SIKILIZA KILIO HIKI CHA WANANCHI KILWA

Rai - - MBELE -

UJINGA ni mzigo, ni mzigo mkubwa ambao ukituama kichwani mwa mtu kuutua kwake si kazi ndogo na asipopata wa kumtua upo uwezekano wa kufa na ujinga wake.

Hali ya kuwa mjinga inagharimu, gharama ya ujinga ni kubugizwa na kubugia yasiyo na tija. Kwa sababu za kimakusudi, ujinga wa wajinga unawafanya werevu wachache kuutumia katika kuwarubuni kwa vipande vya sarafu chafu zilizotakatishwa.

Hivyo ndivyo ilivyo wilayani Kilwa mkoani Lindi, baadhi ya werevu waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi walio wengi, kwa makusudi waliamua kuutumia udhaifu wa watu wengi kutojua mambo hasa sheria na umuhimu wa ardhi kustarehesha matumbo yao.

Werevu hao wachache waliamua kuviingiza gizani vijiji vinne vya Wilaya ya Kilwa. Wananchi wa vijiji hivyo wamedanganywa na kurubuniwa, wakarubunika sasa wamesaliwa na simanzi zisizo na mwisho.

Ni miaka takribani tisa sasa, wenyeji wa vijiji hivyo wamesalia kuwa wanyonge mbele ya ardhi yao kubwa iliyobeba misitu minene ya asili.

Wamelazimika kuwa wanyonge kutokana na kunyongwa na baadhi ya Watanzania wenzao wachache waliobarikiwa kupata kaelimu ka kuwatoa tongotongo, kaelimu kalikowapa nafasi ya kuwatumikia wakosa elimu.

Masikini ya Mungu wakazi wa vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti sasa wako njia panda, hawajui la kufanya, kama ni kulia wameshalia sana, kama ni kusema wameshasema mpaka wamekosa maneno, sasa wameamua kusubiri utashi, huruma na matakwa ya mkuu wa nchi, Rais Dk. John Magufuli.

Kinachowaliza na kutamani rais awafute machozi wanavijiji hao ni kuhodhiwa kwa eneo kubwa la ardhi yao.

Eneo kubwa la ardhi hiyo iliyobeba misitu ya asili inayoweza kutumika kwa manufaa ya wanavijiji hao imeshikiliwa na Kampuni ya BioShape.

Kampuni yenye makao yake Neer, Uholanzi, ambayo sasa inadaiwa kufilisika baada ya kutumia dola milioni 9.6 katika mradi wa nishati ya mimea ambao hakuna shaka yoyote kwa sasa umeota mbawa.

Mwaka 2006, kampuni hiyo ilikubali kukodi zaidi ya hekta 40,000 za eneo la pwani lenye misitu katika Wilaya ya Kusini ya Kilwa kwa ajili ya kupanda mimea aina ya mibono (Jatropha), ambayo mbegu zake hutumika kutengenezea mafuta ambayo yanaweza kuendesha mitambo mbalimbali yakiwemo magari.

Ilipotua nchini kampuni hiyo ilipanga kuajiri mamia ya wakulima wa eneo hilo. Dhamira kuu ilikuwa ni kuhakikisha wanapata mbegu za kutosha za mibono ambazo wangezipeleka Uholanzi ambako wangezisindika na kuzalisha umeme, mvuke na dizeli ya mimea.

Mibono ni moja ya mbegu zinazopendelewa zaidi kwa ajili ya mafuta. Aina hiyo ya nishati inadaiwa kutokuwa na madhara makubwa ya kuchafua hali ya hewa ikilinganishwa na mafuta mengine kutoka ardhini. Bahati mbaya hakuna umeme uliozalishwa hadi leo.

BioShape iliwekeza kiasi cha euro milioni 25 katika mtambo uliokuwa na lengo la kusindika tani 45,000 za mafuta kwa mwaka na kuzalisha megawati 25 za umeme ambazo zingetosha kusambaza umeme kwa kaya 50,000.

Mtambo wa Lommel ulikuwa moja tu ya sehemu ya mtandao mkubwa wa mitambo ya kusafishia na kuzalishia mafuta ambao BioShape ilipanga kujenga katika nchi za Ubelgiji na Uholanzi.

Mradi huo uliungwa mkono na wawekezaji wakubwa kama vile Benki ya biashara ya Kiholanzi ya Kempen & Coand na Kampuni ya ugavi wa umeme ya Eneco.

Utamu wa maelezo hayo hapo juu ulisaidia kuiingiza kwa kishindo kampuni hiyo ya kigeni hapa nchini, ilibebeshwa sifa ya kuwa na nia na dhamira ya kuzalisha nishati salama kwa mazingira, bahati mbaya sasa imewaacha na maumivu wakazi wa hasa Mavuji.

