WENZETU WANAKWENDA SAYARI NYINGINE, SISI TWENDE VIJIJINI (2)

Rai - - MBELE -

Toleo lililopita la gazeti hili kongwe pendwa la RAI Nguvu ya Hoja, nilianza makala haya ikiwa ni sehemu ya kwanza. Nilielezea baadhi ya changamoto zinazokabili maeneo mengi katika vijiji vya nchi yetu na kwanini tunatakiwa kwenda vijijini na kuviangazia vijiji vyetu kwa jicho la kukabili changamoto hizo ili kufikia maendeleo.

Shukrani kwa wasomaji wangu ambao hamkuishia tu kusoma bali mlikwenda mbali zaidi na kunitumia jumbe mbalimbali za kunipongeza na hata baadhi kunikosoa kulingana na mitazamo binafsi. Kazi ya fasihi ili ujue kuwa imepata hadhira ni lazima upate mrejesho kutoka kwa hadhira hiyo. Mrejesho niliupata umenipa picha kuwa ‘chakula’ nilichopika kimepata walaji. Walaji wangu baadhi wamepongeza utamu wa chakula na wengine wamekosoa ladha ya chakula kwa kutoa kasoro ndogo ndogo, mara ooh, chumvi ilikuwa kidogo, mara ooh…chakula kibichi kwa mbali, lakini kubwa zaidi chakula hicho kimepata walaji.

Msomaji wangu ayejitambulisha kwa jina la Fredrick Kinemo akiwa Turiani Morogoro, yeye amenipongeza kwa makala nzuri. Ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa wakati anasoma makala hayo, picha za vijiji vingi ilimjia kichwani. Anakumbuka vijiji ambavyo amewahi kuishi. Anasema kuwa pamoja na jitihada nyingi na kubwa za Serikali, bado hali halisi ya maisha ya vijijini yanakabiliwa na changamoto lukuki.

Kinemo anasema anao mfano mmoja wa vijiji katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, binadamu wanatumia maji katika Bwawa moja na mifugo. Kijiji hicho hakina chanzo cha maji, hivyo wananchi wanatumia maji ya bwawa kwa kunyweshea mifugo, kufulia, kuoshea vyombo, kupikia na hata kunywa maji hayo hayo.

Nionavyo huu ni mfano mmoja katika mifano mingi ya vijiji vyetu. Ndiyo! Hali ni mbaya kupita kiasi. Vipo vijiji vya baadhi ya mikoa ambavyo vina unafuu wa hali za maisha. Vijiji vya Mkoa wa Kilimanjaro na baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Arusha vina nafuu kubwa ya maisha. Vijiji vya Mkoa wa Singida, Shinyanga, Dodoma, vingi kati ya hivyo hali ya ufukara imetamalaki. Kuna kila sababu za kuweka na kuelekeza nguvu zetu katika kuwainua wakazi wa vijijini kuondokana na kero na changamoto lukuki zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Leo katika makala hii nitajikita zaidi katika kuangazia ni nini kifanyike katika kuvisaidia vijiji vyetu kuondokana na umasikini uliokithiri.

VIWANDA VIDOGO VIDOGO

Hii inaweza kuwa moja ya vichochea vya ukuaji wa uchumi ambao ungeliondoa Taifa letu katika hali ya umasikini uliokithiri kwa wananchi wake waishio vijijini na hata mijini.

Shukrani kwa Serikai ya Awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Rais Mzalendo aliye tayari kupambana na rushwa, ufisadi na dhuluma ili kuwaletea maisha bora wananchi, Rais John Pombe Magufuli. Serikali ya Awamu ya Tano imejinasibu kuwa ni Serikali ya Viwanda.

Nalipongeza sana wazo hili la Serikali ya Awamu ya Tano kuelekeza nguvu zake katika viwanda. Ni ukweli usiopingika kuwa viwanda vitakuwa mkombozi wa maisha ya wanyonge walio wengi. Swali ni je, viwanda hivyo ambavyo Serikali imekusudia kuhamasisha wawekezaji kuvijenga ni viwanda vya aina gani? Je, vinajengwa wapi?

Tukianza na ni viwanda vya aina gani; ukweli ulivyo, hapa nchini petu Tanzania kwa kuwa tuna maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ni vema viwanda ambavyo tutakusudia kuvijenga viwe ni vile ambavyo vinaongeza thamani ya bidhaa za kilimo.

Mfano, mwaka jana eneo la Dumila wilayani Kilosa, maelfu ya tani za nyanya ziliharibika shambani zikiwa zimemea na kuzaa vizuri. Tatizo kubwa lilikuwa ni ukosefu wa masoko.

Wakulima walijitahidi kulima na kuzalisha kwa wingi zao hilo. Tatizo lilikuwa ni wapi bidhaa hizo zitauzwa. Huo ni mfano mmoja katika mifano mingi ya mazao kuharibika shambani kwa kukosa soko.

