Matukio haya yadhibitiwe haraka

Rai - - MAONI/KATUNI -

MWENDELEZO wa uhalifu wa kutumia silaha kwa kushambulia watu wa kada mbalimbali ni jambo lisilopaswa kupuuzwa kwa namna yoyote ile.

Katika kipindi kifupi Watanzania wameshuhudia vifo vya watu vilivyotokana na kupigwa risasi pamoja na majeruhi waliojeruhiwa na silaha za moto.

Jambo baya zaidi yote hayo yanatokea huku wahusika wakiwa hawajulikani, hali hiyo imekuwa ikiibua hofu na mshaka kwa Watanzania ambao kimsingi hawakuzoea kushuhudia hali hiyo.

Ukweli ni kwamba hadi sasa haijawekwa wazi ni mtu, watu, kikundi au vikundi gani vinavyotekeleza uhalifu huo muda wowote wanaotaka wao.

Watanzania wameyashuhudia hayo mkoani Pwani kwenye maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, raia na askari kwa nyakati tofauti waliuwawa kwa kupigwa risasi.

Hali ile iliibua taharuki kubwa kwa wananchi ambao kwao lilikuwa ni suala jipya kwani hawakuwahi kukutana na hali ile tangu nchi hii kupata uhuru.

Mioyo ya wakazi wa maeneo hayo ilikufa ganzi, shughuli za kiuchumi zilizorota na kudorora kwa sababu ya tishio la kuuwawa bila hatia.

Tunaamini mMauaji hayo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) yamedhibitiwa vyema na vyombo vya Ulinzi na Usalama na tunapongeza kwa hatua hiyo.

Wakati suala la Mkiru likiwa limedhibitiwa, sasa umeibuka uhalifu mpya wa kuvamia ofisi za mawakili, kushambulia wanasiasa na viongozi wastaafu.

Hili si jambo jema, halipaswi kuachwa limee ndani ya nchi yetu, tunaamini Jeshi la Polisi nchini linaouwezo mkubwa wa kuwasaka na kuwakamata wahusika wote wa kadhia hizi.

Si jambo jema kuwaacha waendeleze uhalifu wao huu, unaweza kukaribisha makundi makubwa ya kihalifu kutumia mwanya huu kupenyeza mambo yao.

Tunaliomba jeshi la polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini kuhakikisha inatokomeza uhalifu wa namna hii ambao unaharibu sura nzuri ya nchi yetu mbele ya uso wa dunia.

Aidha tunaungana na viongozi wote wa dini na taasisi nyingine, zilizotoa wito kwa Serikali kulichukulia suala hili kwa uzito na umakini wa hali ya juu.

Tunaunga mkono maoni ya baadhi ya Wabunge, ambao wameonesha kukerwa na vitendo hivi ambavyo vinashiria kuvuruga amani na utulivu wan chi yetu.

Haileti maana kama vyombo husika vitaacha wahalifu hawa waendelee kutamba ndani ya nchi yetu yenye uongozi imara na makini.

Tunayo imani kubwa na Jeshi la Polisi, tunajua lina watu wenye uzoefu mkubwa katika medani ya upelelezi. Uzoefu huo ni vema ukatumika kuwabaini na kuwadaka hawa watu wanaofanya uhalifu huu.

Tunaishauri Serikali kutofumbia macho suala hili la usalama wa maisha ya raia wake na mali zao.

Mambo haya ya mauaji, kupotea kwa watu na mashambulizi kutoka kwa “watu wasiojulikana” ni mwenendo mbaya kwa nchi na Serikali.

Tunaliomba jeshi la polisi kutumia weledi wake katika masuala ya kukamata wahalifu kushghulikia mambo haya ili yasiote mizizi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.