Wachezaji wa kigeni waongezwe si kupunguzwa

Rai - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

KUMEKUWEPO na dhana kwamba kuwepo na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni imekuwa ikiathiri ubora wa timu ya soka ya Taifa nchini.

Dhana hiyo imekuwa ikisambaa miongoni mwa wadau wa soka nchini ambapo wako wanaoamini wapunguzwe kwa madai kuwa wamekuwa wakiwanyima nafasi wachezaji wazawa na baadaye kuathiri kiwango cha timu ya taifa.

Vilevile wapo wanaoamini uwepo wa wachezaji wa kigeni unachochea changamoto ya kujituma zaidi kwa wazawa hivyo kujituma na hatimaye kusaidia kukuza viwango vyao.

Hoja kama hiyo pia imetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto wakati akichangia bungeni na kutoa rai akitaka idadi ya wachezaji wa kigeni ipunguzwe kutokana na sababu kama hizo.

Katika maoni yake, mheshimiwa Mwamoto alidai maendeleo hafifu yanayotokana na kiwango duni kinachooneshwa na wachezaji wa timu ya taifa kinatokana na wazawa kutopata nafasi ya kutosha kucheza katika timu zao katika Ligi.

Hivyo alipendekeza idadi ya wachezaji saba wa kigeni ilioruhusiwa kikanuni ipunguzwe hadi watatu ili tu wazawa wapate fursa zaidi ya wageni kucheza ambapo hoja hiyo imepokewa kwa hisia tofauti.

Mbunge huyo anaamini ujenzi imara wa timu ya taifa utatokana na uwepo wa Ligi Kuu bora ambayo ndiyo itakayozaa kiwango kizuri cha wachezaji watakaokwenda kuunda kikosi cha timu ya taifa.

Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya soka wanaliangalia suala hilo kama ni hoja dhaifu na isiyokuwa na mashiko kutokana na ukweli kwamba ujenzi wa timu ya taifa hautokani na kuwepo kwa Ligi Kuu bora kama kigezo muhimu ingawa wanakubali Ligi bora inaweza kuzalisha timu imara ya taifa.

Nchi kama England inaweza kuwa mfanbo mzuri kuthibitisha hilo kutokana na ukweli kwamba Ligi yake ina wachezaji wengi wanaotoka nje lakini bado timu yake ya taifa imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

England ni ruksa klabu kusajili wachezaji wengi wa kigeni na hata kuwatumia katika mechi kwa idadi watakavyo kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Chelsea aliyopambana na Totenham huku ikiwa na kikosi kizima cha wachezaji 11 wanaotoka nje ya England na kushinda kwa mabao 2-1.

Ukiangalia Ligi ya Hispania bado unaweza kuona ikishamiri wachezaji wengi kutoka nje ya nchi hiyo lakini bado imeweza kuwa na timu bora ya taifa.

Ukiangalia nchi kama Uganda ambayo ni jirani na Tanzania unaweza kubaini faida kubwa wanayoipata ndani ya timu yao ya taifa kwa wachezaji wao wengi kutoka na kujifunza vitu tofauti nje na warejesha faida wanaporudi nyumbani.

Kwa mfano kikosi cha Uganda kilichocheza hivi karibuni mechi ya kwuania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Misri ilichezesha wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi yao huku watatu pekee wakwia ni wanaocheza ligi ya ndani.

Huo unaweza kuwa mfano mzuri kutokana na ukweli kuwa kadri wachezaji wao wanavyotoka na kwenda kucheza nje ndivyo wanavyokuza kiwango cha timu yao ya taifa kwa kufanya vizuri.

Wachambuzi hao wanaiona hoja hiyo kama ni sawa na kuwanyima zaidi wachezaji wazawa fursa ya kujifunza kutoka kwa wenbzao wanaotoka nje. Katika hilo inaaminika kuchanganyika kwa wachezaji kutoka nchi tofauti kunawafanya wote kwa pamoja kila mmoja kujifunza kitu kutoka kwa mwenzake.

Hoja iwe ni jinsi gani kama taifa inaweza kuzalisha wachezaji wanaoweza kutoka kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na si kuwazuia wageni.

Kupinga idadi ya wachezaji saba na kutaka wapunguzwe ni sawa na kutaka kuwa na Ligi yenye hadhi ya mtaani ambayo haitakuwa na changamoto hasa miongoni mwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe.

Wachezaji kushindana kupata namba ndani ya timu kunawafanya wazawa kupambana vilivyo kujihakikishia nafasi ya kucheza ndani ya timu, hiyo ni ishara tosha ya kuwafanya wapambane na kukuza viwango vyao kwa kushindana na wageni.

Hiyo inatokana na ukweli kuwa kila nchi ina utamaduni zake tofauti sambamba na maendeleo tofauti ya kisoka waliyonayo hivyo kuwakutanisha wachezaji wa sehemu mbalimbali kunachagiza fursa ya kujifunza na kupata uzoefu.

Bila ubishi Ligi ya Tanzania na soka lake kiujumla ni la ridhaa hasa kutokana na kuendeshwa kwa kutegemea mapato ya viingilio vya mlangoni. Katika VPL angalau Azam pekee inaweza kuwa ndiyo timu inayoendeshwa katika mfumo wa soka la kulipwa.

Katika hilo wadau wengi wanaona kuna haja ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni ili kuwafanya wazawa nao sio tu kutafuta fursa ya kujifunza lakini pia hamasa ya kutoka kwenda kucheza soka nje.

Katika hili hakuna hofu wala uoga bali ni kuwaandaa wachezaji wa kitanzania nao kuwa na uthubutu wa kutoka nje kwa wingi ili kwenda kuchota uzoefu huko na kuurudisha nyumbani kufaidisha timu ya taifa.

Kikosi cha Taifa Stars

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.