Familia yachekelea kifo cha ‘mteka watoto’ Arusha

Rai - - MBELE - NA HARRIETH MANDARI, GEITA

SIKU chache baada ya baba wa kijana Samson Petro (18) anayedaiwa kuteka watoto jijini Arusha kugoma kuuzika mwili wa mwanae ameonesha kutosikitishwa na kifo cha mwanae huyo. RAI linaripoti.

Petro Aron (42), ambaye ndie mzazi wa kijana huyo aliliambia RAI kuwa familia yake haikushtushwa kwa sababu walijua mwisho wa mtoto wao hautakuwa mzuri kutokana na matendo yake maovu.

Samson aliuawa hivi karibuni kwa kupigwa risasi wakati akijaribu kuwakimbia Polisi alipokuwa amekwenda kuwaonyesha washirika wenzake wa utekaji katika eneo la Muriet Mkoni Arusha.

Kijana huyo alikamatwa mapema mwezi huu kwa tuhuma za kuteka mtoto mmoja Mkoani Geita na wengine sita Mkoani Arusha akishirikiana na wenzake ambao bado wanatafutwa na jeshi la polisi.

Kijana huyo alikamatwa kwa mara ya kwanza mkoani Geita katika kata ya Katoro baada ya kumteka mtoto Justine Ombeni (2) ambaye alijificha naye katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu iliyopo mjini Karoro mtaa wa Carlifornia.

Tukio la kutekwa kwa mtoto Justice, ambaye liliripotiwa kutekwa siku ya sikukuu ya Iddi nyumbani kwao eneo la Shilabela Mkoani Geita, alipokuwa akicheza na wenzake, alipatikana baada ya Polisi kufanikiwa kumkamata mtekaji.

Kabla ya kukutwa na mauti kijana huyo aliwaambia Polisi kuwa watoto wawili aliowateka aliwarudisha kwa wazazi wao baada ya kupewa malipo ya Sh.300,000.

Alisema wengine wawili aliwatelekeza mtaani baada ya wazazi wao kutotoa kiasi cha fedha walichotakiwa kutoa.

Kijana huyo alisema alijiingiza katika utekaji watoto kutokana na mahitaji ya fedha. Alisema aliacha shule akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lutozo iliyopo Katoro.

Baba mzazi wa kijana huyo Aron (42), mkazi wa Kata ya Katoro mkoani Geita, alisusa kuzika mwili wa mtoto wake kwa madai kuwa familia haikushitushwa na tukio la kifo hicho cha kijana wao kwani walijua ipo siku angeishia mwisho huo mbaya kutokana na aina ya maisha ya wizi na vitendo viovu alivyokuwa akijihusisha navyo kwa miaka mingi.

Alisema kijana wao huyo ni wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto saba, alianza tabia ya utukutu tangu akiwa mdogo na baada ya kushindikana kubadili mwenendo wake walimfukuza katika familia yao.

Marehemu Petro alizikwa na serikali wiki iliyopita ambapo wanajamii na familia waligoma kuufuata na kuuchukua mwili wa mtoto wao kwa madai kuwa alifariki dunia kutokana na kutenda vitendo vya kikatili ambavyo havifai katika jamii.

Katika mazungumzo yake na RAI, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema siku ya tukio mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake watatu ambapo alitokea mtekaji huyo, Samson Petro (18) ambaye aliwanunulia watoto watatu pipi na kasha kughilibu Justice kwa kumwambia aende naye dukani akamnunulie Sharubati (juisi) jambo ambalo mtoto huyo alikubali akafanikiwa kuondoka naye.

Kamanda Mponjoli akaongeza kuwa baada ya msako mkali wa tukio hilo ambalo liliambatana na tukio kama hilo lililoripotiwa Mkoani Arusha, Kikosi cha Polisi cha Geita pamoja na kikosi cha Arusha vilianza upelelezi kwa pamoja baada ya kubaini kuwa kuna viashiria vya mtuhumiwa Petro kuteka watoto mkoani Arusha kwa wakati mmoja.

Aidha, alisema mtuhumiwa huyo ambaye amebainika kufanya matukio kama hayo mara kadhaa, baada ya kumteka mtoto alituma ujumbe wa kitisho kwa mzazi wa mtoto uliosomeka “Msitume taarifa Polisi, mtoto wenu yuko salama endapo mtaripoti tutamkatakata mtoto wenu mikono na miguu”

Alitoa wito kwa wazazi na walezi mkoani Geita kuwa makini katika kuhakikisha usalama wa watoto wao hasa wadogo ambapo husababisha utekwaji kama ilivyotokea kwenye tukio hilo.

“Tusiamini watu kwa kuwaachia watoto wetu tunapotoka tuhakikishe watoto wapo katika mikono salama huku pia mzazi ukiendelela kufuatilia usalama wake kwa ukaribu”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.