Madhila waliyopandikiza wakoloni hayajakoma Afrika

Rai - - MAKALA - NA ROCKY AMINI

kurudi nyuma ni suala gumu, huku wakisahau kuwa ni rahisi kuwa kiwete kuliko kiwete kutembea. Matatizo ni sehemu ya maisha kwani huwezi kula mua bila kukuta kifundo. Popote unapoanguka inuka, jiulize kipi kimekuangusha, rekebisha kisha endelea na safari, binafsi nakutakia mafanikio mema ila kumbuka bora ugali mkavu kwenye amani kuliko wali nyama vitani!. Kwa vyovyote vile Mwafrika lazima atafakari kwa kina juu ya anguko lake ndani ya ukombozi wa fikra na kuwako kwake ulimwenguni.

Uongozi ni uwezo wa kuendana na wananchi uwaongozao. Uthamani wa kiongozi umo katika kuchukua matatizo ya wananchi wake na kuyafanya kama sehemu ya matatizo yake. Huwezi kutatua matatizo ya wananchi wako kama hutaki kubeba mapungufu hayo ya wananchi kama sehemu ya mapungufu yako. Kiongozi kama akikosa maelewano mazuri na wananchi wake, nguzo ya uongozi iliyopo ipatikanayo kati ya kiongozi na wananchi hufifia na mwishoni kupotea. Kuna muunganiko mkubwa uliopo kati ya kiongozi na yule anayeongozwa, muunganiko huu ndio huleta maendeleo juu ya yale yanayozungumzwa na pande zote mbili (tawala na tawaliwa).

Kukaa na kuzungumza na wananchi inahitaji uwepo wa maelewano baina ya pande mbili. Kama pande mbili hazielewani, basi tusitegemee kuwako kwa mazungumzo yoyote ya kimaendeleo. Unadhani taswira ya uongozi wa aina hii utakuwa na tafsiri zipi?

Tujikumbushe kipindi cha utumwa jinsi Afrika na wananchi wake tulivyokuwa tunachukuliwa na watawala wa kipindi kile. Wengi kipindi cha utumwa walituchukulia kama hatuko miongoni mwa watoto wa Mungu. Manyanyaso ya rangi ya Kiafrika yaliyokuwako kipindi kile yalikuwa mambo ambayo kwayo hayakutakiwa kuendelea kuwako katika miaka yetu hii ya sasa. Manyanyaso haya ya kibaguzi yameegemea wapi hivi sasa?

Inashangaza kuona Afrika inaendelea kunyanyasika na kuteseka kutokana na damu chafu iliyopandikizwa na wakoloni ya kuendelea kunyanyasiana sisi kwa sisi (tabaka tawala na tawaliwa).

Tumlaumu nani katika haya yote? Je ni sisi wananchi ama viongozi wanaoshikilia hatamu? Tafsiri ya mambo haya ni kwamba, kuna sehemu fulani Mwafrika katika suala la uongozi amefanya makosa, hivyo akajikuta ameangukia katika shimo kubwa lenye kelele za kila aina, huku sauti mbalimbali za unyonge zikisema:

“Hatuna maji safi, barabara nzuri, zahanati, watoto wetu wanatembea umbali mrefu wakielekea shuleni, vyuo nchini havitengenezi wanafunzi wenye uwezo wa kuangalia taswira ya Taifa katika jicho la tatu.”

Pamoja na matatizo mengine zaidi ya haya, swali la kujiuliza: “Tumekubaliana sisi pande mbili (tabaka tawala na tawaliwa) kuendelea kusikiliza sauti za namna hii?

Damu ya ukombozi iliyoibuka miaka ya 1920 mpaka 1960 kipindi nchi nyingi za Kiafrika zilipopata Uhuru, ni damu ambayo haikuwa na malengo mbadala zaidi ya kulikomboa bara la Afrika kutoka utumwani. Utumwa wa kikoloni. Hatuwezi kusahau mchango wa Jommo Kenyata, Kamuzu Banda, Milliton Obote, Keneth David Kaunda, Kwameh Nkrumah, Patrice Emery Lumumba na shujaa wetu Julius Kambarage Nyerere. Hawa wote walikuwa kwa pamoja na damu ya ukombozi kwa manufaa ya bara lote la Afrika na watu wake.

Hawa ni viongozi wachache ambao ni mashujaa wa Afrika ambao hawakupenda Afrika iendelee kukosa mlezi wa kuiongoza na kuimulikia mwangaza wa maendeleo. Mwangaza wa kuimulika Afrika na mwongozo wake ulipatikana baada ya wapiganaji wa uhuru kuacha mambo yote yasiyofaa ya manufaa yao na kuwekeza nguvu yao yote kuikomboa Afrika.

Wote hawa kwa ujumla walitoa mapendekezo yao juu ya mustakabali wa bara la Afrika pamoja na viongozi mbalimbali kote duniani ambao hawakupendezwa na unyanyasaji wa rangi duniani kote. Viongozi hawa wote wakiongozwa na Kwameh Nkrumah waliendelea kutafakari suala la kuwa na Afrika moja na yenye dola moja. Haya yalikuwa mawazo mapana sana ambayo leo hii yangepatiwa ufumbuzi na kuwekewa msisitizo na jopo zima la waliokuwa viongozi enzi hizo, basi leo hii tusingekuwa tunajiita sisi Wakenya, sisi Watanzania ama sisi Wasomali na kwingineko, huku tukiacha kutanguliza uasili wetu wa sisi Waafrika. Nadhani leo hii tusingekuwa na minong’ono mingi juu ya maswala ya Mwafrika na uongozi badala yake tungelikuwa na mjadala wa Afrika huru na yenye mategemeo makubwa ya kuingia katika maendeleo ya vitu na fikra na nchi zingine duniani ndani ya miaka hamsini ijayo. Mantiki ya Afrika ya vitu ikiwa ile Afrika ambayo itakuwa na uwezo wa kutengeneza bidhaa yenyewe bila kutegemea nchi nyingine za Ulaya na Mashariki ya mbali, huku ikichoma bidhaa zote zinazoletwa kutoka nje ya bara la Afrika. Huku Afrika ya fikra ikiwa ile itakayokuwa na uwezo wa kuiaminisha dunia na watu wake juu ya mawazo mapya na yenye mitazamo tofauti inayoishangaza dunia na wala si aina ya mawazo yale mgando ya kuendelea kuhimiza mwananchi kuwa na uvumilivu wa nafsi na kuaminishwa kuwa katika kisiwa cha amani, amani inayojipinga yenyewe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.