Tanga iliyokufa kiuchumi itafufuka?

Rai - - MAKALA - NA SUSAN UHINGA

WIKI iliyopita niliuelezea Mkoa wa Tanga kwa kugusa maeneo mbalimbali ikiwamo ukubwa wa eneo la mkoa huo, makabila yaliyopo, hali ya hewa na shughuli za kiuchumi.

Ukweli ni kwamba Tanga ilikuwa kitovu cha uchumi wa Tanzania, kabla ya kukaribishwa kwa sera ya ubinafsishaji miongo zaidi ya miwili iliyopita, uchumi wa Tanga ulikuwa imara, ajira zilikuwa za kutosha, viwanda viliifanya Tanga ing’are, bahati mbaya hali sasa ni tofauti.

Tanga ya leo imechoka, haina nuru tena, imekosa matumaini ya kurejea kuwa moja ya mikoa inayochangia pakubwa bajeti ya Taifa.

Kwa sasa wakazi wengi wa mkoa huu hutegemea kilimo cha kubahatisha kinachosubiri zaidi mvua za msimu, ufugaji na uvuvi.

Mazao ya chakula hasa ni mahindi, muhogo, ndizi, maharagwe na mpunga, mazao ya biashara ni katani, pamba, kahawa, chai, nazi, tumbaku na korosho.

Mifugo inayopatikana Tanga ni ng'ombe, mbuzi, kondoo pamoja na kuku.

Katani ilikuwa zao la biashara hasa kwa ajili ya Tanga tangu kuingizwa kutoka Mexico zama za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Zao hili hulimwa kote mkoani isipokuwa Lushoto, eneo kubwa linalolima katani ni Muheza na Korogwe kwenye mashamba makubwa. Mashamba hayo yalikuwa ya walowezi, yakataifishwa baada ya uhuru. Tangu kuanguka kwa sekta ya umma yamebinafsishwa tena siku hizi, zao la katani linategemea sana soko la dunia, umuhimu wake ulirudi nyuma tangu miaka ya 1960.

Hali imekuwa hivyo kwa miaka mingi sasa, huenda mkombozi wa uchumi wa Tanga sasa amepatikana.

Ujio wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga –Tanzania unaweza kusaidia kuhuisha uchumi uliokufa na kuelekea kuoza.

VIWANDA

Tanga ilikuwa na viwanda vingi kiasi katika miaka ya 1960 na 1970, lakini sasa karibu vyote vimekwama kutokana na Siasa ya Ujamaa na uchumi wake ulioiga mfumo wa nchi za kisoshalisti.

Viwanda vichache vilivyobaki havizalishi mali kulingana na uwezo wao. Kilichobaki hasa ni kiwanda cha saruji Tanga.

Utalii umeanza kupanuka kidogo, hasa katika maeneo ya Pangani, Mapango ya Amboni na kituo cha Makumbusho ya Urithi Tanga.

Ili kuendelea kuwapa wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla ufahamu wa fursa ya ujio wa bomba la mafuta ghafi, tutaendelea kuleta mfululizo wa makala zenye kuainisha na kufafanua masuala mbalimbali yanayohusiana na mradi huo mkubwa barani Afrika.

Natoa shukurani zangu za dhati kwa msomaji wa safu hii, nakiri kupokea maoni na pongezi zenu.

Kama nilivyopata kusema kwenye makala kadhaa zilizotangulia juu ya dhima ya makala zangu hizi.

Dhima kuu ni kuhakikisha najaribu kuwapatia Watanzania wenzangu ufahamu wa kutosha juu ya mradi huu mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi.

Huu ni mradi wa kihistoria kwa nchi yetu ukiachilia mbali ule wa TAZAMA uliojengwa miaka mingi iliyopita.

Imani niliyonayo ni kwamba mradi huu una tija kubwa kwa Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa jumla, lakini tija kubwa zaidi ni kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga.

Kwa kuzingatia umuhimu huo, ndipo ninaposhawishika kuzama kwenye kina kirefu cha mradi huu ili kuibuka na mambo mbalimbali yanayohusu mradi huu, ambayo naamini yataibua chachu kwa mwananchi mmoja mmoja kuuona umuhimu wa mradi huu.

Ikumbukwe kuwa fursa kama hizi hujitokeza mara chache kwa miaka mingi, hivyo basi kama Taifa na kama wakazi wa Tanga, hatupaswi kuiacha fursa hii ipite na kuwanufaisha wageni.

Wanufaika wa kwanza tunapaswa kuwa sisi Watanzania na hasa wakazi wa Tanga.

Ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,443, huku ardhi ya Tanzania ikitumika kwa kilomita 1,155 ni jambo la kufurahia.

Kufurahia fursa hiyo kwa maneno hakutoshi, bali tunapaswa kuifurahia kwa vitendo ambavyo ni kuwa na utayari wa kuwekeza kwa hali na mali.

Pamoja na kupaswa kuwa na utayari wa kuwekeza kwa hali na mali, lakini pia tunapaswa kuutazama uchumi wa Tanga katika kipindi hiki cha kuelekea mradi huo.

Ukweli ni kwamba kwa sasa Mji wa Tanga umechoka kiuchumi, viwanda vingi vilivyokuwapo hapo awali sasa havipo tena.

Kilimo cha mkonge nacho kimebeba sura ya kuzeeka na hakionekani kama kimeacha watoto ama wajukuu, hii inamaanisha kilimo cha zao hilo ambalo lilikuza Uchumi wa Tanzania kabla ya Uhuru, sasa limepoteza hadhi yake.

Yapo maswali kadhaa ya kujiuliza, kubwa likiwa ni je, ujio wa mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, utafufua uchumi wa Tanga ambao ulishakuwa kwa zaidi ya miongo miwili?

Si rahisi kujibu swali hili bila takwimu na vielelezo stahiki, lakini kutokana na umuhimu wa swali hili mfululizo wa makala hizi utatupatia majibu yote stahiki kutoka kwa wahusika wote bila kujali yuko wapi na anafanya nini.

Bomba la mafuta

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.