Safari ya Omog imewadia?

Rai - - MAKALA JASMEPITIEMBA - NA AYOUB HINJO

SIMBA ni moja ya timu ilizofanya usajili mzuri wa wachezaji unaodhaniwa kuwa bora pengine kuliko timu nyingine yoyote katika msimu huu wa 2017/2018.

Klabu hiyo ambayo kwa takribani misimu mitatu sasa ilisajili wachezaji kwa gharama kubwa inayodaiwa kufikia shilingi Bilioni 1.3 ikihusisha mastaa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Ni usajili ghali zaidi kwa timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ukihusisha wachezaji takribani 11 ambapo ni sawa na kusema wamesajili kikosi kizima. Ni wazi kwamba usajili waliofanya sio wa kawaida kufanywa na klabu hiyo kwa kipindi kirefu hivyo kutumia kiasi hicho cha fedha sambamba na kuchukua wachezaji kadhaa wenye uwezo na majina ni wazi unaiweka katika kumbukumbu nzuri.

Timu ipi isingependa kuwa na wachezaji kama Aishi Manula, Erasto Nyoni, Haruna Niyonzima au Emmanuel Okwi? Sidhani kama ipo.

Hata hivyo pamoja na kufanya usajili huo wa gharama kubwa bado timu hiyo inaonekana kukosa nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo lina wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu mkubwa kama vile Okwi, John Bocco, Laudit Mavugo, Nicholas Gyan na Juma Luizio.

Licha ya safu hiyo ya ushambuliaji kuundwa na kikosi kazi hicho lakini bado timu hiyo imeshindwa kutibu tatizo la ufungaji ambalo kwa sasa unaweza kusema ni sugu licha ya hivi karibuni kufanikiwa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi yao ya kwanza ya Ligi.

Simba imekuwa ikisumbuliwa sana na tatizo la kufunga mabao katika mechi zake nyingi kwa misimu kadhaa ukiwemo uliopita ambapo imekuwa ikishinda kwa taabu ama bao moja au mbili tu huku idadi kubwa ikiwa ni ile katika mchezo mmoja iliposhinda kwa mabao 4-0.

Msimu uliopita timu hiyo ilikosa ubingwa kutokana na tofauti ya mabao tu kwani walizidiwa magoli 10 na wapinzani wao wa jadi, Yanga iliyoutwaa ubingwa.

Msimu uliopita hawakufanikiwa kufunga magoli ya kutosha. Idadi ya magoli mengi katika mchezo mmoja walifunga magoli manne tu. Michezo mingine walikuwa wanashinda kwa shida, tena dakika za mwishoni kabisa.

Usajili wa Bocco, Okwi na Gyan ulitakiwa uwavushe sehemu

waliyoshindwa kuifikia msimu uliopita. Lakini toka wachezaji hao wasajiliwe huku ikiwa imecheza mechi kubwa takribani saba, bado hawajafanikiwa kuonyesha makali ya kuogopwa na wapinzani wao.

Ukiacha mechi dhidi ya Ruvu Shooting kwa kufunga mabao 7-0 huku Okwi akiziona nyavu mara nne peke yake, bado Simba ilishindwa kupata mabao katika mchezo wa Ngao ya jamii dhidi ya Yanga na kutoka sare ya bila kufungana sambamba na ile ya hivi karibuni dhidi ya Azam.

Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Simba ilishinda kwa idadi hiyo ya mabao kutokana na ukweli kuwa waoinzani wao hawakuwa bora hasa kutpokana na kutokuwepo kwa wachezaji wao kadhaa wa kikosi cha kwanza.

Walionekana kucheza vile wanavyotakiwa kucheza, lakini ukiangalia kwa jicho la tatu utagundua Ruvu Shooting walikuwa dhaifu sana sababu wachezaji wao wengi walikuwa kwenye mashindano ya majeshi kwa nchi za Afrika Mashariki.

Bocco alikuwa kinara wa mabao wakati akiwa na azam hali kadhalika kwa Gyan ambaye ni mmoja katika orodha ya wafungaji wazuri katika ligi ya Ghana lakini bado mpaka sasa wameshindwa kuonesha cheche kiasi cha kuzua maswali je tatizo liko kwao au kwa benchi la ufundi?

