Wizara ya Nishati yamaliza mawaziri

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

KUJIUZULU kwa mawaziri wawili hivi karibuni, kunaibua haja ya Rais Dk. John Magufuli kulifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri

KUJIUZULU kwa mawaziri wawili wa Serikali ya awamu ya Tano hivi karibuni, kunaibua haja ya Rais Dk. John Magufuli kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri aliloliunda Desemba 10, 2015, huku kiti cha Wizara ya Nishati na Madini kikionekana kuwa mwiba mkali kwa Mawaziri wanaokikalia. RAI linachambua.

Mawaziri waliojiuzulu mwishoni mwa wiki iliyopita ni aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani.

Wateule hao wa Rais walichukua uamuzi huo baada ya aliyewateua kutoa agizo la kuwataka wateule wake wote walioguswa na ripoti mbili za Kamati za Bunge zilizoundwa na Spika, Job Ndugai kuchunguza uchimbaji na uendeshaji wa madini ya Almasi na Tanzanite kukaa kando ili kupisha uchunguzi.

Ripoti mbili za Kamati ya Bunge zilizoongozwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (Madini ya Almasi) na Dotto Biteko mbunge wa Bukombe (madini ya Tanzanite), zilitaka Serikali iwawajibishe mawaziri wa zamani wa Wizara ya nishati na Madini ambao ni William Ngeleja, Profesa Sospeter Muhongo na Simbachawene.

Mhandisi Ngonyani anaingia kwenye dhahama hiyo baada ya kuliongoza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo alikuwa akishikilia wadhifa wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu.

Hatua hiyo inaibua uwezekano safu ya Baraza la Mawaziri ambalo tangu liundwe halijapanguliwa badala yake limepungua kutokana na kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Dk. Abdallah Posi, kutumbuliwa kwa Prof. Muhongo na kujiuzulu kwa Simbachawene na Mhandishi Ngonyani.

Kujiuzulu kwa Simbachawene na Ngonyani kunaifanya Wizara ya Nishati na Madini kuwa eneo la kazi hatari kwa mawaziri kwa kubeba historia mbaya kwa mawaziri wengi

waliopita kwenye wizara hiyo.

KUNA NINI NISHATI NA MADINI?

Wizara hiyo ni moja ya wizara za Serikali ya awamu ya nne na hata hii ya Tano zenye kuacha maswali mengi kwa Watanzania kwa kuwa mwiba mkali kwa mawaziri na watendaji wake.

Katika kipindi cha miaka tisa cha utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete na hata kwenye muda mfupi wa Rais Magufuli wizara hiyo imekuwa ikikumbwa na kashfa nzito zilizolisababishia taifa hasara.

Kashfa zilizoikumba wizara hiyo zimesababisha mawaziri wake kungolewa, hali iliyomlazimisha wizara hiyo kuongozwa na mawaziri wanne tofauti katika utawala wa Serikali ya awamu ya nne huku mawaziri watatu kati yao wakivuliwa nyadhifa zao baada ya kukumbwa na kashfa.

Katika utawala wa Serikali ya awamu ya Tano, tayari Wizara hiyo imeshamtesaProf.Muhongopamoja na kumsulubu Simbachawene na Mhandisi Ngonyani.

MAWAZIRI WALIOTESWA

Mawaziri walioiongoza wizara katika kipindi cha miaka tisa ya utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo, ambaye tayari amefungua milango ya mateso ya wizara hiyo.

Katika kipindi chote hicho wizara hiyo imekuwa kaa la moto kutokana na viongozi wake kudaiwa kuingia mikataba mibovu ama kuhusishwa na ufisadi.

Dk. MSABAHA NA KARAMAGI

Kumbukumbu zinaonesha kuwa jinamizi la wizara hiyo kuwa hatari lilianza kwa mawaziri wawili Dk. Msabaha na Karamagi, ambapo kwa pamoja walikumbwa na kashfa ya Richmond.

Kabla Rais wa awamu ya nne hajafanya mabadiliko ya Baraza la mawaziri Oktoba 2006, Dk. Msabaha alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, lakini baada ya mabadiliko hayo akakabidhiwa wizara ya Afrika Mashariki na Naziri Karamagi kukabidhiwa wizara hiyo.

Hata hivyo, tatizo kubwa la uhaba wa umeme, lililoibuka mara baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani na kuisababisha Serikali kusaka suluhu ya jambo hilo, ndilo lilifungua njia ya hatari kwa wakuu wa wizara hiyo.

Kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development (LLC) ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco).

Wakati Serikali chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa ikiamini kuwa Richmond, ndio tiba ya kweli kwenye janga la umeme, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa na kwamba kulikuwa na mchezo mchafu uliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Suala hilo lilifikishwa bungeni mwaka 2007, ambapo aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta aliunda Kamati Teule iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe kuchunguza.

