Lissu aibua hofu mpya

Hatua hiyo inatokana na misimamo, uzalendo na kusema bila hofu kama ilivyokuwa kwa hayati Sokoine dhidi ya wahujumu uchumi katika miaka hiyo ya 1980.

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

UWEZEKANO wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kurejea katika hali yake ya kawaida unatoweka siku hadi siku kutokana na watu wasiojulikana kumshambulia kwenye maeneo hatari ya mwili wake hali inayoibua hofu mpya. RAI linachambua.

Hofu ya awali ilikuwa ni mwanasiasa huyo kupoteza uhai kutokana na kudaiwa kumiminiwa risasi nyingi kwenye mwili wake.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kwa sasa hakuna tishio lolote la shambulizi hilo kuchukua uhai wake, badala yake upo uwezekano wa kutoweza kutembea kabisa au kutembea kwa kutumia visaidizi.

Hofu hiyo inakuja baada ya vyanzo vya uhakika vya gazeti hili vilivyopo nchini Kenya, kubainisha kuwa Rais huyo wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), pamoja na kushambuliwa kwa risasi miguuni, tumboni na mikononi pia baadhi ya risasi hizo zimemvunja nyonga.

Taarifa hiyo ya kuvunjika kwa nyonga ya Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, imethibitishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji.

Dk. Mashinji amesema Lissu ambaye alipigwa risasi wiki iliyopita mkoani Dodoma na watu wasiojulikana, amevunjika nyonga, miguu yote miwili na mkono.

Akifafanua zaidi Dk. Mashinji alisema Lissu ambaye bado anapatiwa matibabu nchini Kenya, amevunjwa mguu wa kulia zaidi ya mara tano, mguu wa kushoto, nyonga na mkono wa kushoto.

“Tuliambiwa alipigwa risasi tano mwilini mwake, lakini kwa jinsi mwili ulivyobomolewa, yawezekana zilizidi. Risasi ni za kivita halafu ziupate mwili wa mtu, unategemea nini kitaendelea?

“Jana (juzi) saa 4 asubuhi, alianza kupata matatizo ya kifua, hali ilibadilika ikabidi madaktari wamwekee mashine ya kupumulia. mchana ilitengemaa wakaitoa.

“Madaktari walianza kumtibu sehemu za ndani ambazo zingeweza kuhatarisha maisha yake na wamemaliza. Awamu iliyofuata walianza kuunganisha mifupa kuanzia mkononi.

“Alifanyiwa upasuaji mara tatu, tumelazimika kusitisha operesheni ili aweze kupumzika. Wamemuumiza mno na tulitegemea atatibiwa kwa muda mfupi na kurudi nyumbani, lakini kwa namna alivyoumia, itachukua muda mrefu… naomba tujiandae kama chama,” alisema Dk. Mashinji.

Dk. Mashinji juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa hali ya Lissu ambaye pia ndiye Mwanasheria Mkuu wa Chadema imekuwa ikibadilika badilika na kwamba ameendelea kuongezewa damu.

“Bado najisikia uzito kuelezea jamii ya Watanzania hali ya Lissu inavyoendelea. Ni majonzi makubwa na kama kuna mtu katika taifa hili alifanya hicho kitendo, anatakiwa ajitafakari sana… inatia hasira sana,” alisema.

Dk. Mashinji alisema kutokana na tatizo lililompata Lissu, hali yake haitakuwa sawa kama alivyokuwa kabla ya kushambuliwa kwa risasi.

Daktari bingwa wa upasuaji kwa watoto wadogo Hospitali ya Selian mkoani Arusha, Dk. Catherine Mung’ong’o alisema jeraha lolote ndani ya nyonga linaweza kusababisha madhara makubwa ikiwamo kutembea kwa shida au kutotembea kabisa.

Akizungumza na RAI, Dk. Mung’ong’o alisema madhara hayo hutegemea na jeraha lililotokea kwa kuwa nyonga ni kubwa na inahusisha mishipa ya damu pamoja na ile ya fahamu.

