Klopp aliwaacha Liverpool wapambane na hali yao

Rai - - MBELE - Inatoka uk 24

NDIO, ni kweli kabisa Liverpool ilibaki na ukiwa mara tu baada ya Sadio Mane kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Man City wikiendi iliyopita. Ila kocha wao, Jurgen Klopp alizidisha ukiwa huo kwa kupotea zaidi wakati vijana wake walipomhitaji kwenye wakati mgumu.

Klopp anasifika kwa kuwa kocha mhamasishaji sana, wafuatiliaji wa mpira wa miguu na wenye kuitambua historia ya Mjerumani huyo hawatopata shida kufahamu hilo. Ila kwenye mchezo huo, alijificha, hakutaka kuonekana kama mmoja wa wahanga wa kichapo cha mabao 5-0.

Huenda pengine kitendo cha kutoonesha ule mzuka wake wa kuwahamasisha wachezaji wake kilisababishwa na uamuzi wa refa, Jon Moss.

Huenda presha ya mchezo wenyewe ilimzidi ukijumlisha na uwezo wa hali ya juu wa wachezaji wa Man City uliivuruga akili yake na mara chache alionekana kuinuka kutoka kwenye benchi lake, lakini kwa kuvizia, kama aliyetaka kusema kitu lakini mdomo ukawa mzito.

Alikutana na Man City ambayo ilikuwa bora mchana wa Jumamosi iliyopita, City iliyokuwa bora kama ile Liverpool iliyoifunga Arsenal mabao 4-0 wiki chache zilizopita.

Utofauti wake uko sehemu ndogo tu, Arsenal ilipoteana ikiwa na wachezaji 11 ndani, na Liverpool baada ya kupunguzwa mchezaji mmoja. Lakini wote walipoteana. Na makocha wao vivyo hivyo.

Kadi nyekundu ile iliharibu mipango yote ya Liverpool, kwa kiasi kikubwa. Lakini, mbona Man City iliweza kuonesha utofauti katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Everton wiki chache zilizopita ambao mchezaji wao mmoja alioneshwa kadi nyekundu? Ndio tunakuja kugundua kwamba Pep Guardiola alifanikiwa katika kuwahamasisha vijana wake wajitahidi kuokoa jahazi.

Lakini kwa upande mwingine, Liverpool ilikutana na moja ya timu iliyo bora msimu huu, ilikuwa ni changamoto nzito kama sio jaribio la kwanza kubwa msimu huu.

Liverpool haikuhitaji kingine chochote siku hiyo zaidi ya morali. Hawana kikosi tunachoweza kusema ni bora zaidi kuwania mataji angalau matatu msimu huu. Katika Ligi Kuu ambayo ina timu tano hadi sita zinazowania taji, Liverpool walihitaji vikosi viwili vyenye wachezaji wasio wa kubahatisha na ndio maana Klopp anabaki kuwa mtu asiye na uwezo wa kukwepa lawama katika mechi kama hizi.

Kama alianzisha kikosi chenye mabeki kama Joel Matip aliyemchukua bure huko Schalke 04 Ujerumani, kinda Trent-Alexander Arnold upande wa kulia dhidi ya winga Leroy Sane, Ragnar Klavan, veterani huyo kutoka Ujerumani, dhidi ya Man City ambayo nayo ilikuwa ikihitaji ushindi kwa lazima, basi Klopp hakutakiwa kusahau jukumu lake la uhamasishaji.

Kikosi chake hicho hicho ambacho kilifanikiwa kutinga fainali ya Europa mwaka juzi, ndicho kilifanya kazi nzuri msimu uliopita lakini mara kwa mara kumekuwa na mapungufu ya kufanyiwa kazi ikiwemo safu ya ulinzi wa kati na kiungo.

Katika mtanange dhidi ya Man City, bao la kwanza kufungwa na Aguero, lilitokana na pasi ya Kevin De Bruyne, akiipitisha katikati ya Klavan na Matip.

Bao la Gabriel Jesus, lilitokana na krosi ya De Bruyne tena. Safari hii, straika huyo akifunga akiwa huru bila kubughudhiwa na yeyote ndani ya boksi la yadi sita.

Kwa mara nyingine, Jesus akafunga bao kutokana na pasi ya Aguero, jinsi gani mastraika hao wawili wa Man City walivyokuwa wakifanya mambo yao kwa uhuru mkubwa ndiyo inadhihirisha kuwa Liverpool ina walinzi wasiokuwa makini, kama sio ubora hafifu.

Ukiachana na hayo mabao, safu ya kiungo ilikuwa nyanya sana kwa upande wa Liverpool. Mipira kadhaa ilikuwa ikipotezwa katikati na nahodha, Jordan Henderson.

Nini anachotakiwa kukifanya Klopp kwa wakati huu? Ni kutowaacha vijana wake wapambane na hali zao wenyewe, na yeye anatakiwa kuungana nao bila kuchoka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.