Ukichunguza kikosi cha timu hiyo utagundua kuwa katika safu ya ulinzi na kiungo iko vizuri sana. Lakini wadadisi wa masuala ya soka wana amini kwamba huenda ni kutokana na kocha mkuu wa timu hiyo Joseph Omog kuwa muumini wa mfumo wa kuzuia zaidi.

Rahisi kugundua hilo kwani ukichunguza hata katika msimu uliopita utagundua wazi timu hiyo iliruhusu kufungwa mabao machache sana katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Mpaka sasa inaaminika timu hiyo ndiyo bora zaidi katika eneo la kiungo kwa sasa ukilinganisha na timu zingine.

Matatizo yapo katika eneo la mwisho la timu hiyo. Kwa maana hiyo huwezi kusema timu hiyo imekamilika. Hawajakamilika kwa sasa, tatizo bado lipo katika umaliziaji kitengo ambacho ndiucho muhimu katika kutafuta matokeo.

Naamini katika mfumo wa kucheza washambuliaji wawili unaweza kuwa msaada mkubwa kwa Simba. Muda mwingi wamekuwa na utamaduni wa kuchezesha mshambuliaji mmoja huku wakiwa na viungo wengi nyuma yake.

Mara nyingi mshambuliaji anayesimama kuongoza safu ya ushambuliaji huwa anashindwa kubeba majukumu, pia ina kuwa rahisi kwa walinzi kuharibu mipango.

Endapo Bocco na Mavugo wakisimama pamoja inaweza kuwa dawa kwao. Mavugo si mshambuliaji anayependa kusimama eneo la mwisho la umaliziaji, ni rahisi kwake kuwafanya mabeki wafunguke pia ni mzuri katika kutengeneza nafasi kwa wenzake lakini si kumalizia.

Ni ngumu sana kwa washambuliji wa Simba kufunga sababu, mfumo wa viungo wao unakuwa mgumu. Kila kiungo anataka kuugusa mpira, ni kitu ambacho kinapunguza mashambulizi ya timu hiyo na kuonekana muda mwingi wanacheza mpira katika eneo la kati.

Dhidi ya Azam walishindwa kuitambuka safu ya kiungo cha Azam sababu mifumo yao ilishabihiana, kocha alikosa mbinu mbadala ya kuivuka sehemu hiyo.

Muda mwingi walionekana kucheza chini zaidi, kuliko eneo la ushambuliaji. Omog bado ana kazi ya kukifanya kikosi hiko kiwe na makali eneo la ushambuliaji.

Timu nyingi zitashindwa kutawala mpira dhidi ya Simba, wataamua kukaa nyuma ya mpira ili kutumia mipira mirefu. Endapo Simba watashindwa kutegua mbinu hizo itakuwa shida kubwa kwao.

Kubadili mfumo ni suala lingine linalopaswa kutazamwa na makocha, ni hakika kabisa kuamini kwamba hakuna kocha asiyependa matokeo kila mtu mwenye dhamana ya kufundisha timu ni wazi atapenda kuona timu yake inafanya vizuri, lakini je ni vipi kwa kocha Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja?

Taarifa za Simba kutaka kubadili benchi la ufundi huenda zikawa tamu kwa mashabiki wake wanaoamini wana kikosi bora hivyo kuhitaji matokeo katika kila mchezo lakini vilevile zikawa shubiri kwa wahusika kutokana kufungishiwa virago.

Wachambuzi wa soka nchini wana amini kabisa kwamba upana wa kikosi cha Simba ndio hasa tatizo kwa benchi la ufundi ambao wanashindwa kuwatumia kikamilifu wachezaji ilionao kulingana na mifumo sahihi wanapokutana na wapinzani wao.

Ni presha kwa Omog na Mayanja ambao kwasasa watatakiwa kushinda michezo minne inayofuata ya ligi kwa idadi nzuri ya mabao ili kulinda kibarua chao ndani ya klabu hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.