Yapo maelfu ya manansi yanayoozea shambani kwa kukosa soko. Yapo maelfu ya machungwa yanayoozoea shambani kwa kukosa soko. Ukitaka kuamini hilo tembelea

maeneo yanakozalishwa mazao hayo uone jinsi yanavyooza yakiwa shambani eti kwa sababu yamekosa soko. Katika nchi yenye watu wanaokadiriwa kufika milioni 50 ni ngumu kukosa soko. Tunayo Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki ambayo kimsingi imepanua wigo wa soko la mazao ya biashara na chakula. Tatizo lipo tunatumiaje fursa hizo? Kama Serikali ingewekeza au kuhamasisha wawakezaji kuwekeza katika viwanda vya juisi na viwanda vingine vya usindikaji wa mazao ya kilimo, ukweli ulivyo bidhaa hizo zisingeozea shambani kwa sababu ya kukosa soko. Mazao ya matunda na mboga mboga kama kungelikuwa na viwanda vya kusindika matunda hayo na soko la uhakika la bidhaa hizo, hali za maisha za wananchi zingeboreka haraka sana.

Kinyume chake wananchi wa maeneo mengi wanakata tamaa ya kulima mazao hayo kwa kuwa wanahofia kuingia hasara ya uzalishaji.

Serikali ya Awamu ya Tano inayojinasibu kuwa ni ya viwanda izingatie kuwa kama inaandaa mazingira ya uwekezaji na fursa za ufunguaji wa viwanda, basi kuwa na mkakati maalumu wa kuwaelekeza wawekezaji kuwekeza katika viwanda vinavyosindika mazao ya chakula na kutafuta masoko ya ndani na nje.

Nasema hivyo kwa kuwa ninautazama kwa jicho la shaka mfumo wa ajira. Je, ni sekta ipi imeajiri asilimia kubwa ya Watanzania? Ukweli ulivyo sekta ya kilimo ndiyo sekta iliyoajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania. Japo Watanzania wengi hawakichukulii kilimo kama ajira. Fikra za walio wengi ni kwamba mtu anaweza kuwa mkulima baada ya kukosa ajira nyingine. Hapa ninaona kuwa kuna kila sababu ya sera ya viwanda ikaenda sambamba na ikawa sera pacha na sera ya kilimo kwanza. Viwanda vitakavyowekeza katika usindikaji wa mazao ya kilimo vitakuwa vimetoa hamasa kubwa ya vijana wengi kuwekeza katika kilimo, kwani kutakuwa na soko la uhakika wa mazao ya kilimo sambamba na ubora wa bei.

Hivi sasa kilimo kimekuwa kama laana hivi. Vijana wenye elimu ya kati na juu hata wasio na elimu hawataki kushiriki shughuli za kilimo, wengi wao wamekuwa wakisaka ajira kwenye viwanda na makampuni makubwa. Kwa kuwa teknolojia imekua, viwanda vinavyozalisha bidhaa nyingine zisizo za kilimo vinaajiri watu wachache hivyo kutopunguza tatizo la ajira. Ikiwa tutakuwa na viwanda vinavyojishughulisha na bidhaa za kilimo na sera nzuri ya masoko, hakutakuwa na tatizo la ajira au litapungua sana.

Tumeona hivi majuzi jijini Dar es Salam katika usaili ya Malmaka ya Mapato Tanzania (TRA). Nafasi 400 zimeombwa na watu 56,000. Hii ndio kusema kuwa tuna tatizo kubwa la ajira katika nchi yetu? Kundi kubwa la vijana linahangaika kutafuta ajira za maofisini kwa kuwa Serikali bado haijakifanya kilimo kufikirika na kuthaminiwa kama ni ajira.

VIWANDA VIJENGWE WAPI?

Kuna kila sababu za kuzingatia mahali ambapo viwanda hivyo vinajengwa. Viwanda hivyo vijengwe maeneo ambayo bidhaa za kilimo zinazalishwa. Huwa nashangazwa sana ninapoona kiwanda cha kusindika tumbaku kipo Morogoro wakati tumbaku hiyo inazalishwa Tabora, Ruvuma kwa wingi. Nashangaza sana kuona kiwanda cha kukamua juisi ya nanasi kipo Dar es Salaam, wakati manasi yanapatikana na kulimwa kwa wingi mkoani Geita. Ni vema Serikali ikaweka utaratibu wa kuwaelekeza wawekezaji maeneo maalumu ya kuwekeza viwanda vyao. Hii itawapunguzia wawekezaji hao gharama kubwa za uendeshaji sambamba na kumwinua mkulima, kwani gharama za usafirishaji hazitakuwepo hivyo bei ya bidhaa itakuwa na unafuu mkubwa kwa wakulima. Hatuna namna na hatuna muujiza wowote wa kufanya kama Taifa. Njia pekee ya kujikomboa na umasikini ni kuwekeza katika kilimo chenye tija. Kilimo kitaajiri si tu wakulima bali makarani na wafanyakazi wengine wa viwandani na kupanua wigo wa masoka ya bidhaa, ambapo zitazalisha wafanyabiashara wa mazao ya kilimo yaliyosindikwa.

Yapo mengi ya kufanya kuhakikisha safari ya kijiji inafikiwa kwa lengo la kuboresha hali za maisha ya wananchi. Itaendelea wiki ijayo. 0717809933

Wakulima wakipalilia mahindi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.