Tusiitafsiri changamoto ya ajira kwa njia nyepesi

Rai - - MAONI/KATUNI -

Wiki iliyopita iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba zaidi ya Watanzania 30,000 wengi wakiwa vijana walijitokeza kufanya usaili katika kanda 10 zilizopo maeneo mbalimbali nchini.

Watanzania hao kwa wingi wao huo walikuwa wakiwania nafasi 400 za ajira ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Maafisa wa mamlaka hiyo walitaja changamoto zilizojitokeza pamoja na idadi kubwa ya waombaji kuwa ni kutokuwa na vyeti vya elimu ya sekondari kwa baadhi ya waombaji kwa madai walivipoteza na wengine kuchelewa kufika kwenye vyumba vya usaili.

Hata hivyo tungependa kuzungumzia kauli nyingine ya TRA kwamba kujitokeza kwa idadi kubwa ya watu kufanya usaili huo hakumaanishi kuwa watu hawana ajira isipokuwa ni kwamba wengi wao wanafanya kazi kwenye taasisi binafsi na sasa wanatamani kupata ajira Serikalini.

Kauli hiyo inaweza ikawa na ukweli au si kweli kwani ni vigumu kuithibitisha. Hata hivyo si vyema kulitafsiri suala la ukosefu wa ajira kwa njia ya mkato namna hiyo – kwamba huenda halipo au si tatizo kubwa.

Gazeti moja la kila siku lililotoka Jumanne ya wiki hii liliripoti kwamba zaidi ya watu 5,000 mjini Morogoro walivamia na kufanya vurugu kwenye kiwanda kipya cha kutengeneza mafuta ya kupikia wakishinikiza kupewa ajira kiwandani humo.

Hatua hiyo ilitokea siku mbili baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kukizindua kiwanda hicho.

Tukio hilo na wingi wa watu waliojitokeza kwenye usaili wa TRA kwa pamoja vinaashiria uwapo wa tatizo la ajira hapa nchini.

Hii ni changamoto kubwa na ni ya siku zote. Hata Juni,2014 zaidi ya watu 10,000 walikusanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kufanya usaili wakiwania nafasi 70 zilizotangazwa katika Idara ya Uhamiaji.

Mwezi uliofuata watu 6,740 walifanyiwa usaili wa kuwania nafasi 47 zilizotangazwa na Shirika la Viwango (TBS). Tunaamini mifano hiyo hapo juu ni michache kati ya orodha ndefu ya matukio ya usaili ambayo yamekusanya idadi kubwa ya watu.

Siku zote tumekuwa tunakumbushwa kwamba ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiriwa kulipuka. Haliwezi kumalizwa kwa kutangaza nafasi chache za kazi Serikali huku maelfu ya watu wakizigombea.

Ukubwa wa changamoto hii umewafanya hata baadhi ya viongozi wetu kutoa tafsiri mpya ya neno “ajira.”

Sasa hivi “ajira” ni pamoja na zile za kujiajiri kama vile “biashara za ‘wamachinga” wakiwa na liseni zao za “nguvukazi,” au vibarua katika sehemu za ujenzi na vibarua wengine wanaopata ujira siku kwa siku katika maeneo ya sokoni, sekta ya usafiri na sehemu nyingine ndogo ndogo za kiuchumi ambazo hazina kinga za kazi au bima.

Ni vyema tukaendelea kuwa na tafsiri “ajira” katika mantiki ya kiuchumi kama ilivyo ile ya Marekani au nchi nyingine au jinsi ilivyokuwa hapa Tanzania miongo kadhaa iliopita.

Mwelekeo mzuri wa kutatua changamoto ya ajira ni kuwa na uchumi wa viwanda, kama vile suala hili linavyopigiwa kampeni na serikali ya awamu hii ya Tano, tusijaribu kuitafsiri changamoto ya ajira kwa njia nyepesi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.