Tujifunze kutoka kwa tusiowapenda

Rai - - MAKALA - NA BALINAGWE MWAMBUNGU

NI kama nilipigwa na ‘shoti’ ya umeme. Miguu ikalegea magotini. Nilitamani kukaa chini, lakini kwa vile kulikuwa na watu wengi wanapita njia hiyo,

nikajikaza ili wasijefikiri kwamba nimeanguka.

Madhila haya yalinipata niliposoma ‘breaking news’ kwenye simu yangu ya kiganjani nikiwa njiani kuelekea Sinza— kwamba Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya.

Baadaye ikatolewa taarifa fupi kwamba Lissu alikuwa amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, na kwamba hali yake ilikuwa tete kutokana na majeraha ya risasi.

Wiki mbili kabla ya hapo, nilimwona Tundu Lissu amesimama na mwanasiasa mkongwe, na ambaye amewahi kushika nyadhifa za uwaziri katika awamu tatu, Paul Kimiti pale Kibo Complex, Tegeta. Nikachepuka kwenda kumsalimia Kimiti— ambaye ananiita ‘Bwana mdogo’ tangu nikiwa Daily/Sunday News. Nilishangaa kimoyomoyo Tundu Lissu aliponiamkia.

Nilishangaa kwa sababu watu wengine wakipata madaraka au umaarufu, hujawa na kujisikia, hawajisikii vizuri kunyenyekea kwa watu wasio na majina au vyeo, hata kama wamewazidi umri. Lakini mimi na Lissu hatukukutana barabarani na nadhani pia anayo kumbukumbu ya harakati tulizofanya pamoja wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Tuliongea mawili matatu pale Kibo Complex na watu walianza kukusanyika kwa mbali, ili kumwona Lissu. Kabla ya kuondoka nikamwambia: Keep the candle burning—asiuzime mshumaa aliouwasha. Naye akaniambia: Keep on writing to inform the people—endelea kuandika na kuhabarisha wananchi.

Nilibahatika kufanya kazi na Tundu Lissu kupitia Chama cha Wanasheria Wamazingira Tanzania (LEAT), wakati huo nikiwa kiongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET). Chama chetu kilikuwa kinapinga utekelezaji wa mradi wa kufuga samaki aina ya kamba katika Delta ya Rufiji.

Mradi huu uliokuwa umeidhinishwa na Serikali. Waliokuwa wanatuunga mkono wakatushauri tushirikiane na LEAT

ili wawe wanatuongoza katika mambo ya kisheria. Tulifanya nao kazi kwa ukaribu sana hadi mradi huo ulipokufa kifo cha mende.

Tulipewa majina mengi tu, kwamba sisi (JET), sio wazalendo kwa sababu mradi ule ulikuwa na faida kwa uchumi wa nchi, na kwamba ungetoa fursa kwa vijana wa Rufiji Delta. Mkubwa mmoja akasema JET ni chama cha ‘mjahidina wa mazingira’.

JET na LEAT pia tulijihusisha na suala la machimbo ya madini na kupinga ubabe uliokuwa unafanywa na Serikali kwa wachimbaji wadogo wadogo hasa kwenye mgodi wa Bulyanhulu ambako watu walifukiwa mashimoni wakiwa hai kumpisha mwekezaji.

Lissunawenzakewaliwezeshwa na kusoma zaidi masuala ya madini na naweza kusema Lissu ni ‘airthority’ katika kesi za madini hapa nyumbani na kimatifa. Wako wanasiasa ambao hawajui hata abc za madini, lakini wanampinga Lissu na kumbeza eti anatafuta umaarufu wa kisiasa, hana uzalendo, ni msaliti, na mhujumu uchumi. Mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka huu, yametokana na ukweli kwamba Lissu aliishauri Serikali ifanye mambo mawili kwanza Tanzania ijitoe kwenye mikataba ya kimataifa inayohusiana na madini. Pili ifanye mabadiliko katika Sheria ya Madini ya mwaka 2015.

Wako watu wanaofiki kwamba uzalendo ni kumwongopea mkuu wa nchi na kumjaza misifa kwamba ili kumwonesha kwamba wao ni wazalendo. Kuna hadithi moja ya mfalme aliyeagiza kwamba anataka kushonewa suti ya ajabu na kwamba atakaye ishona atapata zawadi nono.

Mjinga mmoja akajua kwamba duniani hakuna ambaye angeweza kushona suti ya ajabu, isiyoonekana, Akabuni namna ya kumhadaa mfalme na waliokuwa barazani kwake kwamba amekwisha mshonea mfalme suti ya ajabu ambayo ni watu wasio na dhambi tu, ndio watakaoiona suti ile. Wenye dhambi hawataweza kuiona. Siku ilipofika, mbele ya baraza la mfalme, mjinga yule akamtaka mfalme avue majoho yake ya kifalme, ili amvalishe suti ya ajabu.

Mfalme akavua nguo zote na ‘kuvikwa’ suti ya ajabu na wote waliomzunguka wakakiri kwa kwamba suti ya ajabu ya mfalme ilikuwa nzuri sana. Mfalme

akapandishwa juu ya farasi na kutembezwa kwenye barabara za mji wake, huku watu wakishangilia na kusifia uzuri wa suti ya mfalme. Akatokea mtoto mmoja mjinga, akapiga kelele Mfalme uko uchi.

Mfalme aliabika pamoja na wanafiki waliokuwa wanashangilia kwamba mfalme amevaa suti nzuri ya ajabu.

Iko siku wanaomdhihaki Tundu Lissu na kutaka kuchukua uhai wake, wataaibika. Tujifunze kuyatafakari maneno ya watu tusiowapenda na kuyapima. Kuyapuuza na kuwavika ‘lable’ za kishabiki na kwamba ni wasaliti, hawana uzalendo, ni wahujumu uchumi kuna siku watatafuna ndimi zao na kupata kigugumizi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.