‘Vijana msijione wanyonge huu ni wasaa wa kushika hatamu’

Rai - - MAKALA - NA RAYMOND MINJA, SINGIDA

UNAPOWAZUNGUMZIA makatibu wenye umri mdogo kuteuliwa katika awamu ya tano ya Rais John Magufuli, huwezi kumwacha Jimsoni ambaye ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida.

Mhagama ndiye kijana mwenye umri mdogo kuliko makatibu wote Tanzania Bara. Kabla ya kuteuliwa alikuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi na katika uchaguzi uliopita alifanikiwa kupigania majimbo matatu ya wilaya hiyo na kuendelea kubaki chini ya himaya ya CCM.

Licha ya kuwa na umri mdogo wa miaka 29, Katibu huyo amekuwa ni machachari na mchapakazi anayetegemewa na wanachama wa chama hicho mkoani Singida na pindi apazapo sauti yake, wakubwa kwa wagogo hutulia kusikiliza busara na hekima za Katibu huyo.

Hivi karibuni nilipata kutembelea mkoa huo wa Singida na kushiriki moja ya mikutano yake ya hadhara aliyokuwa akifanya ya kuwafunda wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama hicho, kwa kuwataka kuachana na dhana potofu ya kutaka uongozi kwa kutumia rushwa na endapo kuna atakayebainika basi hatakuwa salama.

Mhagama anasema katika kipindi hiki hakuna mgombea yeyote wa uongozi wa chama hicho atakayepitishwa kwa kutumia njia ya rushwa na atakayebainika kutoa rushwa basi jina lake litakatwa.

Anasema hakuna haja kwa mwanachama yeyote kujiona mnyonge kwa kuhofia kuwa kuna baadhi ya wanaotaka uongozi kwa njia ya rushwa, kwani chama kimejipanga kusimamia misingi ya katiba ya chama hicho na anayetaka kugombea uongozi katika chama hicho lazima aifuate.

“Tutasimamia misingi ya uongozi katika chama chetu, hakuna mwanachama katika mkoa wetu wa Singida atakayepata uongozi kwa kutumia rushwa na wote watakaopatikana lazima waheshimu maadili ya chama chetu na tutalisimamia na wanachama msijione wanyonge jitokezeni kuchukua fomu,” anasema.

Anasema lengo la chama hicho ni kupata viongozi waaminifu, waadilifu na wanaochukia ufisadi kwa vitendo ambao wana uwezo wa kulitetea taifa na kuwatumikia wananchi kwa misingi ya CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi.

“Wote tunatakiwa kucheza wimbo mmoja ambao ni kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Magufuli ya kuchukia rushwa na ufisadi.”

Anasema matokea chanya ya Rais Magufuli yameshaanza kuonekana, kwani kila Mtanzania anaonja matunda ya nchi baadhi ya kudhibiti rushwa na ufisadi.

“Rais Magufuli amerudisha imani kwa Watanzania wa chini, amewezesha kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Ni nani asiyeona utendaji kazi wake? Amefufua viwanda, anajenga barabara, kila siku tunasikia anazindua miradi na kubwa kuliko ni hili la makinikia yaliyokuwa yakisafirishwa nje kwa kutuibia, ambayo sasa amepiga ‘stop’ na tunakuja kulipwa ndio maana nasema tunapaswa kuunga mkono kwa hali na mali.

“Hata wale waliokuwa wakiilalamikia Serikali kila kukicha, sasa wameanza kukaa kwenye mstari na kumuunga mkono Rais Mgufuli,” anasema.

Anasema kila mtumishi na watendaji wanapaswa kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kuwatumikia wanachi kwa weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kujiona ni mabwana wakubwa.

Mgahama pia anawaonya viongozi wote ambao wamefanya ufisadi katika mbolea ya ruzuku kwa kuwapatia watu ambao hawahusiki katika mgao wa mbolea hiyo, wakiwamo watoto wachanga na marehemu.

Kutokana na hali hiyo, anasema wote waliochakachua mbolea ya ruzuku hawakuwatendea haki wananchi wanyonge hivyo wajiandae kwa ukaguzi na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kufukuzwa kazi, kwa kuwa Serikali ya sasa haitaki kumuona mtu wa hali ya chini anaonewa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Jimsoni Mhagama, akiwa katika moja ya mikutano yake mkoani humo hivi karibuni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.