Tanga iliyokufa kiuchumi itafufuka?

Rai - - MAKALA - NA SUSAN UHINGA ITAENDELEA

MWAKA 2013, msomi wa uchumi wa kiwango cha juu Duniani, Profesa Ibrahim Lipumba aliwahi kuushangaa mdororo wa uchumi wa mkoa wa Tanga.

Prof. Lipumba akiwa kwenye harakati zake za kisiasa, alipata kusema kuwa licha ya kuimarika kwa bei ya mkonge katika soko la dunia, bado hali ya kiuchumi mkoani humo ni mbaya.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hatua hiyo pia imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja mkoani Tanga.

Mshangao wa msomi huyo wa uchumi, unaweza kuwakumba wengi hasa wanaoijua vema historia ya Tanga kwa miaka dahari.Mkoa wa Tanga kabla ya kukumbwa na hali iliyonao sasa ilikuwa ikitambulika duniani kote kama miongoni mwa maeneo yanayo zalisha kwa wingi zao la mkonge ambalo takwimu za mwaka 2009 zinaonesha kuwa bei ya zao hilo katika soko la dunia imefikia dola za Marekani 2,632 kwa tani.

Mwaka 1964 Tanzania iliweza kuzalisha kiasi cha tani 234,000 za mkonge huku asilimia 60 ya kiasi hicho cha tani kilitoka Tanga.

Mbali ya Tanga kubarikiwa zao la mkonge, lakini pia imebarikiwa ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha aina yoyote ile, madini ya kila aina, bandari iliyozungukwa na bahari yenye kina kirefu, lakini vyote hivi havina tija kwa wananchi wa Tanga.

Badala yake mkoa umechoka na hata wananchi wake wengi wamechoka, kitu pekee kilichosalia na ambacho hakiimarishi uchumi wa mkoa huo badala yake inasaidia mtu mmoja mmoja ni ni bahari.

Angalau vijana wanapoteza muda wao kwenye kuvua viumbe vilivyomo baharini na kujipatia kipato cha kukidhi mahitajhi ya siku.Wiki iliyopita nilieleza namna Tanga ilivyokuwa iking’ara kwa viwanda nchini, nilijaribu kuvitaja viwanda kadhaa ambavyo vilikuwa vikifanya kazi.

Viwanda vilivyoondoa kabisa tatizo la ajira mkoani Tanga, maana mamia kama si maelfu ya vijana walikuwa wakifanya kazi kwenye viwanda tele vilivyokuwa vimetapakaa kwenye mitaa ya Chuda, Gofu Juu na hata Raskazoni.

Leo hii viwanda vingi kama si vyote vimekuwa magofu, vinavyofanya kazi ni vichache visivyo na uwezo wa kuajiri hata vijana 1000.

Yapo maswali kadhaa ya kujiuliza, kubwa likiwa ni je, ujio wa mradi mkubwa Afrika Mashariki, wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Kenya mpaka Chongoleani utafufua uchumi wa Tanga ambao ulishakufa kwa zaidi ya miongo miwili sasa?

Si rahisi kujibu swali hili bila takwimu na vielelezo stahiki, lakini kama ambavyo Prof. Lipumba ameonesha kushangaa, huenda hata wataalamu wengi wasiwe na majibu ya kutegua kiutendawili hiki, hata hivyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo alipata kusema kuwa Bandari ya Tanga inatarajia kuwa ya kimataifa kabla na baada ya kukamilika kwa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Dk. Pallangyo aliyasema hayo Agosti 03, mwaka huu jijijni Dar es Salaam kupitia mahojiano maalum kwenye kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kupitia kituo chake cha TBC1 lengo likiwa ni kuelezea uzinduzi wa Mradi wa Bomba hilo uliofanyika Agosti 5, mwaka huu.

Alisema kiasi cha Dola za Marekani milioni 200 kinatarajiwa kupatikana kama kodi wakati wa ujenzi na kuongeza kuwa mradi utatoa takribani ajira 10,000 kwa watanzania hususan katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu ya Bomba hilo.

“Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi aliye karibu na miundombinu ya Bomba hilo anakuwa sehemu ya uchumi wa bomba husika kupitia ajira na utoaji wa huduma mbalimbali.”

Alitoa rai kwa wananchi husuan waliopo katika maeneo yatakayopitiwa na bomba hilo kujinga na Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) itakayokuwa na jukumu la kuwaunganisha watoa huduma wote na kuwapa elimu ya namna bora ya kupata mikopo katika taasisi za serikali na kutoa huduma bora kwa kampuni zitakazojenga bomba hilo. Kuhusu usalama wa bomba hilo, Dk. Pallangyo alisema Serikali imepanga mkakati maalum wa utoaji elimu kwa wananchi waishio karibu na miundombinu ya Bomba ili wawe walinzi na kufunga mfumo maalum wa usalama kwenye Bomba.

Maelezo ya Dk. Pallangyo yanashiria tija kubwa kwa mkoa wa Tanga kama walivyosema baadhi ya viongozi waliofanya mahojiano maalum na safu hii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.