Wanyonyaji wa KCU(1990) Ltd washughulikiwe

Rai - - KUTOKA MTANDAONI -

Ushirika ni dhana muhimu inayowasaidia Wananchi hasa wenye kipato cha chini na kati kuanzisha na kumiliki chombo chao (chama cha ushirika) kidemokrasia na kuchangia mtaji unaohitajika kwa usawa na kukubali kuyakabili matatizo na kupata manufaa kutokana na shughuli za chombo hicho ambazo wao hushiriki kikamilifu.

Ushirika pia unatoa fursa kwa wananchi hasa wenye uwezo mdogo kuunganisha nguvu zao pamoja katika kujijengea nguvu za kiuchumi ambazo ni muhimu katika kukabiliana na ushindani wa soko huru na utandawazi.

Katika Vyama vya Ushirika, wanachama wana jukumu la kutatua matatizo yao ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia juhudi zao za pamoja katika kufikia malengo ambayo yasingefikiwa kwa juhudi za mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo hali imekuwa tofauti kwa vyama vingi vya ushirika nchini. Ushirika umekuwa ukinufaisha kundi dogo la watu huku wahusika wakuu wakiishia kunyonywa kila uchwao.

Ukweli wa jambo hili umedhihirika wazi kwenye Chama Kikuu cha Ushirika Kagera –KCU (1990) Ltd.Chama hiki kimeliwa vya kutosha, baadhi ya waliokuwa viongozi wake walikitumia kikamilifu kujinufaisha.

Taarifa za kuliwa kwa chama hiki zipo, katika kipindi cha muda wa miaka 10 nilibaini kuwapo kwa ubadhirifu wa sh. bilioni 20.

Natambua yapo mabadiliko makubwa yamefanyika kwenye uongozi wa KCU (1990), lakini nashindwa kujua ni kwanini wale walionyonya jasho la wengi kwa miaka mingi hawajashughulikiwa hadi sasa.

Nashindwa kuelewa hii bodi mpya ya chama chetu inashindwaje kurejesha jasho la wanyonge lililoliwa kwa muda mrefu huku wakijua wazi vielelezo vyote vipo, yote waliyoyafanya wala hayahitaji uchunguzi wa miaka mingi, labda wenzangu wanatafuta vielelezo zaidi ambavyo wanavijua wao.

Taarifa zote muhimu za ujanja wao walioufanya zipo, walinunua hoteli mbili ikiwemo Yasira ambazo zote taarifa zilizokuwa zikitolewa zilidai zinajiendesha kwa hasara.

Mbali na hilo, lakini pia hoteli zilinunuliwa kwa bei ndogo, lakini kwa wanachama zilielezwa kununuliwa kwa fedha nyingi.

Niliwahi kuuliza kwanini tunanunua Yasira hoteli wakati Lake hoteli tumeshindwa kuiendesha, hapo ndipo nilipoingia kwenye mgogoro na waliokuwa viongozi wa ushirika wetu wa Kagera.

Ajabu kubwa zaidi ni baadhi ya viongozi kuwadanganya wahaya kuwa eti, baadhi ya Kahawa zetu zinategemea dawa zaidi, jambo ambalo si kweli kwani kahawa zetu zote za Bukoba ni za asili (organic) hazitegemei mbolea wala dawa yoyote.

Wajanja walikuwa wakitumia udhaifu wa wakulima kutojua mambo kuwanyonya, wao walikuwa wanauza kahawa kama organic, lakini wakulima wanaambiwa kahawa yao si organic. Kibaya zaidi baadhi ya viongozi walikuwa wakiwachagulia wakulima viongozi wa kuongoza vyama vya msingi, lakini yote haya yamesababishwa na wakulima kukosa elimu ya ushirika.

Nina imani kubwa na Mwenyekiti wa Bosi ya chama hicho kwa sasa, namuomba asiruhusu wanyonyaji wale waendelee kutamba mtaani, ni vema wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Lakini pia ipo haja ya Serikali kuimarisha zaidi vyama vya msingi kwa kutoa elimu juu ya ushirika, wakipatiwa elimu ya kutosha itawasaidia kuzijua haki zao. Mimi Archard Muhandiki ni mdau wa zao la kahawa na mwanaushirika wa KCU (1990) Ltd na pia ni mwakilishi wa Chama cha Msingi Kamachumu, naiomba Serikali iwashughulikie wanyonyaji wote waliokizamisha chama cha Ushirika Kagera, lakini kubwa zaidi ni kuwapa wakulima wa Kahawa elimu ya kutosha ya ushirika .

Jengo la Ofisi Kuu ya Chama cha Ushirika KCU 1990 LTD Mkoani Kagera

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.