Vita vya kiuchumi bila mahakama imara ni bure

Rai - - MAONI/KATUNI - NA MOSES NTANDU

KATIKA hali ya kushangaza, Mahakama ya Tanzania ina mipango na mikakati mizito katika kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha haki kwa wote inapatikana kwa wakati, lakini jamii haielewi chochote juu ya haya na vyombo vingi vya habari vipo kimya katika kutoa elimu hiyo.

Mahakama ya Tanzania ina mamlaka kamili ya utoaji wa haki hapa nchini kama ilivyofafanuliwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sura ya tano kuanzia ibara ya 107 hadi 123, kuwa Mahakama ya Tanzania ni mhihimili unaojitegemea katika kutenda kazi zake, ukiwa na dhima ya utoaji wa haki pamoja na mambo mengine ya kisheria kwa wakati husika.

Katikamakalahiinitazungumzia mipango, mkakati na jitihada zinazofanywa na mahakama katika kile kinachoelezwa ni uboreshaji wa huduma za kimahakana nchini kwa miaka mitano toka mwaka 2015 hadi 2020, ingawa jamii kwa kiwango kikubwa sana hawana uelewa wowote juu ya upatikanaji wa haki zao na hata hii mipango mizuri jamii haijaweza kufahamishwa ipasavyo.

Kwa kweli katika kipindi hiki tunapaswa kuona mahakama ikifanya kazi kwa kiwango cha juu sana ili kuchangia katika juhudi zinazoendelea kwa sasa nchini za ukombozi wa kiuchumi na mapambano dhidi ya waporaji wa rasilimali za nchi. Vita hii inaongozwa na Rais John Magufuli.

Kuna mambo mazuri sana yanaendelea katika mikakati ya kuboresha mahakama katika mpango mkakati huu wa miaka mitano, lakini kilichonistaajabisha ni kwamba mambo haya yanakwenda kimya kimya bila umma kwa ujumla kufahamu na kuwa karibu kwani wao ndio wadau wakuu wa jitihada zote hizo.

Septemba 21, mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa taasisi za umma na vyombo vyote vya Serikali kuhakikisha wanasogeza huduma za kijamii karibu na wananchi ili kuchangia katika upatikanaji wa huduma za kijamii kwa karibu na kwa gharama nafuu, hii yote ni njia pia ya kuchangia katika uboreshaji uchumi wa nchi.

Waziri Mkuu alitoa wito huo alipokuwa akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ambao unalenga kuboresha huduma za mahakama nchini. Mpango ambao ni wa miaka mitano kwa kipindi cha 2015 – 2020, pamoja na mpango mkakati huo pia alizindua Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama.

Katika matarajio yaliyowekwa katika mkakati huo wa uboreshaji huduma za mahakama nchini, ni pamoja na kuongezwa kwa uwajibikaji na utoaji wa huduma za kimahakama kwa wakati. Katika uzinduzi huo, utoaji wa huduma za mahakama ulikadiriwa kuwa ni asilimia 20 kwa mwaka wa 2015/16 na ilikadiriwa kuwa maboresho hayo yatasaidia kupandisha uwajibikaji na utoaji wa huduma hadi kufikia asilimia 40 kwa mwaka 2016/17, pia hali hiyo ilitazamiwa kuongezeka zaidi kwa kadiri siku zitakavyokuwa zikisonga mbele.

Kufikia 2018/19, inaelezwa kuwa maboresho hayo yatapanda hadi kufikia asilimia 60 na yatafikia kiwango cha asilimia 70 hadi 100 kwa mwaka 2019/20.

Katika maboresho hayo ya 2015– 2020, yanahusisha miradi kadhaa ikiwepo ya maboresho ya huduma za mahakama ya Tanzania na pia ujenzi wa mahakama za wilaya ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo; miradi hiyo imegharimu kiasi cha Sh bilioni 139.5, fedha ambazo zilitolewa na Serikali kutoka bajeti yake ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Pia katika mikakati hiyo ya mahakama, ilielezwa kuwa kutakuwa na ujenzi wa mahakama kuu kati ya tano hadi saba katika kipindi cha miaka hiyo mitano ijayo ya maboresho ya huduma za mahakama.

Kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja toka uzinduzi wa mkakati huo, kuna mabadiliko kadhaa yamejitokeza ikiwa ni pamoja na ongezeko la kiutendaji na miundombinu ya mahakama, ikiwa inaendelea kuimarika kwa ukamilishaji wa mairadi mingi ya ujenzi wa mahakama za mwanzo, wilaya na maboresho ya mahakama kuu pia.

