TUNA MENGI YA KUJIFUNZA UCHAGUZI KENYA

Rai - - MBELE -

Mapema wiki hii Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, ambaye alikuwa mmoja miongini mwa watazamaji wa nje katika uchaguzi wa Kenya mwezi uliopita amesema hakuna chochote kipya cha kujifunza kutoka uchaguzi huo wa Kenya.

Jaji huyo amenukuliwa katika mahojiano na gazeti moja la kila siku kwa lugha ya Kiswahili akisema hata maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo (Supreme Court) ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi ni ya kawaida na yangeweza kutolewa hata hapa nchini endapo Katiba na sheria zingekuwa zinaruhusu jambo hilo.

Aliongeza kwa kusema si sahihi kusema kwamba hapa Tanzania majaji au watendaji hawako huru eti tu kwa sababu wanateuliwa na Rais na akasisitiza kuwa wanafanya kazi zao kwa uhuru na wamewahi kufanya maamuzi makubwa ambayo ni kinyume na matakwa ya Serikali au chama tawala.

Alitolea mfano wa ile kesi ya uhaini ya Zanzibar ambayo mahakama ya Rufani ilikuja kutoa uamuzi wa kuwaachia huru watuhumiwa, kwa kutaja Zanzibar si nchi kamili.

Tukiacha hilo suala la hapa kwetu kutowapo kwa mazingira tofauti yasiyoruhusu hayo yaliyojiri Kenya kutokea, sikubaliani naye kuhusu kitu kimoja – ile azma nzima itokanayo na taaluma yake – ya kutenda haki, kwani haki ina misingi yake, haihitaji mazingira yoyote ya kiutawala.

Jaji Lubuva, kama Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu bila shaka anaufahamu msingi mkuu wa kutoa haki unaosema: “Si kwamba haki itendeke tu, bali pia ni lazima ionekane inatendeka” (justice must not only be done but must also seen to be done).”

Msingi huu ulitokana na maamuzi ya Jaji Mkuu wa Uingereza, Gordon Hewart mwaka 1924 kwamba kuonekana tu kwa chembe ya upendeleo (appearance of bias) katika mwenendo mzima wa kesi ni tosha kabisa kupindua uamuzi wa mahakama. Msingi huu ndiyo unatakiwa kuwa mlinzi mkuu wa uhuru wa mahakana na hivyo kujipambanua katika ubora wake.

Napenda tu kumwambia Mheshimiwa Jaji Lubuva kwamba pamoja na anavyosema, naamini tunavyo vya kujifunza kutoka Kenya. Tuchukulie mfano wa nchi hiyo kuhusu uteuzi wa Jaji Mkuu kwamba ni tofauti kabisa na hapa kwetu. Uteuzi wake (pamoja na wakuu wengine wa vyombo vya dola na kadhalika) una mchakato mrefu wa kusaili wagombea kupitia tume husika kwa kazi hiyo na hatimaye Rais wa nchi hupewa jina la kutangaza na baadaye kuthibitishwa na Bunge.

Na ni ukweli hili linawezekana Kenya kwa sababu ya Katiba yao mpya. Bila shaka anaamini kwamba njia hiyo ndiyo aina bora ya kumpata Jaji Mkuu. Na kama anaamini hivyo kuliko ilivyo hapa kwetu basi haoni kwamba hicho ni kitu cha kujifunza – kwa kupigia debe upatikanaji wa Katiba mpya itakayosheheni vitu bora pamoja na hicho?

Na tunaweza kabisa kuwashinda hata Wakenya kwa kupata Katiba mpya kwa njia ya amani kabisa, kuliko namna walivyopata wao – ambayo ilikuwa baada ya ghasia kubwa na za umwagaji damu. Hata lile suala la kupinga ushindi wa rais mahakamani, ambalo naamimi Mh Lubuva anakubaliana nalo, tunaweza kulipata kupitia Katiba mpya kama anavyosema.

