BURUNDI INAFAIDI MAPATO YA ASKARI WA KULINDA AMANI

Rai - - MBELE - BUJUMBURA, BURUNDI

Burundi sasa hivi inategemea sana vikosi vyake vya kulinda amani katika nchi za nje ambao hulipwa vizuri ili kuleta hali ya utulivu jeshini. Lakini wachunguzi wa mambo wanahoji – hali hii hadi lini?

Mgogoro unaoendelea ambao umeikumba nchi hiyo ndogo ya Afrika ya Kati tangu Aprili 2015 ni matokeo ya ya mikwaruzano miongoni mwa viongozi wa ndani katika chama tawala cha CNDD-FDD.

Baada ya kupigana pamoja katika vita ya msituni, baadhi yao waliona kwamba wakati umewadia kwa Rais Pierre Nkurunziza kuwachia wenzake nafasi hiyo ya juu, na wamekuwa wakiukataa mpango wake wa kutawala milele.

Viongozi wengi waandamizi wa utawala huo wameendelea kuwa maafisa wa jeshi ambao baada ya vita ya msituni walijiunga katika jeshi jipya na kupewa vyeo vya juu.

Utawala wa Burundi umekuwa ukijionyesha kwa mataifa ya nje kuwa ni wa kiraia, lakini kiroho ni wa kijeshi tu. Ingawa viongozi wa vyeo vya chini hawahusiki katika misuguano hii, ilionekana dhahiri jeshi lingejiingiza tu – na mfano ni jaribio la mapinduzi la Mei 2015.

Na tangu wakati huo mauaji yakuvizianayawatumashuhuri yamewafanya wale wanaomtii Nkurunziza kujizatiti dhidi ya ‘maadui’ wao – wa kikweli au bandia, na wingu la wasiwasi umelikumba jeshi hilo.

Historia ya jeshi la Burundi inatoa mwanga kwa haya yanayoendelea. Lilianzishwa mwaka 2004 kutokana na kuungana kwa vilivyokuwa vikundi vya uasi vya kabila la Hutu na jeshi la zamani lililokuwa linadhibitiwa na kabila la Tutsi. Makundi haya mawili yalipambana bila ushindi kwa upande wowote kwa miaka kumi (1993-2003).

Hivyo kwa msaada mkubwa wa nchi za kimataifa, jeshi jipya la Burundi lilionekana kama ni “ushindi” mkubwa kwa nchi hiyo katika kujijenga baada ya vita vya msituni. Na hili lilikuwa na msingi wake.

Mafunzo na kupigana nje ya mipaka liliongezea morali ya askari, na hii ni sababu kubwa jeshi hilo kutochukua upande wowote katika misuguano ya ndani kwa ndani inayoendelea.

Hata hivyo faida iliyopatikana kutokana na mafunzo na kupelekwa nje kulinda amani ina viwango vyake.

Maafisa wa vyeo vya juu bado ni sehemu ya ghasia na ufisadi ndani ya utawala. Amri zinazokinzana hufikia hadi kwa rais. Lakini kitu kikubwa ambacho kimeendelea kuleta umoja katika jeshi – pamoja na nchi yenyewe kuwa ni ya kimasikini – ni fedha. Na chanzo cha fesdha hizi ni operesheni za kulinda amani zinazofanywa na askari wake wanaopelekwa nchi za nje.

Operesheni hizi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) ni moja miongoni mwa shughuli kubwa tano za jeshi hilo jipya la Burundi.

Kuanzia Desemba 2007 askari kutoka jeshi la Burundi limekuwa Somalia, katika operesheni kubwa zaidi ya kijeshi Barani Afrika – iliyopachikwa jina la “African Mission in Somalia” - AMISOM.

Inakadiriwa kuna askari wapatao 5,000 na urefu wa muda waliokaa huko ina maana kwamba takriban askari wote wa jeshi la Burundi na maafisa wao wametumikia angalau kipindi kimoja katika operesheni hiyo nchini Somalia.

Shughuli za AMISOM zinatoa fursa za kiwango cha kimataifa katika mafunzo na hivyo fursa ya kupelekwa eneo lingine linalohitaji askari wa kulinda amani – hususan katika operesheni za Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Kwa ujumla mishahara nchini Burundi ni midogo sana – inaanzia Dola 80 za Kimarekani kwa mwezi kwa askari hadi Dola 250-300 kwa mwezi kwa maafisa wa ngazi za juu. Lakini hadi mwaka 2015 askari katika AMISOM wamekuwa wakipata mshahara wa Dola 1,032 kwa mwezi.

Yakijumlishwa na marupurupu mengine kama vile mikopo ya riba nafuu, mapato haya ni tosha kwa askari wengi kununua ardhi, kuanzisha maisha na kadhalika. Viwango hivi ni sawa kwa askari wa ngazi zote.

Wakati huo huo askari akifa akiwa katika operesheni familia yake hupata Dola 50,000 – fedha nyingi mno kwa viwango vya nchi kama Burundi.

Hivyo pamoja na hatari nyingi ya kuuawa katika operesheni, bado kuna wengi wanaojitolea kujiunga katika jeshi la Burundi kutokana na vivutio hivyo.

Hadi 2016 serikali ya Burundi ilikuwa inachukua Dola 200 kutoka kila askari kama gharama za uendeshaji jeshi. Kiwango hiki siyo kidogo, hasa tangu wafadhili walipoanza kujitoa kuisaidia nchi hiyo.

Mfaidika mkuu ni serikali – kutokana na fedha wanazolipwa askari ambazo zinawafanya wapiganaji msituni wa zamani waishi makambini kwa utulivu.

Kuanzia miaka ya 90 Burundi imekuwa miongoni mwa nchi zinazotumia au zilitumia majeshi yake katika operesheni za kulinda amani katika nchi nyingine ili kujiongezea hadhi kimataifa, kupata misaada kutoka kwa wafadhili na pia kutuliza uasi wa kijeshi nchini mwao. Nchi nyingine ni Chad, Uganda, na Rwanda.

Askari wa Burundi nchini Somalia katika mpango wa AMISOM.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.