Makundi ya Whatsapp yanaweza kukuza Kiswahili

Rai - - MAKALA - NA CAESAR JJINGO, AFRIKA KUSINI

KWENYE makundi ya vijana wa kawaida, kuna mchanganyiko wa Kiswahili na Kiingereza lakini zaidi maandishi mkato yamekuwa yakitamalaki kwa kiasi kikubwa kwenye lugha zote mbili. Makundi haya mengi yanachangia sana kuharibu lugha kwani hakuna usanifu katika maandishi yao iwe kwenye Kiswahili au Kiingereza.

Lakini kwa ujumla lugha ya Kiswahili ndiyo lugha inayotumiwa zaidi kwenye makundi mengi ya mtandao wa WhatsApp inchini Tanzania. Hali hii inatokana na Kiswahili kuwa lugha ya Taifa ambayo angalau inaeleweka na kila mmoja hivyo basi ni rahisi zaidi Kiswahili sanifu kukua miongoni kwa watumiaji wa mtandao huu.

Kwa hoja na mtazamo wa usahihishaji, ni dhahiri kwamba kipengele cha usahihishaji baina ya watumiaji wa lugha, ni vyema ikaeleweka kwamba bayana kwamba usahihishaji ni kati ya vipengele vya lugha ambavyo hujitokeza na kutumika hata nje ya darasa la lugha (yakiwemo makundi ya WhatsApp), kwa maana huweza kutumiwa na mtu yeyote yule mwenye ujuzi wa lugha husika.

Kwenye kitabu cha Cognition and second language instruction kilichohaririwa na Peter Robinson, mwaka 2001, kitabu kinaonesha kwamba kumsahihisha mzungumzaji ni njia ambayo msahihishaji anaitumia kurekebisha makosa ya kimazungumzo yanayojumuisha usahili wa maneno yaliyosemwa na mzungumzaji mwingine.

Katika mwendelezo huo pia kitabu cha The Oxford Handbook of Applied Linguistics, kilichohaririwa na Robert, B. Klapman mwaka 2010, kimeandika kwamba kuna njia nyingi za kumsahihisha mzungumzaji. Moja ya njia hizo ni ukanushaji wa wazi. Ukanushaji wa wazi ni pale mzungumzaji au mwandishi mmoja anapomfahamisha mwengine kwa mfano, kuwa neno alilolitamka au kuandika si sahihi na badala yake kumsahihisha kwa kumuonesha jinsi neno husika linavyopaswa kutamkwa au kuandikwa.

Kwa kizingatia maoni ya hapo juu, kwenye makala zijulikanazo kama Makala za semina ya Kimataifa ya waandishi wa Kiswahili volume II: Uandishi na uchapishaji, zilizohaririwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja ya makala hizo inasisitiza kwamba hata kama msahihishaji ni mzungumzaji wa lugha ya kwanza, suala la kumsahihisha mzungumzaji mwingine mara zote hukumbwa na changamoto kadhaa.

Zaidi, kuwa changamoto nyingi hujitokeza pale msahihishwaji anapoamini kuwa neno alilolitamka ni sahihi kuliko lile linalopendekezwa na msahihishaji. Kwa mujibu wa makala ya TUKI, chanzo kikuu cha wasahihishwaji kujiamini kuwa wako sahihi hata kama hawajui kama wamekosea, ni vitabu ambavyo wasahihishwaji hawa huvisoma. Aidha, makala hiyo inadai kuwa mara nyingi vitabu hivi huandikwa na waandishi wasio na utaalamu wa kutosha wa uandishi wa lugha.

Mathalani, katika makundi ya Whatsapp ni dhahiri kwamba chanzo kimojawapo cha kujiamini kwa wasahihishwaji hawa ni mazingira yaliyowazunguka ambayo huwafanya wasahihishwaji kusikiliza mazungumzo ya wazungumzaji wengine ambayo yanaweza kuwa na makosa kama vile makosa ya kitamshi au ya kiuandishi au kisarufi.

Ili kuepukana na changamoto hizi, makala ya TUKI inasisitiza kwamba msahihishaji ni lazima awe na njia mbadala ili kuweza kumsahihisha na kumrekebisha msahihishwaji wa namna hii. Kati ya njia zinazotajwa na TUKI ni ile ya kumrekebisha papo hapo kabla kosa tajwa halijakomaa kichwani mwa msahihishwaji au kuingia vichwani mwa wanaosikiliza au kumsoma.

Ili kufanikisha mkakati huu, makala ya TUKI inaeleza kwamba msahihishaji ni lazima atafute mbinu mbadala ambayo yaweza kuwa ni pamoja na kutumia mifano ya lugha mbalimbali yenye maana sawa au maana ya karibu na neno ambalo linasahihishwa. Kwa namna hii, kuna uwezekano wa msahihishwaji kukubali maoni ya msahihishaji kutokana na mifano mbadala ambayo imetumika kwenye kumsahihisha.

Kwa namna hii wanaWhatsapp wanaweza kikidumisha na kukiendeleza si tu Kiswahili bali pia Kiingereza na pia kwa kurekebishana wao kwa wao na pia kurekebisha makosa ya waandishi wenzao hasa makosa yanayojitokeza na kusikika kwenye mazungumzo na kusomeka kwenye maandishi ya kila siku.

Kwa upande mwingine, japokuwa kitabu kiitwacho Lessons from good language learners, kilichohaririwa na Carol Griffiths mwaka 2009, kinakubaliana na maoni ya vitabu vilivyojadiliwa hapo juu kuhusu kipengele cha usahihishaji, bado kitabu hiki cha Lessons from good language learnerskina shaka na namna ya kumsahihisha mkoseaji ukizingatia vigezo kama vile tofauti ya umri baina ya msahihishaji na msahishwaji, usahihishaji wa mmoja-mmoja au kwenye kundi la wasahihishwaji kwa ujumla au sehemu maalumu kama vile kwenye jukwaa zima la Whatsapp au kwenye ‘inbox’ ya wanaWhatsapp.

Kwa kuhitimisha, nayaacha wazi madukuduku hayo hapo juu kama yalivyojitokeza kwenye kitabu cha Lessons from good language learnersili yawape hamasa wasomaji na hususani wanaWhatapp ya kuyatafakari wakati wa kutekeleza kipengele cha usahihishaji baina ya wanaWhatsapp na watumiaji wengine wa Kiingereza na lugha nyinginezo katika mitandao ya jamii hususani mtandao wa Whatsapp ili juhudi za kuiendeleza lugha sanifu zifanikiwe.

Mwandishi wa Makala Haya ni Mwanafunzi wa Uzamivu wa Lugha, Chuo cha Stellenbosch, Afrika Kusini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.