“Shambulio linaweza kuwa limetokea kwenye mishipa ya damu au ya fahamu, lakini pia mishipa hiyo inauelekeo wake kuna mingine ni ya kwenye miguu, viungo vya uzazi na mambo mengine. Hivyo madhara hutegemea na mgonjwa mwenyewe kapata jeraha upande upi, lakini hakika madhara ni makubwa na anaweza hata kuparalyze (kiharusi) kwa kiwango kidogo, cha kati au kikubwa,” alisema.

Kauli hiyo ya Dk. Mung’ong’o inaungwa mkono na moja wa madaktari bingwa wa mifupa nchini ambaye amekataa jina lake na hata jina la hospitali yake kuandikwa gazetini.

Mtaalamu huyo, ameliambia RAI kuwa kuguswa kwa aina yoyote ile kwa nyonga kuna madhara makubwa kwa mhusika.

Alisema pamoja na nyonga kuwa ni eneo kubwa lililokusanya vitu vingi, lakini ndilo eneo linalomfanya binadamu yoyote kuweza kutembea, kukaa na kufanya shughuli zozote zinazohusiana moja kwa moja na mishipa ya fahamu na damu.

“Si rahisi kwa mtu aliyeshambuliwa nyonga kurejea katika hali yake ya kawaida ni miujiza tu ndio inaweza kumrejesha kwenye hali yake ya kawaida.

“Ukweli ni kwamba mtu aliyejeruhiwa nyonga ana nafasi kubwa ya kutotembea kabisa na kama ataweza kutembea basi atatembea kwa shida sana na hadi kufikia hatua hiyo inaweza kuchukua muda mrefu sana,” alisema.

HOFU YAWATAWALA WANASIASA

Hatua hiyo ya kushambuliwa kwa Lissu inatajwa kuwajaza hofu pia baadhi ya wanasiasa hasa wabunge wa vyama vyote vya siasa nchini.

Lissu alipigwa risasi wiki iliyopita na kujeruhiwa vibaya katika maeneo ya tumbo na miguu

Mwenyekiti wa Chadema Freema Mbowe, alisema katika risasi 32 zilizoonekana kushambulia gari la Lissu, risasi tano zilimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Kutokana na hali hiyo, hofu imejaa miongoni mwa wanasiasa na wasomi ambao tangu tukio hilo litokee mwishoni mwa wiki iliyopita waliweka bayana namna walivyoguswa.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kwa upande wake alionesha kuguswa moja kwa moja hali iliyomsukuma kuomba mwongozo wa Spika ndani ya Bunge akitaka kujua hali ya usalama wa nchi, kwa kuwa matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea nchini yanaonekana kutokuwa na hitimisho.

Mbunge huyo alisema “Mhe. Spika katika taifa letu katika kipindi cha muda mrefu kumekuwa yakitokea matukio mbalimbali ambayo sisi kama wawakilishi wa wananchi tunawajibu wa kupata taarifa sahihi juu ya muendelezo wa matukio hayo ambayo hayana hitimisho.

“Sisi tunawaakilisha Watanzania milioni 50 lakini matukio haya yanayotokea yanaharibu heshima ya taifa letu ningekuomba kama utaridhia na wabunge wataniunga mkono, uitake kamati yako ya ulinzi na usalama ya bunge tukufu ikutane na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuweze kupata taarifa kamili juu ya mambo haya yanayoendelea katika taifa letu, ili Watanzania na sisi wabunge tuwe na uhakika kwa sababu hali inavyoendelea hakuna mtu mwenye uhakika na maisha yake ya kesho,” alisema.

Aidha, katika kudhihirisha hofu hiyo, Spika wa Bunge Job Ndugai hakusita kukubali hoja na kutoa amri kwa kamati ya ulinzi na usalama ya bunge iende kukutana ili wapange ni jinsi gani ya kulishughulikia jambo hilo na watakapokuwa tayari kabla Bunge kuahirishwa kesho warudishe majibu juu ya walichoamua.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) naye hakuwa nyuma katika kubainisha hofu aliyonayo kuhusu tukio hilo.

Katika ukurasa wake wa Twitter Nape alibainisha alichoambiwa na Lissu wakati wakitoka Bungeni kabla ya kupigwa risasi mjini Dodoma.

