Uzalendo gonjwa sugu linaloitafuna Taifa Stars

Rai - - MAKALA JAMSEIPITEMBA - NA MWANDISHI WETU

UZALENDO ni neno dogo tu lakini lenye maana kubwa sana. Unapozungumzia uzalendo

unazungumzia mapenzi ya dhati yasiyo na kificho juu ya kitu kinachomuhusu mtu.

Katika michezo suala la uzalendo limepotea sana hususani ule wa soka. Uzalendo unaoonekana kwa sasa ni katika klabu mbili kongwe nchini za Simba na Yanga tu.

Ukitaka kuona hamasa ya ushabiki hasa ikiambatana na uzalendo basi ziangalie klabu hizi mbili hasa pale zinapokutana kucheza mechi ya watani iwe ya kirafiki au mashindano yoyote.

Lile gumzo na vuguvugu la mechi huanza hata wiki kabla na kila mahali habari zinazotawala ni kuhusu pambanmo baina ya timu hizo.

Hamasa ya uwanja siku ya mchezo ni kitu kingine ambacho mara nyingi hubaki kuwa kumbukumbu kwa namna ambavyo mashabiki wa timu husika hujitoa. Haishangazi kuona au kusikia uwanja ukijaa kama siyo kufurika mashabiki.

Unaweza kuingiwa na mshangao sasa pale utapoona timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ inapocheza mechi zake si zile za kirafiki tu bali hata zile za mashindano.

Miezi kadhaa iliuyopita Taifa Stars ilicheza mechi yake ya kwanza ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afcon za mwaka 2019 kwa kupambana na Lesotho jijini Dar es Salaam, lakini mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walikuwa ni wachache.

Kama vile hiyo haitoshi mwishoni mwa wiki timu hiyo ilicheza pia mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, licha ya kushinda kwa mabao 2-0 lakini mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo walikuwa kiduchu sana.

Hamasa kidogo iliyopo inatokana na mapenzi binafsi ya mashabiki dhidi ya wachezaji wanaotoka katika timu zao.

Taswira ya haraka haraka inayoonekana kwa timu hiyo ni kwa mashabiki kukosa uzalendo kwa timu yao ya taifa. Lakini ni kwanini ifikie hali hiyo kiasi cha mashabiki kuichoka na hata kukosa uzalendo?

Wachambuzi wa masuala ya soka nchini wanaiona hali hiyo kama inasababishwa na timu hiyo kupata matokeo mabaya inapocheza mechi zake. Ni kama vile sasa wameichoka lakini je tujiulize vipi kwa timu zao hali huwa ni hivyo hivyo?

Wakati Kocha kutoka Brazil, Marcio Maximo akija nchini kuifundisha timu ya Soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilimchukua muda kuweza kurejesha na hata kujenga uzalendo kwa mashabiki wa soka hapa nchini kwa timu yao ya taifa.

Halikuwa jambo dogo hata kidogo lakini kutokana na dhamira yake kweli alifanikiwa kuwashawishi na hata kuondokea

kuwa na uzalendo dhidi ya timu yao ya taifa.

Kwa watanzania wengi nina amini watamkumbuka zaidi Maximo kwa jitihada hizo kwani alifanikiwa kwa asilimia kubwa sana mashabiki kurejesha uzalendo kwa timu yao ya taifa.

Mechi kati ya Taifa Stars na Cameroon au dhidi ya Brazi na hata Algeria zinaweza kuwa mfano tosha ambapo hamasa ya mashabiki ilikuwa ni zaidi ya mapenzi kwa timu ya taifa lao lakini leo hii hali ile haipo tena.

Miaka saba sasa toka kuondoka kwa Maximo uzalendo kwa timu ya taifa umepotea sana. Haishangazi kuona timu hiyo ikicheza katika ardhi ya nyumbani kana kwamba iko ugenini huku wachache wanaojitokeza wakilenga kuwafuatilia wachezaji wanaotoka katika timu zao hasa wale wa Simba na Yanga.

Je nini sababu zinazosababisha timu hiyo kushindwa kuungwa mkono na mashabiki wengi wa soka hapa nchini? Ziko sababu nyingi lakini kubwa ni matokeo mabovu inayokutana nayo kila inaposhiriki michuano mbalimbali.

Mashabiki wa soka siku zote hupenda matokeo. Huwa hawana uvumivu kabisa juu ya hilo na hali inapokuwa tofauti basi ni wepesi wa kukata tamaa.

Kimsingi bado kiwango kinachoonesha na timu hiyo kimekuwa cha kutilia shaka licha ya hivi karibuni kushinda mchezo dhidi ya Botswana.

Wengi kukata tamaa hata ya kwenda kuishuhudia inapocheza. Haishangazi kuona mashabiki wakifurika katika mechi za ligi lakini zinazoihusu timu ya taifa wakijitokeza wachache.

Lakini pia uteuzi mbovu wa kikosi hicho nayo ni sababu nyingine ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa mashabiki kutokana na ukweli kuwa wengi wanajua viwango vya wachezaji wengi kutokana na kufuatilia Michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo ndiyo msingi wa uteuzi wa timu hiyo.

Ukiangalia kikosi hicho unaweza kugundua kuwa uteuzi wake umebebwa na dhana ya siasa katika michezo wa soka kwa kuvikumbatia zaidi vilabu vikubwa vya Simba na yanga.

Makocha hawapati nafasi ya kuzunguka nchi zima achilia mbali kushuhudia mechi za Ligi Kuu kwa asilimia 80 ili kuweza kubaini hasa viwango vya wachezaji wengi.

Kosa la kwanza la kiufundi kwa timu hiyo linaanzia pale uteuzi ulipozingatia majina na sio uwezo halisi wa wachezaji.

Lakini pia kukosekana kwa uzalendo kwa makocha wenyewe na wachezaji kumesababisha kuwepo na pengo baina ya timu na mashabiki. Wachezaji au makocha hawana muda kabisa wa kujisogeza karibu kwa mashabiki ambao mwisho wa siku ndio wanaochagiza ushindi wao uwanjani.

Taifa Stars ile ya Maximo ilitingisha kwa sababu kocha mwenyewe alikwua mstari wa mbele kuhamasisha lakini leo hii hata baada ya mchezo ni nadra sana kumuona kwa mfano Salum Mayanga akienda sehemu ya mashabiki na kuwapungia japo mkono.

Lakini pia kukosekana kwa mipango na mikakati ya kweli juu ya ya timu hiyo ni moja kati ya sababu zinazowakatisha tamaa mashabiki.

Ukimya wa TFF katika kuifanyia promo timu pamoja na viongozi wa TFF wakiwemo wale wa Serikali kushindwa kujitokeza nayo imechangia mashabiki kuona timu hiyo si mali yao.

Si viongozi wa Serikali wala TFF wanaojitokeza hadharani kuendesha kampeni juu ya kusambaza upendo kwa mashabiki dhidi ya timu ya taifa lao.

Kipa wa Botswana, Mwambule Masule akiruka juu kuokoa hatari iliyoelekezwa langoni kwake wakati timu yake ilipocheza Tanzania, ‘Taifa Stars’ hivi karibuni. Taifa Stars ilishinda mabao 2-0.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.