Mgogoro wa mafuta ulivyomwagusha Rais Nixon

Rai - - HOJAYA WIKI SIASA - NA GAMANYWA LAITON

KIJASHO chembamba kilikuwa kikimtiririka katika paji lake la uso, mbele yake lenzi za kamera zaidi ya 100 zilizokuwa mbele yake, miale ya taa kali za kamera zilikuwa zikimweka kila sekunde na kumulika mbele ya uso wake, mbele yake waandishi zaidi ya 400 walikuwa wakisubiri jibu kutoka kwake, akiwa Rais wa kwanza wa Marekani kung’atuliwa madarakani bila kupenda kwa kashfa dhidi ya Serikali iliyokuwa ikimkabili.

Huku mate yakiwa yamemkauka mdomoni Rais Richard Nixon, akitazama huku na kule kama akihesabu umati wa waandishi wadadisi na wenye kuchokoza mbele yake akatamka: “I’m not a Crook,” kwa Kiswahili akimaanisha yeye si ‘Mhalifu’.

Kuna msemo mmoja wa Kiswahili unaosema kuwa ‘Kamba hukatikia pabovu’ ndivyo ilivyokuwa kwa Nixon, mambo yalikuwa yamemkaba shingoni, kwani ukiachana na kashfa kubwa ya karne ya ‘WaterGate’ iliyokuwa ikimkabili, katika mitaa na katika chati za uchumi, mambo yalikuwa hayaendi sawa.

Mapema mwaka huo, Katibu wake wa Ikulu, Henry Kissinger, alikuwa amefanya ziara mahususi Mashariki ya Kati, ziara hiyo ililenga kunusuru hali ya uchumi iliyokuwa ikididimia kutokana na sababu moja ambayo ni ’Janga la Mafuta’.

Mafuta ya Petroli na Dizeli yalikuwa yameadimika mitaani, visima vilikuwa vimekauka, vituo vya kusafisha mafuta na kuuza vilikuwa vimefungwa, viwanda vikasimama, tone moja la mafuta likawa na thamani ya dhahabu. Hali ngumu ya uchumi ilikuwa imetia shinikizo na kufanya mambo yawe magumu kwa wakubwa wa Ikulu ya ‘White House’. Janga hili la Mafuta lilikuwaje? Lilisababishwa na nini? Na nini kilitokea baadaye?

Kabla ya mwaka 1970, Taifa la Marekani na Mataifa ya Ulaya Magharibi yalikuwa walaji wakubwa wa mafuta ghafi. Marekani pekee ilikuwa ikitumia zaidi ya mapipa milioni 20 ya mafuta ghafi kati ya mapipa milioni 80 yaliyokuwa yakizalishwa duniani kote kwa siku.

Kwa kiasi kikubwa soko la mafuta duniani lilikuwa limetawaliwa na mataifa haya ambayo kwa miaka mingi yalikuwa na kiburi na imani kuwa mataifa ya Kiarabu ambayo yalikuwa wazalishaji wakubwa wa mafuta ghafi hayana kauli juu ya wapi na nani yamuuzie mafuta ghafi ya petroli.

Na kadiri miaka ilivyokuwa ikienda, mataifa haya makubwa ya Magharibi yalizidi kuwa tegemezi kwa malighafi ya mafuta kwa kuwa kuanzia mwaka 1940 kuelekea kukomaa kwa vita ya pili ya dunia, mafuriko ya bidhaa za plastiki yaliikumba dunia, baada ya viwanda vingi Ulaya na Marekani kuanza kuzalisha bidhaa mbalimbali kutokana na plastiki ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa inatengenezwa kutokana na malighafi ya petrol.

Bidhaa hizo zilitia ndani chupa za vinywaji ambazo zilikuwa mbadala wa chupa za glasi, ongezeko la bidhaa hizo nyingi za plastiki kulichochea utegemezi mkubwa wa mafuta ghafi kama malighafi.

Lakini hali ikaanza kubadilika kuanzia mwaka 1970, ambapo mataifa mengine ya Ulaya hasa Ulaya Mashariki na Asia nayo yalipoanza kutengamaa kiviwanda, hivyo kuongeza shinikizo la uhitaji wa idadi kubwa ya mapipa ya mafuta kwa kuwa idadi ya wateja waliyokuwa wakihitaji

mafuta ilikuwa ikiongezeka maradufu katika soko la mafuta la dunia.

Kuongezeka kwa wateja katika soko kukapunguza ‘kuwatetemekea au kutegemea wateja wachache’ waliokuwa na kiburi hapo mwanzo mataifa ya Kibepari ya Marekani na Ulaya Magharibi, hali hii ilipelekea mataifa ya kiarabu (wauzaji wakubwa wa mafuta OPEC) sasa kuwa na kiburi, kujiamini na kuwa na kauli dhidi ya mafuta waliyokuwa wakizalisha juu ya nani wamuuzie, kiasi gani na kwa masharti yapi.

