WENZETU WANAKWENDA SAYARI NYINGINE, SISI TWENDE VIJIJINI

Rai - - MBELE -

Ninamalizia mfululizo wa makala hii ambayo kimsingi inaweza kuwa ndefu zaidi ya vile nilivyo irefusha. Safari ya kwenda kijijini ni safari isiyo na mwisho. Vijiji vingi kama nilivyokwisha eleza kuwa vinakabliliwa na hali mbaya ya umaskini uliokithiri.

Mfululizo wa makala haya ya safari ya kijijini imenipeleka kijijini. Naam, Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS) wamenipeleka kijijini kujionea hali halisi ya masiha ya kijijini sambamba na changamoto zinazowakabili wananchi waishio vijijini. Mradi huu unafanya kila liwezekanalo kuhakikisha katika vijijini vinne katika Halmashauri ya Morogoro, vinaondokana na umaskini ulikithili na kuweza kumudu kutunza misitu yao ya asili na kuzalisha mazao ya kilimo kwa tija kwa lengo la kujikwamua na umaskini wa kipato. Nimekwenda pamoja na kufanya ziara ya siku nne katika vijiji kumi vya Halmashari ya Wilaya ya Morogoro. Mimi na wadau wa TTSC kwa pamoja tulikwenda kwenye vijiji wa Tafara ya Ngerengere, Kata za Matuli na kata ya Tununguo ambako binafsi nimejifunza na kujionea hali halisi ya maisha ya wakati wa vijijini.

Nilichokishuhudi huko ni changamoto nyingi ambazo zinawakabli wananachi waishio katika maneeo hayo. Changamoto ya mwingiliano kati ya wakulima na wafugaji ni moja ya mambo yanayowakatisha tamaa wananchi kuzalisha mazao ya chakula na Biashara. Vijiji vya Mlilingwa, Matuli na Diguzi na vitongoji vyake vyote vinakabiliwa na hali mbaya ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Wananchi katik vijiji hivyo kwa miaka mingi wamekuwa wangiingia matatani na hali ya kutoelewana kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wote kwa pamoja wanalalamikiana kuwa ni chanzao cha uharibifu wa mazao na mifugo.

Mifugo imekuwa ikilishwa katika mashamba ya wakulima kipindi ambacho mazao ya kilimo yapo shambani. Wafugaji mara nyingi wamekuwa wakifanya hivyo na hata kuwatisha wakulima na kulisha mifugo yao kwa lazima katika mashamba ya mpunga, mahindi na mazao mengine. Wakulima nao wamekuwa wakimwaga sumu kwenye majani ili mifungo idhurike. Inariprtiwa kuwa mamia ya mifugo imekufa kwa kula nyasi ambazo zimewekwa sumu na wakulima kwa lengo la kulipiza kisasi.

Wakulima wanalalamika kuwa wafugaji wanapendelewa na mamlaka za utoaji wa haki. Wanalaamika kuwa pindi waendapo kwa mtendaji, polisi au mahakamani, wafugaji hushinda kesi au wanalipishwa viasi vidogo vya pesa visivyolingana na thamani halisi ya mazao yao yaliyoharibiwa. Hali hii imekuwa ikizua uhasama na hali ya kutoelewana baina ya wakulima na wafugaji si katika maeneo ya vijiji vya Tarafa ya Ngerengere tu bali ipo maeneo mengi nchini kwetu. Wananchi wa kata za Matuli na Tununguo kwa kiasi kikubwa wanashukurumradi ulioletwa na TTCS wa Mkaa Endelevu na Kilimo Hifadhi ambao kwa pamoja umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya baina ya wakulima na wafugaji kwani mradi huo umepanga matumizi bora aya ardhi sambamba na mipaka ya maeneo ya kilimo na ufugaji.

Wapo wafugaji na ambao hawaheshimu mipaka yao ya kuchungia na wameendelea kuwa kikwazo katika juhudi za wakulima. Hapa serikali kwa muktadha ule ule wa kwenda vijijini una kila sababau ya kwenda katika vijiji hivi kukomesha tabia hii ya wafugaji na wakulima ambao wameshindwa kuheshimu mipaka ya shughuli zao za kilimo na ufugaji. Baadhi ya wakuliwa waliacha kulima kabisa au kulima maeneo madogotu kwa hofu ya kuharibiwa mazao yao na mifugo. Pia wapo wafugaji ambao walihama aua kufilisika kabisa kutokana na mifugo yao kufa kwa kuwekewa sumu na kuuwawa na wakulima pindi wanapoingia katika maeneo ya mashamba.

