Ushirikina watia doa mechi ya Cameroon, Nigeria

Rai - - MICHEZO KIMATAIFA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WIKI iliyopita, Bara la Afrika lilipambwa na michezo mbalimbali ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Urusi na hizo zilikuwa ni mechi za kwanza kabla ya zile za marudiano zilizochezwa mwanzoni mwa wiki hii.

Ukiacha ule wa marudiano uliochezwa Jumatatu iliyopita mjini Younde, mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu za Taifa ya Cameroon na Nigeria ‘Super Eagles’ ulikuwa gumzo barani Afrika.

Kutokana na historia na mafanikio makubwa ya mataifa hayo kwenye soka, mashabiki wengi wa mchezo huo walikuwa wakiusubiri mtanange wao wa kwanza uliochezwa mjini Lagos.

Katika mchezo huo wa Kundi B, Nigeria iliweza kuwatambia wapinzani wao hao baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0. Mabao hayo ni yale yaliyopachikwa na mastaa Odion Ighalo, John Mikel Obi, Victor Moses na Kelechi Iheanacho.

Hata hivyo, kilichozua gumzo katika pambano hilo si tu matokeo hayo, bali kile kilichotokea kabla ya timu hizo kuingia uwanjani.

Kikosi cha Cameroon kiliwasili nchini Nigeria, kilikataa Hoteli ya kifahari ya Le Meridien Ibom waliyokuwa wameandaliwa na wenyeji wao, wakidai kuhofia kufanyiwa vitendo vya kishirikina.

Waliokataa timu hiyo kuingia kwenye hoteli hiyo ya hadhi ya nyota tano ni viongozi wa Chama cha Soka Cameroon (FECAFOOT), ambao waliamua kuandaa sehemu nyingine, wakidai kwamba wachezaji wao wangerogwa endapo wangefikia Le Meridien Ibom.

“Hatuwaanini Wanigeria, wanaweza kutaka kutufanyia urozi,” alisema ofisa mmoja wa FECAFOOT aliyeungwa mkono na wenzake.

“Tunawajua Wanigeria kwa uchawi lakini mnajua jinsi uchawi wa Cameroon ulivyo moto wa kuotea mbali?,” alisema bosi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya FECAFOOT, Jean Jacques Mouandjo.

Bosi mwingine wa Chama hicho cha Soka, Valery Gweha, alizungumzia uchawi wa Nigeria katika soka, ambapo alisema hata kichapo cha timu yao ya wanawake katika mchezo wa fainali za Afcon za mwaka jana dhidi ya Nigeria kilitokana na sababu kama hizo kutoka kwa wapinzani wao hao.

Katika mchezo wa fainali uliozikutanisha timu hizo bao la dakika za majeruhi lililofungwa na mwanadada, Desire Oparanozie ndilo lililoipa Nigeria taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0.

Akilizungumzia bao hilo la dakika ya 86, Gweha alidai kwamba halikuwa la kawaida na badala yake lilitokana na nguvu ya giza (juju). “Lile bao la (Desire) Oparanozie dhidi ya Cameroon katika fainali za Wanawake za Afcon lilikuwa la ‘juju’, nina uhakika kwani lile bao halikuwa la kawaida,” alisema Gweha.

Hata Cameroon waliwahi kutajwa kutumia uchawi katika fainali za Afcon za mwaka 2010, ambapo mwandishi mmoja wa habari alifunguka kuwa mabosi waliokuwa kwenye msafara wa timu hiyo ndiyo waliokuwa wahusika wakuu.

“Mmoja wao alikuwa na kiberiti wakati hakuwa mvutaji sigara. Cha kustahajabisha, alikuwa akiwasha mshumaa hata mchana. Kama hakuwa mshirikina, ungemwitaje?,”alihoji mwandishi huyo.

Kwa miaka mingi, vitendo vya kishirikina vimekuwa sehemu ya soka la Afrika. Mbali na hilo la Cameroon na Nigeria, vitendo hivyo vimekuwa vikitajwa katika mchezo wa soka barani humu huku vikielezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha maendeleo ya mchezo huo. Katika fainali za Afcon kwa vijana wenye umri wa miaka 20 zilizofanyika mwaka huu nchini Zambia, timu ya Taifa ya Senegal iliripotiwa kufanya vitendo hivyo katika mchezo ulioikutanisha na wenyeji hao.

Tukio lililowashitua wengi na kuzua mzozo kwa dakika kadhaa za mtanange huo ni ni lile la nyota wa Senegal, Ndiaye, kutupa kitu cheusi kwenye lango la Zambia, kitendo kilichosababisha alimwe kadi ya njano.

Pia, tuhuma za kishirikiana ziliwahi kumkuta straika wa Ghana, Andre Ayew, ambaye kamera za uwanjani zilimnasa akitupa kitu uwanjani dakika chache kabla ya mchezo wao wa Kundi D dhidi ya Misri ambao hata hivyo walichapwa bao 1 – 0.

Lakini je, ni kweli vitendo vya kishirikina vina mchango wowote kwenye mchezo wa soka? Mwaka 1974, Timu ya Taifa ya Zaire ilishiriki fainali za Kombe la Dunia ikiwa ‘imepikwa’.

Katika msafara wa timu hiyo, kulikuwa na ‘wazee’ lakini iliondoshwa kwenye michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani Magharibi ikiwa ndiyo timu iliyochapwa mabao mengi zaidi.

Mbali na hilo, hata straika Ayew alipotupa vitu uwanjani katika mchezo wa dhidi ya Misri bado timu yake ya Ghana ilichapwa bao 1 – 0.

Odion Ighalo wa Nigeria (kushoto), akijaribu kumtoka Michael Ngadeu wa Cameroon katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia uliomalizika kwa sare ya 1-1 wiki hii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.