Urais wa Trump kupingwa Mahakamani

Rai - - MBELE - NA HILAL K SUED

Kuna wito sasa hivi unatolewa kuhusu Katiba ya Marekani kufanyiwa marekebisho ili kuruhusu ushindi wa urais upingwe mahakamani.

Wito huu unajiri kutokana na uchaguzi wa urais wa Novemba mwaka jana ambao Donald Trump wa chama cha Republican aliibuka mshindi dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic.

Wito huu wa marekebisho ya Katiba unatokana na madai yaliyokuwapo ya uendeshaji wa uchaguzi huo kuingiliwa na mamlaka ya nchi za nje – ikitajwa nchi ya Urusi kwamba ilifanya hujuma katika mfumo wa tovuti kuhakikisha Trump anashinda.

Madai ya kuhusika kwa Urusi yamekuwa yakiutikisa utawala wa Trump tangu atangazwe mshindi na baadaye kuapishwa huku yakiwahusisha maafisa wake wakuu, hadi kufikia kuanzishwa uchunguzi rasmi na Idara ya Sheria (Justice Department) kuhusu madai hayo. Hata hivyo, Trump mwenyewe amekuwa akiyakana madai hayo.

Maafisa kadha waandamizi wa utawala wa Trump ama walijuzulu au kufukuzwa kazi kutokana na kashfa hiyo, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI, James Comey na Dana Boente, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Sasa hivi Clinton amekuwa akifikiria namna ya “kuyahoji” matokeo ya uchaguzi huo. Katika ziara yake sehemu mbalimbali nchini humo akikitangaza kitabu chake kipya kiitwacho ‘What Happened’ (Kitu Gani Kilitokea) alisema katika mahojiano na Chaneli ya NPR Jumatatu iliyopita kwamba kamwe hataacha kuyahoji matokeo ya uchaguzi ule pamoja na kwamba sasa ni miezi 10 imepita tangu Trump aliposhinda kwa mshangao mkubwa.

Katika mahojiano hayo aliulizwa: “Nataka kurudia swali langu, je, kweli mtu anaweza kuacha kabisa kuhoji uhalali wa uchaguzi ule iwapo tunaambiwa kwamba uingiliaji wa Warusi ulikuwa mkubwa kuliko tulivyofikiri?”

Clinton alijibu hapana, “haitawezekana kuacha kuhoji”. Alisema hata kama hajayapinga rasmi matokeo, haamini kwamba upo mfumo rasmi unaoruhusu kufanya hivyo.

Alisema hafikirii iwapo kuna njia ya kisheria au ya Kikatiba ya kufuata. Hata hivyo, alisema kuna wanazuoni wengi ambao wamesema kikatiba inawezekana, lakini aliwaambia msimamo wao huo hauna nguvu sana, na kuongeza kwamba kunatakiwa kuwepo mfumo wa Kikatiba wa kufanya hivyo.

Julia Azari, mtaalamu wa masuala ya Katiba ya Marekani anasema Katiba iliyopo inaelezea tu namna ya kuendesha uchaguzi na si maswali yanayohoji kuhusu uhalali wake.

Azari ambaye ni profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Marquette aliongeza kwa kusema kwamba Katiba ya Marekani inaipa Wakala wa Uchaguzi “mamlaka makubwa kuamua malalamiko kwa namna itakayoona inafaa.”

Alisema: “Katiba inatamka kwamba uchaguzi utakuwa halali iwapo Wakala wa Uchaguzi itasema hivyo, basi.”

Alisema wasomi wa masuala ya sheria wamekuwa wakihoji iwapo marudio ya uchaguzi mzima ni njia moja inayotakiwa, lakini pia wanasema njia pekee iliyopo ni kumshitaki rais aliyeingia madarakani kwa njia zisizo halali.

Lakini hata njia hiyo haiwezi ikawa suluhisho sahihi katika kesi kama hii ya uchaguzi wa mwaka jana kwa sababu inatakiwa ijikite katika jinai ya mtu mmoja binafsi.

“Na kama ni hivyo, hata kama kulikuwapo kwa njama baina ya Trump na watu wengine katika uvurugaji wa uchaguzi, mchakato wa mashtaka hautalitatua suala hilo iwapo uchaguzi wake ulikuwa halali,” alisema Azari.

Hivyo alisema marekebisho ya Katiba katika suala hili tata yanatakiwa sana sasa hivi kuliko wakati wowote mwingine – kwamba katiba iruhusu anayeshindwa kwenda mahakamani kuyapinga matokeo.

Alisema kwa hali ilivyo sasa hivi hata kukiwapo ushahidi unaotosheleza kwamba mamlaka ya nchi za nje iliingilia katika kuyumbisha matkeo ya uchaguzi, katiba haina jibu kifanyike nini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.