ATAWASHIKA MKONO VIJANA HAWA?

Rai - - MBELE - NA MARKUS MPANGALA 0764 936655

WIKI kadhaa zilizopita nilikuwa nazungumza na kijana, Ndahani Mwenda, ambaye aliomba kunitembelea ofisini ili kupata ushauri wa masuala mbalimbali ya maisha na mengineyo. Hili ni jambo la kawaida kwa baadhi yetu kuzungumza na vijana, kama tusemavyo ndiyo ‘tunapambana na hali zetu’.

Mazungumzo yetu hayakuwa na ajenda kubwa isipokuwa ushauri. Hata hivyo, katika mazungumzo hayo nilibaini jambo kutokana na udadisi niliofanya.

Jambo hilo ni kwamba, kijana huyo na wenzake wamebeba mzigo mkubwa mno wa majukumu huku wakihitaji sapoti ya wananchi wenzao hapa nchini. Hapo ndipo fikra zangu zilipoanza kuchakata zaidi suala lake.

Mazungumzo ya kirafiki yalibadilika upesi. Kila kitu kilionekana dhahiri mbele yetu tusingeweza kuzibananga akili zetu tena. Lilikuwa jukumu kubwa na la wazi ambao lilionekana mbele yetu. Swali moja nililojiuliza nawezaje kuwasaidia vijana hawa wa Kitanzania wawe chachu kwa wengine?

Wakati naendelea kutafuta suluhisho juu ya suala nililokuwa nalo mezani, rafiki yangu Malisa Godlisten, akatangulia kutumia ukurasa wake katika mtandao kutoa taarifa juu ya vijana ambao kwa namna moja au nyingine ni wahanga wa bomoa bomoa iliyofanywa hivi karibuni na Serikali ya Awamu ya Tano ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.

Wiki mbili baada ya maongezi yetu nilimwomba atekeleze mambo kadhaa ili tuweze kuzungumza na Watanzania wenzetu katika safu hii juu ya suala lililokuwa mbele yetu.

Ndahani Mwenda ni zao la watoto yatima. Hakulelewa na wazazi wake. Amekulia kwenye malezi ya watu baki na jamaa zake wengine. Na zaidi amekulia kwenye mazingira ya kawaida ya kijana wa Tanzania, kwa msaada wa ndugu na jamaa.

Kutokana na hilo, ameamua kujikita kwenye kusaidia vijana wengine wenye shida kama alizowahi kuzipata yeye utotoni angalau wawe na unafuu.

Aidha, Ndahani ni mwanafunzi wa Chuo Usimamizi wa Fedha, akiwa na ndoto mbalimbali maishani mwake lakini anakabiliwa na jukumu kubwa la kuhakikisha mapenzi yake ya kulea watoto yatima yanasonga mbele licha ya jengo lao walilolitegemea kutakiwa kubomolewa kupisha upanuzi.

Kijana huyo aliniambia kuwa wanaendelea na mazungumzo na mamlaka zinazohusika ili waweze kuongezewa muda kutumia jengo lao lililopo Kimara Suka ambalo linatakiwa kubomolewa. Wakati mazungumzo yanaendelea, juhudi za kuhakikisha wanajenga jengo jingine zinaendelea.

Wamefanikiwa kupata eneo lao huko Msata mkoani Pwani ambako wanataka kuendelea na jukumu waliloamua kulifanya la kusaidia jamii na kumpendeza Mungu pia.

Watanzania sasa watanielewa, kuwa vijana hao wanahitaji msaada wa kiutu ili waishi na kulinda uhai si kufanya starehe. Wana nia hiyo na mambo yote yako dhahiri. Kijana aliyeishi bila wazazi naye ameamua kulea watoto yatima. Upendo ulioje huu!