Aidha hakuna haja ya kusema hapa kwamba ghasia hizo hizo zilizotokea zilitokana na uamuzi ambao haukuwa wa haki kuhusu uchaguzi wao mkuu wa mwaka 2007, kwani yalitokana na mazingira yasiyokuwa ya haki. Tungoje nasi yatufike hayo ili tuwe na mfumo bora kama wao?

Na tukiwa katika suala hilo hilo la uchaguzi, Mh Jaji Lubuva alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa zaidi ya miaka sita (kuanzia 2011) na kusimamia uchaguzi mkuu wa 2015.

Aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mkuu wa chama cha siasa kilichoingia katika ushindani mkuu wa kisiasa dhidi ya vyama vingine vya siasa. Bila shaka aliyebuni ulazima kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa na sifa za ujaji wa Mahakama Kuu aliyafikiria masuala mbali mbali likiwemo hili la msingi mkuu wa kutoa haki niliyoutaja hapo juu.

Kwa maneno mengine katika sehemu ya pili ya msingi huo wa haki, haki haitaonekana kutendeka kwa sababu uteuzi wa ‘mtoa haki’ huyo ulifanyika kwa namna ambayo kimuonekano wake hauwezi kutarajiwa kutenda haki. Kuna mwonekano wa upendeleo pale (appearance of bias), mfumo ambao kwa Kenya ilikuja kuwaumiza na hivyo wakaamua kuondokana nao. Kwa hiyo hata hayo Jaji Lubuva anayosema (kuhusu NEC) kwamba pamoja na kuteuliwa na Rais kuna maamuzi mengi wamewahi kufanya na Rais na vyombo vya usalama havikuingilia yanapingana na ule ule msingi mzima wa utoaji haki – kwamba tangu mwanzo mtoa haki hakuchaguliwa kwa namna ambayo ingemwezesha kutoa haki bila kuingiliwa, hata kama hakuingiliwa na mamlaka zilizomteua.

Kuhusu watazamaji wa nje wa uchaguzi wa Kenya ambao yeye alikuwa mmoja wao Jaji Lubuva alisema wao waliona uchaguzi huo ulikuwa huru na haki, lakini Mahakama ya Juu iliona tofauti kutokana na kasoro zilizobainika kuwa za jikoni ambako watazamaji hawaingii.

Katika teknolojia ya sasa inayoendelea kwa kasi ambayo imeingia pia katika michakato ya uchaguzi ni dhahiri udanganyifu na wizi wa kura unafanyika sana kupitia teknolojia na ambayo si rahisi kugundulika kupitia “utazamaji” uliozoeleka.

Hivyo ni vyema kauli za watazamaji hawa ziwe angalifu zaidi, na kwamba kuanzia sasa kuwepo kwa haja ya kutazama ‘jikoni’ pia. Vinginevyo dhana nzima ya ‘utazamaji’ katika uchaguzi inakuwa haina mantiki kabisa.

Mwaka 2005 kauli ya ujumbe wa watazamaji kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu uchaguzi wa Ethiopia kwamba haukuwa wa huru na haki baada ya chama tawala kutangazwa kushinda iliwaingiza wapinzani mitaani Addis Ababa na miji mingine katika maandamano makubwa ambayo yalisababisha mauaji ya mamia yao baada ya kukabiliwa na vikosi vya askari wa utawala.

Kuanzia hapo watazamaji wa EU wamekuwa waangalifu sana na kauli zao hasa pale wanaposema uchaguzi haukuwa huru na haki. Kwa mfano iwapo wangesema hivyo kuhusu uchaguzi wa Kenya – kwamba haukuwa huru na haki – pengine ghasia kubwa zingeibuka.

Aidha hakuna haja ya kusema hapa kwamba ghasia hizo hizo zilizotokea zilitokana na uamuzi ambao haukuwa wa haki kuhusu uchaguzi wao mkuu wa mwaka 2007, kwani yalitokana na mazingira yasiyokuwa ya haki.

Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.