MAMA SAMIA ATOA AGIZO ZITO KWA POLISI

Rai - - MBELE - NA FRANCIS GODWIN

MAKAMU wa Rais Mama Samia Suluhu (pichani) ametoa agizo zito kwa jeshi la polisi nchini kwa kuwataka makamanda wote wa mikoa wa jeshi hilo kuanza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. RAI linaripoti.

Mama Samia amelitaka jeshi hilo kila mkoa kuhakikisha wanawashughulika na wanaume wanaowafanyia wake zao vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa agizo la kuwajibishwa kwa makamanda watakaoshindwa kazi hiyo.

Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa tamasha la 14 la mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP -Mtandao ) iliyofanyika kwenye viwanja vya mtandao huo vilivyopo Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na kuwepo kwa harakati mbalimbali za kuelimisha jamii kuondokana na vitendo vya ukatili kwa wanawake bado matukio ya ukatili wa kijinsia yamezidi kuongezeka na mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye matukio mengi ya ukatili wa kijinsia.

“Naona Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa upo hapa, naomba usimamie, nadhani umesikia taarifa iliyotolewa hivi punde kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vipo hata hapa Dar es Salaam, sasa nakuagiza wewe na makamanda wenzako wote nchini kuwa serikali haitapenda kuona vitendo hivi vinaendelea katika jamii na kama wewe utashindwa kuchukua hatua kwa kuwawajibisha wa chini yako utawajibika wewe, hivyo anza sasa kupambana na vitendo hivyo kwa kuagiza wa chini yako “alisema.

Hatua hiyo inatazamwa kuleta matokeo chanya katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini ingawa baadhi ya mila na desturi zinaruhusu matukio hayo.

“Suala la mila na desturi kwenye jamii yetu linapewa kipaumbele zaidi na kazi ya mwanaume ni kuishi kwa upendo na mke wake na sio kumpiga mara kwa mara mwanamke akipigwa mara moja ama kuonywa mara moja inatosha sio kumpiga kila wakati ama kumfanyia vitendo vya kinyama ….ila hata sisi wanawake tunapaswa kuheshimu waume zetu mimi pamoja na nafasi yangu ya umakamu wa Rais bado mume wangu nampigia magoti na kumnyenyekea tuishi kwa kuheshimiana.”

Alisema kuwa serikali iliyopo madarakani inatambua na kuthamini umuhimu wa masuala ya jinsia katika kuchangia na kuharakisha maendeleo ya nchi ambapo tangu nchi ipate uhuru serikali iliweka misingi thabiti ikiwemo ya kutunga sheria, kanuni, taratibu na sera rafiki na wezeshi zinazosimamia na kuhimiza jitihada za kuleta usawa wa kijinsia .

“Sotenimashahidi kuwa Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika hivyo imeridhia mikataba, itifaki na makubaliano mbali mbali ya kimataifa na kikanda kuhusu suala la kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake ambao ni utekelezaji wa mpango kazi wa mkutano wa Beijing.”

Alisema kuwa hatua nyingine ambazo serikali ya Tanzania inachukua ili kuhakikisha makubaliano na maazimio ya kimataifa na kikanda yanaakisiwa katika sheria na mipango ya nchi ni pamoja na kutunga mipango na sheria zinazomlinda na kumwezesha mwanamke ikiwemo dira ya Taifa ya maendeleo 2025 na mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano na sheria maalum ya makosa ya kujamiiana (SOSPA } ya mwaka 1998.

Hata hivyo anasema kuwa serikali ipo kwenye harakati ya kufufua Benki ya wanawake nchini ili kuweza kuwasaidia wanawake nchini kama njia ya kuwakomboa wanawake hivyo kupitia benki hiyo ni lazima kwa kila mmoja kusaidia kwa nguvu zote kuimarisha benki hiyo na wale wanaojua mitaji ipo wapi basi kujitokeza kuonyesha .

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia nchini TGNP –Mtandao Vicensia Shule anasema kuwa sababu zinazopelekea umasikini huo kukithiri kwa wanawake ni uwekezaji hafifu, miundo mbinu duni, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo hali ambayo imezidi kudhoofishwa na mgawanyo wa rasilimali usiokuwa sawa uharibifu wa ardhi na athari za tabia nchini.

Kuwa Tamasha la wa Jinsia linalenga kufichua ukosefu wa usawa unaowakabili wanawake ambao umeweza kuwaathiri katika Sekta ya Afya, Elimu uwakilishi wa kisiasa na soko la ajira.

Mkurugenzi mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi anasema Tamasha la mwaka huu linaongozwa na mada kuu ambayo ni mageuzi ya mfumo kandamizi kwa usawa wa jinsia na maendeleo endelevu na kuwa katika tamasha hilo la siku nne wadau washiriki watachambua mambo mbali mbali .

Liundi anasema kuwa kuwa kwa ajili ya kutambua mchango wa mafanikio ya TGNP Mtandao uliofanywa na wanawake mbali mbali na taasisi mbali mbali wametumia tamasha hilo kutoa tuzo kwao .

Kuwa tuzo hizo ni kwa ajili ya wanachama waanzilishi wa TGNP Mtandao ambao miongoni mwao kuna waliotangulia mbele za haki ambao wote wamekuwa chachu ya mtandao huo kwenye harakati za kupambana na masuala ya ukatili wa kijinsia .

Wanachama hao ni Fides Chale , Marjorie Mbilinyi, Agripina Mosha, Mary Rusimbi ,Demere Kitunga, Aseny Muro, Zippora Shekilango, Subira Kilaga pamoja na hao pia wanatambua baadhi ya wanawake ambao pia wamekuwa cha Takwimu hizo ambazo zilitolewa mwaka 2015.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.