BioShape wameacha sononeko

Rai - - MAONI/KATUNI -

Utele.

JIO wa Kampuni ya BioShape mwaka 2006, wilayani Kilwa mkoani Lindi, ulikuwa wenye heri na furaha Kwa namna walivyotua nchini wakiwa na ahadi kedekede isingekuwa rahisi kwa mwananchi wa Kilwa hasa katika vijiji vya Mavuji, Nainokwe, Liwiti na Migeregere angekuwa tayari kukusikiliza neno lolote baya linaloihusu kampuni hiyo hiyo ya kigeni kutoka Uholanzi.

Kampuni hiyo ilitua nchini kwa lengo la kuzalisha mafuta kwa kutumia mbegu za mibono. Uzalishaji huo ulitajwa kuwa salama kwa mazingira.

Kiasi cha dola milioni 9.6 kilidaiwa kutumika katika mradi huo wa nishati ya mimea ambao kwa sasa umeacha maumivu na masononeko kwa wananchi wa Kilwa.

Mwaka 2006, kampuni hiyo ilikodi zaidi ya hekta 40,000 za eneo la Pwani lenye misitu katika Wilaya ya kusini ya Kilwa kwa ajili mibono (Jatropha), ambayo mbegu zake hutumika kutengenezea mafuta ambayo yanaweza kuendesha mitambo mbalimbali yakiwemo magari.

Inaelezwa kuwa kampuni hiyo ilipanga kuajiri mamia ya wakulima wa vijiji hivyo. Dhamira kuu ilikuwa ni kuhakikisha wanapata mbegu za kutosha za mibono ambazo wangezipeleka Uholanzi ambako wangezisindika na kuzalisha umeme, mvuke na dizeli ya mimea.

Mibono ni moja ya mbegu zinazopendelewa zaidi kwa ajili ya mafuta. Aina hiyo ya nishati inadaiwa kutokuwa na madhara makubwa ya kuchafua hali ya hewa ikilinganishwa na mafuta mengine kutoka ardhini. Bahati mbaya hakuna umeme uliozalishwa hadi leo.

Kazi ya kuzalisha mibono ilianza kwenye shamba la mfano lenye ukubwa wa ekari 1000, ambalo ni mali ya kijiji. Vijana wake kwa waume waliajiriwa kwenye kampuni hiyo, mambo yalikuwa mazuri kwa wakati huo.

Kijiji cha Mavuji kilifurahia uwapo wa BioShape, waajiriwa wale bila hofu wakashiriki kuiteketeza misitu yao kwa imani kuwa mkombozi wa kweli amefika kijijini mwao.

Miti ya asili mikubwa kwa midogo iliyokuwa imemea kwenye msitu wenye ukubwa wa ekari 1000 ikateketezwa kwa kukatwa na kuchakatwa mbao zilizosafirishwa kwa umbali wa kilomita nyingi nje ya Lindi.

Kamwe haikuwa shida kwa wamiliki halali wa misitu hiyo ambao ni wanakijiji wa Mavuji, walicheka na kufurahia uvunaji huo wa misitu.

Ajabu ya Musa ni kwamba mara baada ya miti iliyokuwa kwenye shamba lililoitwa la mfano kumalizika, ndipo hapo kampuni ilipoanza kupepesuka, upandaji wa mibono haukuendelea na hata uzalishaji haukufanyika.

Haya yanathibitishwa na Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Mohamed Zuberi Ulambe ambaye ni miongoni mwa wanakijiji waliopata fursa ya kuajiriwa na BioShape.

Ulambe anakiri kushuhudia ukataji wa miti ukifanywa na kampuni hiyo ingawa hakushiriki kwenye zoezi hilo kwa sababu alikuwa ndiye msimamizi wa wakulima.

Anasema awali kampuni hiyo ilionekana kuwa mkombozi kwao, lakini kila siku zilivyokuwa zikienda walishuhudia mabadiliko kadhaa yaliyowafanya waamini kuwa dhamira ya kampuni hiyo ilikuwa ni kukata miti yao tu.

“Tuliamini hawa jamaa ni wenzetu na wangeweza kutusaidia kuondokana na tatizo la ajira, ni kweli vijana wengi tuliajiriwa na wengine walikuwa vibarua na walikuwa wakipata fedha zao vizuri tu, lakini ajabu ni kwamba asali hiyo tuliiramba kwa miezi mitano tu.