‘Wewe Nape ni Mjomba wangu, kwanini unabaki CCM? Mimi na wewe tunafuatiliwa na jamaa zako wakitumia gari moja mimi na wewe ni watuhumiwa hama CCM mjomba’.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hakusita kuonesha hofu iliyotanda nchini na kubainisha kuwa Tanzania si mahala salama huku akiwaonya wabunge na wananchama wa upinzani kuchukua tahadhari.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari pamoja na mambo mengine alitoa mfano ya kifo cha Kamanda Mawazo huko Geita, kupotea kwa Ben saanane na kutekwa kwa baadhi ya watu.

Mbowe aliwataka wabunge wa upinzani kuwa na tahadhari kubwa akidai kuwa kama wasipokuwa makini huenda kiongozi mwingine anaweza kupata matatizo kama hayo hata hivyo amesema kuwa tamko la chama chake litakuja karibuni.

“Tutamuenzi Baba wa Taifa aliyetuasa: “tukiwa waoga tutatawaliwa ma madikteta!” Wabunge na viongozi wa upinzani ndiyo “Target”. Nawasihi viongozi na wabunge wetu wachukue kila tahadhari. Wanachama nao wawe tayari kulinda na kupigania wajibu wetu, usalama wa viongozi na chama chetu kwa ujasiri. Tusipochukua hatua, kesho atadhurika mwingine!Tamko na agizo rasmi la chama litafuata karibuni” alisema Freeman Mbowe.

Alisema Tanzania si sehemu salama tangu umefanyika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na kudai kuanzia hapo yalianza kujitokeza kwa mauaji ya viongozi, kutekwa wasanii na kufanyiwa mateso makubwa pamoja na wabunge kufungwa na kushtakiwa kila siku.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT –Wazalendo) ambapo kwa kupitia ukurasa wake wa twitter alisema watu ambao walifanya shambulio hilo la kinyama dhidi ya Lissu wamelenga kuwatisha wabunge na wanasiasa ambao wamekuwa mstari wa mbele kuongea mawazo yao.

“Watu waliomfanyia shambulio Lissu wamelenga kututisha kuzungumza mawazo yetu na mitazamo yetu, na kama tutaamua kukaa kimya watashinda, hivyo hatutakiwi kuwapa nafasi hiyo watu hawa, tunatakiwa kupinga udhalimu huu” alisema Zitto.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba licha ya kutoonesha hofu waziwazi, pia alidai kuwa amelielekeza Jeshi la Polisi kuweka vikwazo njia zote za kutoka Dodoma ili kufuatilia kwa njia tofauti na kuhakikisha wahalifu waliofanya tukio hilo wanatiwa mkononi na kufikishwa katika mkono wa sheria.

Hadi sasa Lissu ameshafanyiwa operesheni zaidi ya mbili nchini Kenya huku viongozi mbalimbali wakimiminika kwenda kumjulia hali akiwamo Waziri Mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

AFANANISHWA NA HAYATI SOKOINE

Aidha, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walienda mbali zaidi kwa kufananisha harakati za Lissu na zile zilizowahi kufanywa na Hayati Edward Sokoine.

Hatua hiyo inatokana na misimamo, uzalendo na kusema bila hofu kama ilivyokuwa kwa hayati Sokoine dhidi ya wahujumu uchumi katika miaka hiyo ya 1980.

Sokoine ambaye alifariki dunia kwa ajali ya gari, Aprili 11, 1984 inaelezwa kuwa ajali yake ilikuwa ya utata kama vile lilivyotokea tukio la Lissu.

Katika kipindi cha uongozi wake wakati akihutubia mkutano kikao wa NEC mjini Dodoma takribani miaka 33 iliyopita alisema “Ole wao wale wanaotumia nafasi zao za umma na serikali, kuiba, kuhujumu uchumi, kupokea rushwa, maana salama yao ni kudra za Mwenyezi Mungu labda nisiwajue”

Wachambuzi hao wanamnasibisha Lissu na Sokoine kutokana na mchango wake kwa Taifa, misimamo na mitazamo yake.

Hayati Sokoine aliamini katika haki, usawa na uwajibikaji, katika siasa za ujamaa zaidi ya siasa yeyote ile na kwamba maendeleo huja kwa watu kujituma kufanya kazi halali na bidii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.