WATOTO WETU TANZANIA

Wanasema: “Kituo chetu kilianzishwa mwaka 1998 na Evans Tegete, alianzia Tabata Mawenzi, alianza kama ‘Tuition’ lakini akajikuta kila mtoto hawezi kulipa ada hivyo ndipo akaanza kuwasaidia. Mwaka 2001 alihamia eneo la Kimara-Suka baada ya kupatiwa nyumba ya kuishi na watoto. Il mwaka 2004 alianza kuishi na watoto wa jinsia zote.

“Mwaka 2001 kituo kilisajiliwa rasmi na Serikali kama kituo cha kulelea watoto yatima na waliotokea mazingira hatarishi. Mwaka 2011 Jina la kituo lilibadilika kutoka “Friends of Don Bosco” na kuitwa “Watoto Wetu Tanzania” baada ya kugundua kuwa watu walidhani kituo kipo chini ya Kanisa Katoliki (Roman Catholic) ili hali si kweli, kituo hakimilikiwi na dini wala kabila ama chama chochote.”

Anaongeza kwa kusema: “Kituo toka kuanzishwa kinajiendesha kwa misaada mbalimbali ya wasamaria wema wanaotembelea kituo kila siku, kituo hakina mfadhili wa kudumu.

“Malengo ya kituo chetu ni kuwasomesha watoto na vijana mpaka kufikia elimu ya chuo kikuu ili waweze kutimiza ndoto zao, pia kuwaunganisha na familia zao na kuwaepusha na magonjwa kama Ukimwi na mengineyo. Mpaka kufikia sasa kuna vijana zaidi ya 40 waliofikia elimu ya chuo kikuu, kati yao vijana 25 wakiwa wamehitimu shahada ya kwanza na wengine wakiendelea na masomo. Pia wapo ambao wanasoma ngazi ya cheti na stashahada.

“Vijana na watoto waliopitia kituoni ni zaidi ya 300 lakini kwa sasa waliopo ni 78 wote wakiwa wanafunzi. Wapo wanafunzi wa awali, shule ya msingi na sekondari. Kidato cha tano wapo wanne na cha sita wapo wanane,” anasema Ndahani. CHANGAMOTO ZA KITUO

Hapo ndipo ninapowategemea Watanzania kushirikiana nasi katika jambo hili kuhakikisha vijana na watoto waliopo katika kituo hicho wanasaidia. Ndugu zangu Watanzania, yeyote anayeguswa anaweza kukisaidia kituo hiki ili wakabiliane na changamoto zifuatazo;

Kwanza kituo hakina mfadhili wa kudumu (Permanent Sponsor) hivyo kituo kinashindwa kuwalipia ada watoto na vijana wanaosoma hivyo wamekuwa wakirudishwa mara kwa mara hali inayochangia wengine kutofanya vizuri katika masomo yao.

Pili, kituo hicho hakina fedha ya kufanya ujenzi wa eneo lake lilipo Msata-Mazizi, mkoani Pwani. Eneo hilo ambalo watoto waliimba kwaya na kupata pesa na kununua. Ni ekari 37, kituo chao kimepanga kujenga makao ya watoto, nyumba za walezi pamoja na shule ili kuwezesha watoto na vijana wengi kupata mahala pa kuishi na elimu.

Tatu, idadi kubwa ya watoto hawana bima za afya, jambo ambalo ni hatari kwa afya kwani hakuna pesa za uhakika za kuwatibu pindi wanapopatwa na maradhi.

Ndugu zangu Watanzania, yeyote anayeguswa na jambo hili anakaribishwa kuwasaidia vijana hawa. Wanahitaji sana michango yetu ili wafanikishe kulea watoto walionao. Unaweza kuwasilisha mchango wako moja kwa moja kwa wafuatao: Ndahani Mwenda 0752247200 na Samweli Charless (Mratibu wa Kituo) 0717439203. Mwenyezi Mungu awalindeni. Kutoa ni moyo.

Ndahani Mwenda (katikati) akiwa na baadhi ya watoto yatima

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.