“Baada ya hapo tukaanza kurambishwa shubiri, wamekata miti yetu mingi, wanamiliki eneo letu kubwa la ardhi, kama hiyo haitoshi hadi leo bado tunadai mafao yetu, hatujui tumdai nani.

“Jambo gumu kabisa na ambalo pengine tunaiomba Serikali iliangalie na itusaidie ni namna ardhi yetu ilivyoendelea kuwa mikononi mwa watu hawa,” alisema Ulambe.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mavuji, Issa Abdalla Majid, akiwa na hofu kubwa aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa chini ya mwamvuli wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), wameachiwa masononeko, hawajui nini cha kufanya kwa sababu ardhi yao iko mikononi mwa wachache, hali inayowakosesha haki ya kuitumia.

“Yapo mengi tunayoyalalamikia kuhusu BioShape, lakini sina sababu ya kuyasema maana hayatakuwa na maana, kubwa ambalo naweza kulisema ni kuomba ardhi yetu irejeshwe mikononi mwetu ili tuangalie namna ya kuifanyia au Serikali impe mwekezaji mwingine atakayekuwa na tija kwetu,” alisema Majidi.

Pili Saidi Likomwa anaweka wazi kuwa kamwe hawamkatai mwekezaji huyo na mwekezaji mwingine yeyote atakayefika kwenye kijiji chao, badala yake kilio chao kikubwa ni kupata mwekezaji sahihi atakayekuwa tayari kuwapatia ajira na kusaidia kuwatatulia baadhi ya changamoto zinazowakabili.

“Ieleweke sisi wakazi wa Mavuji si kama hatuwataki wawekezaji, tunawataka sana, hata huyu BioShape alipokuja tulimpokea kwa mikono miwili kwa sababu tuliamini amekuja kusaidiana nasi kutatua changamoto zetu, bahati mbaya alishirikiana nasi kwa muda mfupi.

“Baada ya kukamilisha matakwa yake ambayo ni kuvuna miti yetu akakimbia, hadi leo hatujui yuko wapi na bado eneo letu amelishikilia.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kulirejesha eneo lote alilopewa mwekezaji ili sisi tujue ni nini tutakifanya kwa masilahi yetu,” alisema.

Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Kijiji cha Mavuji, Yusum Mohamed Ally maarufu kama Tangi, ambaye anatajwa kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la kuwakaribisha BioShape, anaonekana kwenda tofauti na wale wanaoilalamikia kampuni hiyo.

Tangi anasema wanaoilalamikia kampuni hiyo hawana wanachojua na kwamba haungi mkono matakwa ya wenzake wengi wanaotaka eneo hilo lirudi mikononi mwao.

Hoja ya Tangi ni kwamba taratibu zote za kukabidhi eneo hilo zilifuatwa na hakuna ujanjaujanja uliofanyika ingawa wenzake wengi wanalalamikia kuzungukwa na kutopewa taarifa sahihi.

“Wanaosema kuwa kuna ujanjaujanja umefanyika, hawa hawajui kitu, mimi nilishiriki kwenye zoezi la ujio wa BioShape, sisi tuliliuza eneo lote linalomilikiwa na BioShape na lilikuwa limepimwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Nawashangaa hawa wenzangu wanaosema kuna ujanja umefanyika, hakuna ujanja wowote, wawekezaji walitupatia fedha za fidia na hata mgao wa ununuzi wa eneo hilo ambao ni asilimia 40 ya kiasi cha Sh milioni 124 tuliupata.

“Hawa jamaa wametusaidia kwa kweli, wametujengea soko na hata fedha tulizopata tulizitumia kwa uwazi kwa kununua gari la kijiji na kufanyia mambo mengine,” anasema.

Kauli ya Tangi inapingwa vikali na Mwenyekiti wa sasa wa Serikali ya kijiji hicho, Seleman Mahamed Chaola.

Chaola anaungana na wananchi ambao wanataka eneo lao lirudi kwa sababu haliwanufaishi kwa chochote.

Mbali na hilo, lakini pia anaweka wazi kuwa mchakato mzima wa uwekezaji kwenye eneo hilo ulikuwa batili usiojali masilahi ya wengi.

Itaendelea…

mkombozi wa kweli amefika kijijini mwao. Miti ya asili mikubwa kwa midogo iliyokuwa imemea kwenye msitu wenye ukubwa wa ekari 1000 ikateketezwa kwa kukatwa na kuchakatwa mbao zilizosafirishwa kwa umbali wa kilomita nyingi nje ya Lindi.

Jatropha

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.