Mwezi Februari, 2008 Kamati ilikamilisha jukumu lake na kuibuka na taarifa ilionyesha kuwapo kwa ufisadi, hali iliyomfanya Lowassa kuwajibika kisiasa.

Mbali ya Lowassa, pia aliyekuwa waziri wa wizara hiyo aliachia ngazi sambamba na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Msabaha.

NGELEJA

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ni mmoja wa mawaziri aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mine.

Ngeleja aliteuliwa Februari 13, 2008 na kuvuliwa wadhifa huo baada ya kuibuka kwa kashfa mbalimbali ikiwamo ya kudaiwa kushiriki katika uchangishaji wa fedha za kuwahonga wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wapitishe bajeti ya wizara yake ya mwaka 2011/2012.

Aidha, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyochunguza madai mbalimbali yaliyoelekezwa kwa waziri huyo ilibaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Ngeleja aliingia kwenye mvutano wa maneno na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Januari Makamba ambaye alifikia hatua ya kumuita waziri huyo ‘mzigo’.

Makamba alimshutumu Ngeleja kuwa ni waziri mzigo pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) William Mhando, baada ya kushindwa kutimiza ahadi ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme nchini.

PROFESA MUHONGO

Wakati Watanzania wakiwa wameyasahau yaliyowakumba Dk. Msabaha, Karamagi na Ngeleja, zimwi la kashfa lililomo ndani ya wizara hiyo lilimkumba Profesa Muhongo.

Waziri Muhongo ambaye hata katika utawala huu wa sasa ametumbuliwa kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Makinikia wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya nne Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilimtuhumu kulipotosha Bunge juu ya ufisadi wa fedha za Tegeta Escrow na kwamba hastahili kuendelea kushikilia wadhifa huo.

Shutuma kubwa zilizoelekezwa kwa Prof. Muhongo ni hatua yake ya kudai kuwa fedha za Tegeta Escrow si fedha za umma na kuwa ni halali kwa IPTL kupewa fedha hizo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya ripoti ya CAG na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kubainisha wazi kuwa kulikuwa na kasoro kwenye uhamishaji wa fedha hizo.

Wakati akiwasilisha ripoti bungeni, aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema hata mtu wa kawaida angeweza kujua kwamba washirika wa ‘Tegeta Escrow Account’ ni akina nani na masharti ya kutoka kwa fedha hizo kwenye akaunti ni yapi kwa

mujibu wa mkataba uendeshaji wa akaunti hiyo.

Mbali ya wizara hiyo kuwa hatari kwa mawaziri, lakini pia ni mwiba mkali kwa Makatibu wakuu, pamoja na watendaji wengine wa taasisi zilizo chini ya Nishati na Madini.

wa

ARTHU MWAKAPUGI

Mwakapugi ambaye alikabidhiwa wizara hiyo mwaka 2006, pamoja na kutovuliwa wadhifa wake wakati wa kashfa ya Richmond hadi pale alipostaafu mwaka 2009, alitikiswa kutokana na wizara yake kuguswa moja kwa moja na sakata hilo.

DAVID JAIRO

Jairo ni mmoja wa Makatibu wakuu wa wizara hiyo waliokumbwa na balaa ndani ya wizara hiyo baada ya kudaiwa kuchangisha fedha kiasi cha Sh. milioni 50 taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kuwagonga wabunge waipitishe bajeti ya wizara yake.

Sakata hilo lilisababisha Jairo kupewa likizo ya muda ili kupisha uchunguzi, hata hivyo hakurejeshwa tena kwenye nafasi hiyo na badala yake nafasi yake ikachukuliwa na Eliakim Maswi.

Moto wa wizara hiyo pia uliwagusa baadhi ya viongozi wa Tanesco, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wake William Mhando aliyekumbwa na kashfa mbalimbali.

DK. RASHID IDRIS

Dk. Idris ambaye alikuwa mkurugenzi wa Tanesco, alikumbwa na kashfa kadhaa zilizosababisha aandike barua ya kutaka kujiuzulu ambayo hata hivyo Rais Kikwete aliikataa.

Mkurugenzi huyo alikuwa mmoja wa watuhumiwa wa kashfa ya ununuzi wa rada ambayo iliyogharimu Sh bilioni 40. Pia alituhumiwa kumiliki kampuni ambayo ilikuwa na akaunti nchini Uingereza.

WIZARA YA ULAJI

Wakati wizara hiyo ikiwa ni hatari kwa mawaziri, RAI limebaini kuwa wizara hiyo ni kichaka cha baadhi ya vigogo serikalini ambao awali walionekana kuitumia kufanikisha biashara zao.

Simbachawene

Profesa Muhongo

William Ngeleja

Prof. Sospeter Muhongo

George Simbachawene

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.