Hali kadhalika ilielezwa kuwa kuna changamoto kadhaa zinazoikabili mahakama katika mkakati huu ambapo ilielezwa kuwa ufinyu wa bajeti, uchache wa majiji, kutokupatikana kwa sheria zinazoleta changamoto za ucheleweshwaji wa uandikwaji wa hukumu, ongezeko la makosa ambayo huchangia mrudikano wa kesi nyingi mahakamani, uwezo mdogo wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia kwa watumishi na pia uelewa mdogo wa umma kwa masuala ya uongozi wa kimahakama na mienendo yake.

Katika hali hii mahakama imejikuta ikibeba lawama nyingi kutoka kwa umma kuwa imekuwa ikichelewesha kesi nyingi na hata pia kulalamikiwa kuwa na uwezo mdogo wakati tatizo hili lipo kwa uuma pia kutokuwa na uelewa wa masuala hayo.

Hapa suala kubwa ambalo linapaswa kutatuliwa pia ni kuhakikisha kuwa umma unapewa elimu ya kutosha juu ya masuala haya ya kimahakama ili waweze kuchangia pia katika kuboresha upatikanaji wa haki na uboreshaji wa masuala yote yahusuyo mahakama na utendaji wake.

Pamoja na hayo, pia mahakama inakabiliwa na changomoto za kiutendaji ambazo ni pamoja na kutokuwa na watendaji wenye taaluma ili kuweza kukabiliana na ongezeko la wingi wa kesi, kuna tatizo pia la udhaifu wa kutunza kumbukumbu na pia kutokuwa na uwezo wa kiteknolojia na taarifa za kesi.

Uhaba wa vifaa vya kutendea kazi na miundombinu ya mazingira ya kazi pia vimekuwa ni miongoni mwa vikwazo vya utendaji wa kazi pia kutokuwepo na maktaba ya kisasa ya kielekroniki. Hali kadhalika udhaifu wa uwajibikaji na utawala katika mfumo wa taarifa katika taasisi ya mahakama.

Pia matukio ya kukiukwa nidhamu na masuala ya rushwa yanatajwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili mahakama katika utendaji wake.

Haya yote yanapaswa kukabiliwa na kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na kuihusisha jamii nzima ya Watanzania ili kutambua kuwa mahakama pekee haiwezi kutatua changamoto zote zinazoikabili bila ushiriki wa jamii na umma kwa ujumla. Pia Serikali inapaswa kuwekeza kwa kadiri iwezavyo kifedha na kuisaidia mahakama kuweza kutoa elimu ya kutosha kwa umma kama sehemu ya maboresho ya mikakati yake.

Vita hii ya uchumi tuliyo nayo kwa sasa kama ajenda kuu ya Taifa, haitafanikiwa ikiwa mahakama itakuwa nyuma kwani mahakama ndicho chombo pekee kinachoweza kusaidia katika suala ka kutoa haki ya rasilimali zote zilizoporwa hapa nchini.

Serikali kuu pekee haiwezi kufanikiwa katika hili, ikiwa mahakama itakuwa dhaifu na kutokuwa na uwezo kwa kukabiliana na changamoto zake zote hizo, ikumbukwe kuwa uibuaji wa makosa ya uporaji wa rasilimali nako kunachangia kuongeza wingi wa kesi mahakamani kama mahakama itaendelea kuwa na changamoto zote hizo tusitegemee kuwa tutafanikiwa kwa urahisi katika vita hii bila kuwa na mahakama imara.

Pia kwa upande wa mahakama pamoja na kuwezeshwa pia mahakama ihakikishe kuwa inaboresha huduma kwa kuchukua hatua kadhaa za kudhibiti nidhamu ya kazi hasa katika masuala ya rushwa ambayo yamekuwa ni doa kubwa kwa mahakama yetu kwa miaka mingi sana kuanzia mahakama za mwanzo hadi mahakama kuu.

Ili kufikia malengo hayo waliyojiwekea, ni bora sekta na wadau kupewa kipaumbele ili kuhahakisha juhudi hizi zinapelekwa mbele kwa pamoja kwa ushirikiano wa vyombo vya habari, wadau wa sheria na asasi za kiraia na wadau wengine wa mahakama, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa kushirikiana kwa pamoja ikiwa wanaunganishwa vyema na mahakama ili kuhakikisha mpango mkakati huu unafanikiwa kwa kila nyanja za utiaji wa elimu na taarifa ili kufikia asilimia 100 ya uboreshaji wa mpango wa mahakama. Mwandishi wa Makala hii ni Mtafiti na Mwandishi katika kituo cha kutolea taarifa Tanzania, (TCIB) anapatikana kwa namba ya simu 0714 840656 baruapepe mosesjohn08@yahoo.com.

Rais John Magufuli akimuapisha Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.