Safari ya Kijijini imenipelekea kubaini kwa kushuhudia kwa macho adha kubwa wanayoipata wananchi wa vijiji vya Kisanga Stendi, Mlilingwa na vitongoji vya Ruvumo na Lung’wamanzi. Katika maeneo hayo kuna adha kubwa mno ya upatikanaji wa maji safi na salama. Katika vitongoji vya Lung’wamanzi na Ruvumo hakuna chanzo chochote cha maji safi. Hapa wananchi wanakunywa maji yanayopatikana katika kisima kilichochimbwa kwa mkono ambacho kimsingi ni kisima kimoja tu kinachotumika na wananchi zaidi ya 700. Adha ya maji katika kijiji hiki ni kubwa na kuelezea hakutoi taswira halisi ya hali ilivyo. Wananchi wa Vitongoji vya Lung;wamanzi na Ruvumo, katika kata ya Tununguo wanakabiliwa na adha nyingi ikiwemo ukosefu wa zahanati na shule. Wananchi hawa wanatembea umbali wa kilometa 7 mpaka nane katika msitu mnene kufuata huduma za zahanati na shule. Hapa watoto wengi hawasomi kwa kuwa shule ipo mbali sana. Shule ya msingi ipo kijijini Mlilingwa ambako kuna umbali wa kilometa saba toka vitongojini hapo. Halikadhalika zahanati ipo umbali unaofafana na huo. Ni adha kubwa inawakabili wananchi wa vitongoji na kijiji cha Mlilingwa kwa ujumla. Umbali wa kutoka kijijini Mlilingwa mpaka katani Tununguo ambako kuna shule ya kata ni zaidi ya kilometa 20. Sekondari hiyo ya Tununguo haina hosteli za wanafunzi. Wanafunzi hulazimika ama kupanga vyumba maeneo jirani na shule au wengine hulazimia kutembea umbali wa kilometa 30 kwenda na kurudi shule kila siku.

Hali hii imesababisha wanafunzi wengi hususani wa kike kushindwa kufanikiwa kumaliza masomo yao. Hata baadhi ya watoto wa kiume huacha shule kwa kuwa wanashindwa kumudu kwenda shule na kurudi kila siku katika umbali huo na kupita katika msitu mnene kila siku.

Zipo changamoto nyingi katika kata hiyo, Mfano, zahanati iliyopo kijijini Kisanga inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahudumu wa afya. Zahanati hiyo inayotegemewa na wananchi zaidi ya vijiji vitano ina mganga mmoja tu na haina muuguzi hata mmoja. Mganga huyo akienda semina au akipata dharura yoyote ile iwayo, zahanati hiyo hufungwa na wananchi kupatwa na adha kubwa mno ya tiba hususani kwa watoto na akina mama wajawazito. Umbali wa kutoka katani Tununguo mpaka Tarafani Ngerengere ni zaidi ya Kilometa 30.

Maeneo mengi vijijini watendaji wa vijiji na kata wamegeuka miungu watu. Hawa katika maeneo yao ya utawala huwakamata wahalifu, huwafyngulia kesi na kuwatoza viasi vikubwa vya pesa. Hawatumii mashine za EFD, na wamekuwa ni wabadhirifu wakubwa. Watendaji wa vijiji na kata baadhi ya maeneo wamekuwa ni wabadhirifu wakubwa na waonevu kwa wananchi wao. Katika baadhi ya vijiji wenyeviti wa vijiji kwa kushirikiana na watendaji wamekuwa wakiuza ardhi kubwa kinyume na taratibu. Mara nyingi wamekuwa wakisababisha migogoro mingi ya ardhi na kuleta adha kubwa.

Hali halisi ilivyo vijijini ni mbaya, huo ni mfano mmoja katika mfano mingi inayokabili vijiji hapa nchini kwetu. Kama nilivyokwisha toa wito kuwa wakati wenzetu wanakwenda sayari nyingine, sisi twende vijijini. Tuna kila sababu ya kwenda vijijini kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini. Serikali iandae mkakati kabambe wa kuviwezesha vijiji vyetu kwani maelfu ya waTanzania wanaishi vijijini na wanakabiliwa na hali mbaya ya maisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.