameshika nafasi hiyo ya kuwatetea wananchi, ni jambo lipi kubwa la maendeleo amelifanya? Serikali inahamasisha uchumi wa viwanda, je, tayari ameshirikishwa na watendaji juu ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi hayo au amekaa akisubiri kuletewa taarifa kwenye vikao ambavyo asilimia kubwa ni za uongo na wakati mwingine zimekuwa ni chanzo cha migogoro na wananchi?

“Wewe ni diwani wa aina gani ambaye hufahamu jambo lolote linaloendelea katika halmashauri unayoingoza au nyie kazi yenu ni kukataa taarifa za watendaji kwa msingi kwamba hamjashirikishwa? lakini hapo mnaowachelewesha ni wananchi kwani wajibu wenu mnaufahamu,” alisema.

Alisema endapo madiwani watayaelewa maeneo yaliyotengwa na viwanda vinavyojengwa ni vya aina gani, au kufahamu halmashauri zina fursa gani wataweza kushawishi watu kuwekeza na sera ya uchumi wa viwanda itawanufaisha wananchi.

Alisema kwa muda mchache ambao amezitembelea halmashauri za Mkoa wa Mbeya, amegundua kwamba madiwani walio wengi hawafahamu shughuli za maendeleo zinazofanyika ndani ya halmashauri wanazoziongoza na hilo ni tatizo kubwa.

Alisema kinachomshangaza ni kwamba madiwani ndio wameshika hatimiliki za halmashauri kwa kuwa baraza la madiwani ndilo linalofahamu kwamba katika eneo lao kuna ardhi ambayo itaweza kukidhi mahitaji ya uwekezaji ikiwa eneo hilo halikabiliwi na changamoto yoyote ikiwemo migogoro ya ardhi.

“Unajua kazi kubwa inayofanywa na watendaji wetu ni kutuletea takwimu za maeneo lakini takwimu hizo unakuta hazijashirikisha madiwani ambao ndio wanaoishi na jamii kila siku, ikiwa ndio wanaoshiriki kwenye vikao vya kamati za maendeleo ya kata na mwisho wa siku mwekezaji anapatiwa eneo lakini mgogoro nao unaibuka,” alisema.

Alisema ili kuondokana na migogoro ya ardhi katika kipindi hiki cha utekelezaji wa uchumi wa viwanda, madiwani wanapaswa kukaa na watendaji na kupanga mipango ya maendeleo endelevu na yenye tija.

… MARUFUKU KUSAFIRI NJE YA MKOA

Aidha, katika kuhakikisha suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linafanikiwa, Makalla pia alipiga marufuku kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutoka nje ya mkoa kwenda kushiriki mafunzo mbalimbali zikiwemo warsha, semina na makongamano hadi pale mkakati huo wa maendeleo utakapokamilika.

Alisema wakati mchakato huu ukiendelea, ni vema wakuu hao kwa kushirikiana na madiwani wakawajibika moja kwa moja badala kukaimisha nafasi zao ili kusaidia usimamizi mzuri.

“Sasa hawa wakishapigwa ‘pini’ ya kutoka ni lazima wao wasimamie utekelezaji wa shughuli husika na kubaini nani anahusika na uzembe wowote utakaojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango wa uwezeshaji kiuchumi.

“Ni lazima watendaji wakawashirikisha madiwani ili waelewe mpango wa kutenga maeneo kwani wao ndio wana uwezo mkubwa wa kuyafahamu maeneo, ikiwamo kupendekeza ni aina gani ya uwekezaji wanaoutaka kwenye maeneo yao,” alisema.

Hata hivyo, akizungumzia suala la asilimia 10 ambazo zinatakiwa kutolewa na halmashauri kwa wananchi, Makalla aliwataka madiwani kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema mabaraza yamekuwa yakipokea taarifa ya robo mwaka lakini ndani ya taarifa hiyo ni vema madiwani wakajihakikishia kama asilimia 10 za kuwawezesha wananchi kiuchumi zimeainishwa.

“Asilimia 10 hizo ni lazima zitolewe kwa wananchi kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii na hazina mjadala wala mvutano, lakini kama nyie madiwani mtanyamaza basi mtambue kwamba mnawakosesha haki ya msingi na ya maendeleo wapigakura wenu.

“Pia, fedha hizo zinatakiwa kutolewa kwa uwazi, kwani mnaweza kujikuta vikundi hewa vikanufaika na pato hilo la ndani linalokusanywa na halmashauri badala ya walengwa husika.

“Fedha zinapotolewa kwa wajasariamali ni lazima zitolewe kwenye maeneo husika kupitia mikutano ili kuweka uwazi, wakati wa kufanya mambo kimya kimya ndio mwanzo wa kunufaisha watu ambao si walengwa,” alisema.

Alisema tatizo lililopo ni pale madiwani wanapotanguliziwa posho za vikao, wanasahau kabisa wajibu wao kwa wananchi.

“Badala ya kusimamia na kuhakikisha fedha hizo zimetolewa kwa wahusika, sisi tunakaa na kusubiri tuletewe taarifa ambazo naweza kusema nyingi zimejaa ubabaishaji. Madiwani watakaoridhika na taarifa za mezani ni kwamba wameshindwa kufanya kazi yao hivyo wasijeshangaa kazi hiyo ikifanywa na watendaji wa Serikali,” alisema. … Nitawashtaki kwa wananchi Aidha aliwaonya madiwani hao kuwa atatembelea kata moja baada nyingine kuwashtaki madiwani hao kwa wananchi kuwa wameshindwa kazi.

“Binafsi nitapita kwa wananchi kuwashtaki kwani wajibu wenu mnautambua, lakini mnafanya makusudi kupotezea kutokana na virushwa vya posho mnavyohongwa na watendaji, fanyeni kazi, timizeni wajibu wenu kwa wananchi waliowachagua na kuwaamini,” alisema.

Aidha, alisisitiza kutokuwa na utani na suala hilo na kwamba ni lazima madiwani wazembe washtakiwe kwa wananchi na kwamba kazi hiyo ataifanya yeye mwenyewe kwa kupita kila kata.

“Mimi nitakwenda kuwashtaki kwa wananchi, uwezo wa kupita kila kata kuwaambia wananchi halmashauri yenu ina mapato kiasi hiki lakini hamjapata fungu lenu ni nao na hili linatokana na uzembe wa watu mliowachagua kuwawakilisha, haijalishi diwani wa Chadema wala wa CCM, kwa sababu mmeshindwa kuwapigania,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Victor Makinda, Tabora na Pendo Fundisha, Mbeya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.