Uingereza nayo yakiri kufanya makosa Libya

Rai - - MAKALA AFRIKA - TRIPOLI, LIBYA

Waziri wa Nje wa Uingereza Boris Johnson ameungana na Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kukiri kufanya makosa ya kumng’oa aliyekuwa Rais wa Libya Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Johnson amesema kuwa uamuzi wao ule umezalisha janga kubwa kwa wananchi wa Libya.

Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la BBC mapema wiki hii Jiohnson alisema Uingereza ilikuwa na matumaini yaliyopitiliza kuhusu hali ya baadaye ya Libya na kwamba uchaguzi wa 2014 ulizidisha hali kuwa mbaya zaidi.

Waziri huyo wa nje aliyasema hayo baada ya ziara yake ya siku mbili nchini Libya, ambako aliyataka makundi yanaopingana kufikia maafikiano na kuleta umoja nchini humo.

Waziri Johnson aliahidi nchi yake kutoa msaada wa Pauni 9 milioni kusaidia kuyashughulikia masuala ya biashara ya binadamu na ugaidi.

Katika mkutano wake wa kihistoria, Johnson alikuwa mwanasiasa wa kwanza mwandamizi kutoka nchi za magharibi kumtembelea kamanda wa majeshi ya Libya Field Marshal Khalifa Haftar katika makazi yake ya Benghazi. Haftar ni hasimu wa serikali ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj anayetambuliwa na Umoja wa mataifa.

Alisema Field Marshal Khalifa Haftar ambaye anayadhibiti maeneo ya mashariki ya Libya aliahidi kuuondoa utawala wa kijeshi iwapo atachaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo.

Johnson alisema katika jitihada zake za kutafuta muafaka nchini Libya aliwataka wanasiasa waondokane na tamaa za masilahi binafsi, na kutafuta uelewano kwa manufaa ya nchi na kuwa nyuma ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusimika amani.

Aidha aliwataka wanasiasa wa Libya kujifunza kutokana na makosa ya Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May – kutofanya uchaguzi kabla hawajawa tayari.

Balozi wa zamani wa uingereza nchini Libya

Oliver Miles, ambaye pia mi Naibu Mwenyekiti wa Baraza la biashara baina ya Libya na Uingereza alisema ziara ya Boris Johnson ilikuwa ina manufaa kwani ilikuwa ni ufuatiliaji mzuri wa mkutano wa Rais wa Ufaransa ambao Field Marshal Haftar na hasimu wake Fayez al-Sarraj walikubaliana kusitisha mapigano.

Hata hivyo Miles aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba ilikuwa inapotosha kudhani kwamba Libya ilikuwa imegawanyika katika pande mbili, na kuongeza kwamba imegawanyika zaidi ya hapo.

Alisema ingawa ni miaka sita sasa tangu kuondolewa kwa Kanali Gaddafi kuna kuporoka kukubwa kwa mamlaka ya serikali nchini Libya – na imekuwa si sahihi tena kusema nchi hiyo iko katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, bali ni nchi ambayo haina mamlaka na utawala wa sheria kabisa.

Alisema hakuna mamlaka ya serikali kwamba ni nani anaendesha nchi na kuna maeneo mengi na makubwa ambako hakuna serikali kabisa.

Muda mfupi baada ya kuondolewa kwa Kanali Gaddafi mwaka 2011 maelfu ya Walibya walijitokeza kuwashangilia Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza David Cameron na rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy katika mji wa Benghazi kwamba wawili hao ndiyo walikuwa mashujaa na waliokuwa wakiwaunga mkono.

Wakati haya yakijiri Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini amesema ana uhakika kwamba hali ya amani na utulivu itapatikana nchini Libya.

Zuma aliyasema hayo akiwa Congo-Brazzaville Jumamosi iliyopita baada ya kikao cha Kamati ya Ngazi ya Juu cha Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Libya.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wahusika wakuu wa mzozo huo wa Libya pamoja na marais watano wan chi za Afrika, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (Arab League).

Waziri wa Nje wa Uingereza Boris Johnson ma Kamanda wa waasi nchini Libya Field Marshal Khalifa Haftar.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.