Mavuji mbali na ardhi yao kuendelea kuwa chini ya Bioshape ambaye naye anatajwa kuanza mchakato wa kuigawa ardhi hiyo kama pipi kwa kampuni nyingine iliyotajwa kwa jina la Somanga Property, lakini pia wameachiwa jangwa kwenye ardhi yao ya kijiji yenye ukubwa wa ekari 1000.

Mbali na hilo, wakazi wa kijiji hicho wake kwa waume wameachwa solemba, hawakupata mafao wala kiinua mgongo cha kazi waliyowahi kuifanyia kampuni hiyo kwa miezi takribani mitano.

Kibaya zaidi pamoja na kushirikishwa kwenye kuteketeza misitu yao wenyewe, ukweli ni kwamba wengi wao bado wanadai malimbikizo ya stahiki zao ambayo sasa hawajui wamdai nani.

Vijiji hivi vinakadiriwa kila kimoja kutoa zaidi ya ekari 15,000 kwa BioShape, ambaye alitua wilayani hapo mwaka 2006 na kuanza uzalishaji wake mwaka 2008.

Ajabu ni kwamba uzalishaji huo ambao unatajwa kwenda sambamba na ukataji wa misitu, haukuzaa matunda, hakuna kilichopandwa wala kuvunwa kwenye maelfu ya ekari hizo

vijiji hivyo vinne walizochukua.

Badala yake eneo lililotumika kufanikisha matakwa ya wachache halikuwa mali ya mwekezaji bali ni shamba la kijiji, ambalo Bioshape anatajwa kulitumia kama shamba la mfano na hapo ndipo panadaiwa kukatwa kwa maelfu ya miti.

Yapo mauzauza mengi yanayotajwa kuhusisha uwekezaji huo ambao sasa umepewa sura tofauti na ile ya awali. Unatazamwa kama uwekezaji uliokuwa na dhamira ya kuwamilikisha wachache ardhi ya wengi kwa manufaa yao.

Wanavijiji hao pamoja na viongozi wao wa vijiji, hawajui kama ardhi hiyo wameiuza au wameikodisha, hawajui kwa sababuwaliopaswakuwajulisha waliamua kuutumia udhaifu wao huo wa kutojua mambo kufanya maamuzi ambayo yaliwafurahisha wao.

Hapa ndipo wanavijiji walioguswa na kadhia hii wanapoamua kutumia silaha yao ya mwisho ambayo ni kupaza sauti kutoka nyikani ili iimfikie Rais Magufuli.

Ombi lao kwake ni kutaka awasaidie kuufuta umiliki au ukodishaji wa eneo lao kutoka kwa mwekezaji na kuwarejeshea wao ili walipangie matumizi bora ya ardhi au watafutiwe mwekezaji mwingine ambaye atakuwa na tija kwao.

Walitamani kupata fursa hii ya kumweleza rais, lakini hawakujua waanzie wapi hadi pale Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kinachoongozwa na Mkurugenzi shupavu John Chikomo na timu yake imara ya utendaji, kilipowafikia na kutoa nafasi ya kusikiliza sauti isiyosikilizwa na wanaopaswa kuisikiliza.

Jopo la waandishi wa habari za mazingira chini ya mwamvuli wa JET, chama ambacho kimejikita katika kutunza na kupigania uhai wa mazingira kwa kushirikiana na wadau wake Care Tanzania, limedhamiria kupaisha sauti za wanakijiji hao ambao sasa wanakiri kuwa si wajinga tena, semina kadhaa walizozipata juu ya umuhimu wa ardhi zimewafanya kutambua kuwa waliitoa ardhi yao pasi na kujua.

Hii ni bashrafu tu, uhondo wa suala hili uliobeba raha na karaha za mwekezaji huyo kutoka kwa waathirika wenyewe na viongozi wao uko njiani, huenda ukamiminwa kwenye safu hii au nje ya safu hii, lakini uhakika nilionao utakuwa ndani ya gazeti hili la RAI.

Kampuni yenye makao yake Neer, Uholanzi, ambayo sasa inadaiwa kufilisika baada ya kutumia dola milioni 9.6 katika mradi wa nishati ya mimea ambao hakuna shaka yoyote kwa sasa umeota mbawa. Mwaka 2006, kampuni hiyo ilikubali kukodi zaidi ya hekta 40,000 za eneo la pwani lenye misitu katika Wilaya ya Kusini ya Kilwa

Rais John Magufuli

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.