Azam kutumia uwanja wao ni utekelezaji wa kanuni

Rai - - MICHEZO - NA AYOUB HINJO

DEAN Court ni uwanja mdogo zaidi katika Premier League. Unaingiza idadi ya watazamaji 11,360, ni uwanja unaomilikiwa na AFC Bournemouth huko England.

Angalia idadi ya mashabiki wa Manchester United, Arsenal, Chelsea na hata Liverpool ilivyokuwa kubwa lakini hawa wote wanaingia katika uwanja huo mdogo na kucheza michezo yao ya ligi hapo.

Kwanini timu hizi zenye mashabiki wengi zinamudu kuingia pale na kuondoka salama? Kwa sababu kuna utaratibu mzuri ambao umepangwa na unafuatwa na timu zote, hususani mashabiki wao.

Ule uwanja wa Dean Court una afadhali kidogo, kwa uwanja huu wa Ipurua Municipal nchini Hispania unaoingiza idadi ya mashabiki 7,083 tu. Yaani watu 83 zaidi ya uwanja ule unaomilikiwa na klabu ya Azam maarufu kama ‘Azam Complex’ nje kidogo ya jiji la dare s Salaam.

Ilikuwa ngumu sana kwa timu za Simba na Yanga kucheza katika uwanja wa Azam Complex, huku kila timu ikiwa na hoja ya kuwa na idadi kubwa ya mashabiki hivyo uwanja usingekidhi kuchukua mashabiki wao ambao mara nyingi hupenda kujitokeza kwa wingi pindi timu zao zinapocheza mechi zake. Je, Manchester United waseme nini kuhusu uwanja wa Dean Court? Au Real Madrid na Barcelona ziseme nini kuhusu uwanja wa Ipurua unaomilikiwa na Eibar?

Vyovyote vile, iwapo wahusika wenye dhamana ya kusimamia mchezo huu hapa nchini wakiweka utaratibu mzuri basi kila kitu kitaenda sawa bila matatizo yoyote kutokea. Nchi zilizoendelea kisoka walikuwa wanalijua hilo, ndio maana wakaweka sheria zao ili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kutokea.

Leo hii haishangazi kuona Manchestr United, Liverpool au Arsenal zenye mashabiki wengi England zikienda kucheza katika uwanja wa ugenini wenye uwezo wa kubeba karibu theluthi ya idadi ya mashabiki wanaoweza kuingia katika viwanja vyao.

Kila timu ambao inamiliki uwanja wake ina haki ya kuutumia kwa michezo yake ya nyumbani, labda itokee ukawa katika matengenezo kama ilivyokuwa kwa Tottenham ambao wanatumia uwanja wa Wembley kwa sasa.

Msimu uliopita Arsenal walicheza mchezo wa FA, dhidi ya timu ambayo haishiriki ligi rasmi, Sutton United ambao uwanja wake ulikuwa unaingiza idadi ya mashabiki 5013, huku viti 765 ndio vilikuwa na uhakika wa kukaliwa.

Hakuna maafa yaliyotokea, hakuna ugomvi wala vurugu zozote zilizoripotiwa kutokea kwa kuhusisha mashabiki wa pande zote mbili. Kila kitu kilifuata kanuni za kwao na mambo yalienda sawa.

Katika miaka ya mwanzoni mwa 2000 ilishuhudiwa timu za Simba na Yanga zikisafiri na kwenda kucheza katika uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, ambao hutumiwa na Mtibwa Sugar kama nyumbani kwao.

Hata hivyo baadaye Mtibwa Sugar waliridhia kutumia ule wa Jamhuri kwa mechi inazozikutanisha na timu hizo kongwe tu huku sababu kubwa ikiwa ni matarajio ya kimapato zaidi na si suala la usalama kamwe.

Unadhani kuna jambo kuu la maana ambalo lilisababisha kuhamisha michezo ya timu hizo? Wala hakuna, wakati ule ilifika wakati Shirikisho lilikuwa linahitaji mapato zaidi kutoka kwa mashabiki wanaoingia uwanjani katika kujiendesha.

Katika kumbukumbu haijawahi kuripotiwa hata mara moja uwanja huo ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki chini ya 7,000 lakini bado timu hizo kubwa zilipocheza na Mtibwa haikuwahi kutokea vurugu au maafa.

Lakini toka marekebisho ya ratiba yafanyike na kutolewa hadharani huku ikionesha Simba na Yanga zikitakiwa kucheza mechi zake dhidi ya Azam katika uwanja wa Chamaz,i kumezuka mijadala huku baadhi wakipinga uwanja huo kutumika kwa mechi za timu hizo.

Hoja kubwa inayotolewa ni kwamba Uwanja una uwezo wa kuchukua idadi ndogo sana ya mashabiki hivyo inaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani iwapo mashabiki wa klabu hizo mbili watajitokeza kwa wingi kutaka kushuhudia michezo hiyo. Hata hivyo wakati wadau wanajadili na kulkiona hilo ni vema basi wakarejea mifano kutoka kwa timu zingine kubwa nje ya Tanzania ambazo hulazimika kucheza hata katika viwanja vidogo.

Nini kifanyike ili Tanzania nayo iende sawa na nchi zingine ambazo zimefanikiwa kisoka? Hakuna njia ya mkato katika hili, kila kitu kina utaratibu wake, hapa ni suala la utii wa sheria tu.

TFF inaweza kuweka mikakati mizuri ili kuepuka hofu waliyonayo mashabiki hao.

Kwanza wanaweza kuuza tiketi mapema ili kuhakikisha siku ya pambano hakuna pilika pilika za biashara ya viingilio. Utaratibu unaweza kuzingatiwa endapo timu husika zitakuwa na idadi kamili ya tiketi wanazotakiwa kumiliki.

Hata muda wa uuzaji tiketi unatakiwa uzingatiwe, tatizo la hapa kwetu hata siku ya mechi utakuta tiketi zinaendelea kuuzwa nje ya uwanja. Hapa lazima kuwe na tatizo.

Ilitakiwa iwe siku ya mechi kuwe na utaratibu wa watazamaji kuingia uwanjani na kuangalia mpira tu baada ya tiketi zao kukaguliwa na endapo idadi kamili ya tiketi zilizouzwa ikitimia basi milango lazima ifungwe.

TFF wapo sawa katika hili la kupeleka michezo hiyo katika uwanja wa Azam Complex kwa kwua ni haki yao kikanuni lakini pia ni chachu kwa timu zingine nazo kupambana na kuhakikisha wanamiliki viwanja vyao.

Simba walicheza pale msimu uliopita dhidi ya Mtibwa kwenye mchezo wa kirafiki, hata Taifa Stars walicheza dhidi ya Lesotho hapo hapo, huku kila kitu kikienda sawa.

Inakuaje wadau wanaanza kuhoji kuhusu udogo wa uwanja huo wakati timu hizo zimeshawahi kuutumia. Kama kikanuni hakuna kipengele kinachozungumzia idadi ya mashabiki katika uwanja basi wanaopinga hawana hoja hivyo lazima Azam wapewe haki yao.

Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.