Serikali itekeleze sera ya elimu, mafunzo kwa vitendo

Rai - - MAKALA - NA LUGENDO MADEGE (TUDARCO)

RAIS John Magufuli ni mmoja wa viongozi wanaopaswa kupongezwa kutokana na kuthubutu kuwa mzalendo wa kweli katika kutumia lugha ya Kiswahili, hasa pale anapowahutubia Watanzania mbele ya viongozi wa mataifa mbalimbali bila ya kujali kama wao wanaijua lugha hiyo au lah!

Mfano mzuri ni katika ziara ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Mod, katika ziara yake aliyoifanya hapa nchini katikati ya mwaka jana, wakati wa kuhutubia Rais Magufuli aliletewa hotuba iliyoandaliwa kwa lugha ya Kiingereza lakini baada ya kuona umuhimu wa Watanzania kujua nini kilichopo katika hotuba ile, akaamua kuomba iliyoandaliwa kwa lugha ya Kiswahili na kuhutubia mbele ya mgeni wake, jambo hilo pia alilifanya katika mkutano wa wakuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki na hata hivi karibuni alipokuja Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi.

Zipo dalili za kuirudisha heshima ya Tanzania kitaifa na kimataifa kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, kwani alihutubia kwa mara ya kwanza katika Bunge la kwanza la uhuru wa Tanganyika kwa kutumia lugha ya Kiswahili na baada ya hapo alitoa matamko mengi tu ya kukifanya Kiswahili kiheshimike na pia lugha hii ilitumika katika kufundishia na kujifunzia na kuwa somo la kusomeshwa katika shule za msingi na sekondari hapa nchini na elimu ilikuwa ni bora.

Kwa kuwa rais ameonesha mfano wa kukithamini Kiswahili kwa kukitumia katika shughuli za kitaifa na kimaifa, ni vizuri pia kwa viongozi wengine wa Serikali hii ya Awamu ya Tano kufanya hivyo lakini pia hata viongozi wa vyama vya upinzani pale wanapopata mialiko mbalimbali ndani na nje ya nchi wakaweke masilahi ya Taifa mbele kwa kuitukuza lugha yetu ya Kiswahili na kuonesha kwa vitendo kuwa sisi ni Waafrika halisi. Hata Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, aliwahi kuhutubia kwa mara ya kwanza katika mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika (AU) nchini Ethiopia kwa Kiswahili.

Pamoja na hayo niwakumbushe viongozi wetu suala la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia na kujifunzia kama inavyosema sera mpya ya elimu na mafunzo ambayo ilizinduliwa rasmi na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, Februari mwaka 2015, sera hii inaeleza masuala mengi ya elimu, kwa mfano mfumo wenyewe wa elimu, miundombinu na kumwezesha Mtanzania kujiendeleza katika mikondo ya kitaaluma.

Kuhusu suala la Kiswahili, sera inaeleza kwamba lugha ya Kiswahili itatumika katika ngazi zote za elimu na mafunzo, ambapo Serikali yenyewe itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija kitaifa na kimataifa.

Ni vema tamko hili la sera ya elimu na mafunzo kuhusu lugha hii adhimu ya Kiswahili, kuanza kufanyiwa kazi kwa kuwekewa utaratibu maalumu, ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya wadau wa elimu wenye nia thabiti ya kuona elimu yetu inaendelea na kuzalisha wataalamu wenye ubora na ushindani ambao kazi yao itakuwa ni kuandaa mpango wezeshi wa kuona kuwa Kiswahili kinaanza kutumiwa kuanzia darasa la kwanza hadi vyuo vikuu.

Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo nimekuwa kila siku nikishuhudia matamko na ya amri kutoka kwa vingozi wake juu ya kutaka vyombo vya dola kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi ambao wanatuhumiwa kuisababishia Serikali hasara kwa kutosimamia vema matumizi sahihi ya fedha za Watanzania, wakati mwingine nia ni njema, ni vizuri pia ikaanza kutekeleza mipango na sera ambazo imezitunga yenyewe kwa masilahi ya Taifa zima hasa sera hii muhimu sana ya elimu na mafunzo.

Ni wakati sasa tena ni mwafaka kwa Serikali hii kuwaeleza wananchi ugumu uliopo katika kutekeleza Sera hii ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2015 kwa vitendo, kwani tafiti nyingi zilizofanywa na wataalamu wa masuala ya lugha zinaonesha kuwa, ni rahisi sana kwa mtu kujifunza kwa lugha yake ambayo anaijua vizuri na hapa nchini inayotambuliwa na kuzungumzwa na karibu Watanzania wote ni Kiswahili.

Itakuwa vizuri kwa Watanzania kufahamishwa sababu za kushindwa kutekelzwa kwa sera hii hasa juu ya jambo la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia na kujifunzia, maana ni miaka mitatu sasa tangu kuzinduliwa kwake na

ni hatukuelezwa ugumu uko wapi katika kutekeleza hili au tunasubiri wenzetu wa nchi jirani waanze ndiyo na sisi tufuate.

Kenya jirani yetu na ndugu yetu wa karibu ni nchi ambayo ni hodari sana katika kutumia fursa yoyote inayojitokeza, kwani takwimu zinaonesha kuwa ndiyo nchi yenye walimu wengi waofundisha lugha ya Kiswahili katika nchi za nje ikilinganishwa na nchi zote za Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, wakati sisi ndio vinara wa lugha ya Kiswahili lakini tunashindwa kukitumia kwa manufaa ya Watanzania kama fursa.

Ili kufanikisha utekelezaji wa Sera hii ya Elimu na Mafunzo ya 2015 ya ufundishaji wa Kiswahili kwa masomo yote katika elimu ya sekondari, Serikali inapaswa kuweka mkakati wa kuandika vitabu pamoja na kuvitafsiri vile vya sayansi na hisabati kwa lugha ya Kiswahili baada ya kupata idhini ya kutafsiri vitabu hivyo kutoka kwa watunzi wenyewe na kazi hii inaweza kufanywa na chombo chake ambacho ni Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita)

Shughuli ya tafsiri na kuandika vitabu inahitaji uwezo mkubwa na ufahamu wa taaluma yenyewe pamoja na matumizi sahihi ya lugha, hapa ni lazima Bakita waanze mchakato wa kusanifu istilahi kulingana na mahitaji halisi na ninadhani kuwa baraza hilo lipo tayari kwa kazi hiyo, kwani hata wao pia ni wadau wa maendeleo ya elimu kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Hatuna budi kujivunia, ni suala la tamko lililopo katika Katiba inayopendekezwa kuwa Kiswahili ni mojawapo ya tunu za taifa, hii ina maana kuwa lugha ya taifa imethaminiwa kiasi kwamba inatambuliwa katika Katiba ya nchi.

Wazari wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.