Kisha mapema mwaka 1973, vita maarufu iliyokuwa ikijulikana kama ‘Yom Kippur’ kati ya Israeli na Mataifa ya Kiarabu ya Misri na Syria, yaliyokuwa yakipigana kuwatetea Waarabu wa Palestine ikazuka.

Muda mfupi tu baada ya kuzuka kwa vita hii, Taifa la Urusi lilianza kutuma silaha nzito nzito katika mataifa ya Misri na Syria ili kusaidia upande huo wa Waarabu dhidi ya Israeli, kuona hivyo Rais wa Marekani wa kipindi hicho Richard Nixon akachukua hatua mara moja ya kutangaza kuwa Marekani itasimama na Israeli, hivyo mara moja Marekani nayo ikaanza kupeleka silaha nzito nzito Israeli.

Kuona hivyo Mataifa ya Kiarabu wazalishaji wa mafuta ghafi yakapunguza uzalishaji wa mafuta na kukata misafara ya meli zilizokuwa zikipeleka mafuta ghafi Marekani kwa kuweka kigingi kuwa hayatauzia mafuta meli ya kampuni yoyote iliyokuwa ikipeleka mafuta hayo katika ardhi ya Marekani.

Japo vita hiyo iliisha Oktoba mwaka huo, mataifa hayo yaliendelea na msimamo wa kutouza hata pipa moja kwa kampuni yoyote ya mafuta iliyokuwa ikipeleka mafuta Marekani na mataifa kadhaa ya Ulaya Magharibi yaliyokuwa upande wa Israeli.

Kwa muda fulani mataifa haya ya magharibi yalijua kuwa ni utani na kwa muda mfupi tu hali ingerudi kama kawaida, lakini Waarabu walizidi kutia mkazo na kukaza msimamo wao, taratibu Mabepari wa Magharibi wakaanza kuinamisha pua.

Waarabu walikuwa wamewakaba kooni na hali ilikuwa mbaya kwa kuwa viwanda, mifumo ya kifedha, maisha ya kawaida, kijamii na kisiasa katika mataifa haya ilikuwa imezorota kwa muda mfupi tu toka Mataifa ya OPEC yaweke mgomo wa kutoyauzia mataifa ya Magharibi mafuta ghafi.

Pipa moja la mafuta lilifikia Dola za Marekani 35 karibu dola 102 kwa thamani ya sasa, (Sh 228,582 wakati pipa moja kwa bei ya sasa katika soko la dunia linauzwa Sh 105,327 ikipanda sana hufika Sh 116,532 kulingana na Tovuti ya kibiashara ya CNBC. Vituo vingi vya mafuta katika mataifa haya ya Magharibi vingi vilifungwa na visima vya kutunzia mafuta vikakauka, biashara zikafungwa, kwa kiasi kikubwa mambo yakaanza kwenda mrama. Serikali ya Nixon haraka ikaanza kutafuta suluhu.

Januari 18, mwaka 1974, Henry Kissinger akiwa kama Katibu Mkuu wa Ikulu ya Marekani akafanya makubaliano kushawishi Israeli kujiondoa katika sehemu ya Sinai, lakini Mataifa ya Kiarabu yaliendelea na msimamo wao, Mei mwaka huo Israeli ikajiondoa kabisa katika milima ya Golani.

Kwa hali zote Richard Nixon alikuwa katika hali mbaya, kwani kwa wakati huo kashfa ya Watergate (kashfa ya matumizi mabaya wa madaraka) ilikuwa imepamba moto, ilikuwa imeikaba Serikali yake shingoni, hivyo alikuwa akipambana kufa na kupona kujinusuru dhidi ya kuondolewa madarakani.

Lakini Julai 24 ya mwaka huo, zoezi la kumshinikiza Nixon lilianza na Agosti 9 akajiuzulu na kumpa kijiti makamu wake Gerald Ford, tunaweza kusema kuwa ukiachana na kashfa ya Watergate, hali ngumu ya uchumi iliyosababishwa na kuzorota kwa uchumi kulikosababishwa na janga la mafuta kulichangia kwa kiasi flani kujiuzulu kwa Richard Nixon.

Mgogoro huo wa mafuta ghafi wa dunia, pia ulipelekea kuongezeka kwa shinikizo katika mfumo wa uchumi duniani kote na kwa kiasi kikubwa liliathiri hali ya uchumi.

Mataifa masikini hasa yale ya Amerika ya kusini na yale ya Afrika bila kusahau ya Asia ndiyo yaliyoathirika zaidi kwa kuwa, kwanza baada ya hali za kiuchumi kuwa ngumu, mataifa ya magharibi yaliongeza shinikizo na masharti katika aina na viwango vya misaada ambavyo yalikuwa yanatoa kwa nchi hizi.

Kwa hiyo tuseme kwa urahisi kuwa ile misaada iliyokuwa ikichukuliwa kirahisi na burebure na nchi hizi sasa baada ya kutokea kwa janga hili ilianza kutolewa kwa masharti magumu na si kirahisi rahisi tena.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.