Algeria

ilivyojimaliza safari ya Kombe la Dunia 2018

Rai - - MICHEZO KIMATAIFA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KICHAPO cha bao 1-0 ilichokipata wiki iliyopita kutoka kwa Zambia, kilihistimisha safari ya timu ya Taifa ya Algeria kwenye mbio za kuifukuzia tiketi ya kwenda Urusi kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani.

Kutofuzu kwa Algeria kuliwashangaza mashabiki wengi wa soka barani Afrika kwani katika fainali za mwaka 2014 nchini Brazil, timu hiyo ilifika hatua ya mtoano ya 16 bora, tena iliondoshwa na Ujerumani katika dakika za nyongeza.

Kabla ya Zambia kuuvunja mwiko huo, Algeria haikuwa imefungwa katika uwanja wao wa nyumbani tangu walipofungwa kwa mabao 2-0 na Guinea na kushindwa kufuzu fainali za Afcon za mwaka uliofuata.

Ukiacha fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010, ambapo haikufanya vizuri, Algeria ilianza kutajwa kuwa moja kati ya mataifa yanye kiwango kizuri cha soka baada ya michuano ya mwaka 2014.

Matatizo ya sasa ya Algeria yalianza mara tu baada ya kuondoka kwa kocha wake Vahid Halilhodzic raia wa Bosnia, na nafasi yake kuchukuliwa na Christian Gourcuff.

Ingawa kocha Gourcuff alikuwa kipenzi cha wachezaji, mfumo wake wa 4-4-2 ulionekana kuirudisha nyuma timu hiyo na kuwafanya mastaa kama Riyad Mahrez na Yacine Brahimi kushindwa kung’ara.

Mwaka 2015, miezi tisa baada ya kuipa Algeria taji la Afcon, Gourcuff alitangaza kuachia ngazi akitajwa kutoungwa mkono na mashabiki, ambao hawakuwa wakivutiwa na uteuzi wa kikosi chake.

Nafasi yake ilichukuliwa na Milovan Rajevac aliyetangazwa mwaka jana lakini wachezaji walimkataa licha ya kuwa tayari alishapewa mkataba wa miaka miwili. Ikumbukwe kuwa Rajevac aliyeonekana hafai Algeria ndiye aliyeikaribia kuipeleka Ghana nusu fainali ya Kombe la Dunia kama si hatua ya penalti kuwaangusha.

Algeria haikuweza kurejea makali yake ya mwaka 2014 hata alipotua kocha George Leekens, ambaye alikishuhudia kikosi chake kikivurunda katika fainali za Afcon za mwaka huu.

Kitendo cha kuondoshwa kwenye fainali za Afcon ikiwa haijashinda hata mchezo mmoja wa hatua ya makundi kiliibua maswali mengi kwa mashabiki ambao walitaka mabadiliko makubwa kwenye Shirikisho la Soka nchini humo (FAF).

Vuguvugu hilo lilisababisha Rais wa FAF, Mohamed Raouraoua, kujiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na Kheiredine Zetchi.

Aprili mwaka huu, uongozi mpya ulimteua aliyekuwa kocha wa klabu ya Granada ya La Liga, Lucas Alcaraz kuchukua nafasi ya kuliongoza benchi la ufundi la timu hiyo.

Bahati mbaya kwa Mhispania huyo ni kukuta timu ambayo ni kama imesuswa na mashabiki. Baada ya kupoteza michezo yote miwili dhidi ya Zambia, kocha Alcaraz alikosolewa vikali na mashabiki.

“Sikuajiriwa kuipeleka timu hii kwenye michuano ya Kombe la Dunia,” alisema mkufunzi huyo. “Najuwa naweza kutimiza majukumu niliyopewa, ambayo ni kuisaidia timu kufuzu Afcon 2019.”

Rais Zetchi amesema hawatakuwa tayari kutimua makocha kila timu inapopoteza matokeo.

Patson Daka, mfungaji wa bao pekee la Zambia dhidi ya Algeria kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.