Uendeshaji ligi kimazoea unadidimiza soka

Rai - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

Mviwanja ICHUANO ya Ligi Daraja la Kwanza maarufu kama ‘FDL’ imeanza rasmi mwishoni mwa wiki katika mbalimbali nchini kwa kushirikisha jumla ya timu 24.

Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa na hata umaarufu baada ya ile ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara maarufu kama Ligi Kuu ya Vodacom ‘VPL” ambayo ilianza toka mwezi uliopita ikishirikisha timu 16 tu.

Tofauti ya idadi ya timu kati ya VPL na FDL tayari inaonekana wazi kuwa michuano ya Ligi ya daraja la kwanza ni yenye ushindani zaidi licha ya kutokuwa na msisimko unaolingana na ligi kuu.

Ukichunguza FDL unaweza kuona timu nyingi zimekuwa na ushindani wa jadi kwa muda mrefu kama vile Coastal Union, Friends Rangers, African Sports, Ashanti na nyinginezo ingawa hata hivyo msisimko unapungua pengine kutokana na ligi yao kutopewa sapoti kubwa.

Kimsingi hakuna tofauti kubwa sana kati ya Ligi hizo mbili isipokuwa Ligi Kuu inabebwa zaidi na udhamini mnono toka Vodacom pamoja na Azam Tv sambamba na ule ushindani uliopo wa timu kubwa kongwe nchini za Simba na Yanga ambazo ndizo zinazoipa chati michuano hiyo achilia mbali kusimama kama roho ya soka la Tanzania.

Ukiacha timu hizo kongwe nyingine zote zilizobaki Ligi Kuu hazina sana msisimko zaidi ya kuungwa kwao mkono kutokana na siasa za soka tu ndani ya mikoa yao.

Pamoja na umaarufu wa timu nyingi za Daraja la Kwanza lakini inaonekana dhahiri Ligi hiyo haipewi sapoti kubwa sio tu na mashabiki bali hata wasimamizi wa mchezo huo wakiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Ni aibu kwa ligi kubwa na yenye mchango mkubwa katika kuzalisha vipaji ndani ya Ligi Kuu pamoja na ujenzi wa kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ ikiendeshwa bila ya mdhamini wa uhakika hivyo kuendelea kuwepo kwa ile dhana ya kimazoea.

Unapozungumzia ushindani uliopo ndani ya Ligi Kuu huwezi kuacha kuzungumzia kiwango cha wachezaji na hata timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza kwani ndiyo msingi mkubwa wa kuzalisha wachezaji ndani ya michuano hiyo yenye hadhi ya juu kwa hapa nchini.

Ubora uliopo kwa sasa Ligi Kuu unatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na TFF katika usiamamizi wake. Lakini pia wadhamini makini nao wamechangia kuifanya ligi hiyo kuwa na msisimko zaidi, lakini katika FDL vitu hivyo vyote havipo.

Ni miaka mingi sasa Ligi hiyo imekuwa ikiendeshwa kimazoea kwani imekosa ufuatiliaji wa karibu pamoja na mbinu kadhaa za kuiboresha. Pengine baadhi ya matukio ya mara kwa mara kama vile vurugu, ubabe kwa baadhi ya timu pamoja na mashabiki kujichukulia sheria mikononi mwao inaweza kuwa mfano tosha ni jinsi gani michuano hiyo ilivyoachwa yatima.

Timu za majeshi zimekuwa na tabia ya kuhatarisha amani katika viwanja vya soka hasa pale zinapogoma kukubaliana na matokeo ikiwa hayazifurahishi timu yao.

Katika mechi ya mwishoni mwa wiki iliyochezwa katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, mjini Tabora mashabiki wanaodaiwa kuwa wa timu ya Rhino ya Tabora waliwapiga wachezaji wa timu pinzani ya Alliance ya Mwanza baada ya kufungwa bao 1-0. Kama hiyo haitoshi mashabiki hao waliwapiga waandishi wa habari waliotaka kuripoti tukio hilo sambamba na viongozi wa Alliance.

Lakini tukio kama hilo limeshatokea katika viwanja kadhaa kikiwemo cha Mkwakwani Tanga kinachotumiwa na timu za Coastal Union na African Sports, Samora, Iringa ilichokuwa kikitumiwa na Lipuli (sasa iko Ligi Kuu) sambamba na kile cha Njombe.

Katika msimu wa 2015/2016 timu ya Polisi Tabora ilifanya vurugu katika moja kati ya michezo ya mwisho ya Ligi hiyo msimu huo baada ya kupora ripoti ya kamisaa wa mechi baada ya kubaini licha ya kushinda kwa mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro wasingeweza kupanda daraja.

Kama hiyo haitoshi katika mechi nyingine ya kumaliza msimu huo, Geita Gold Mine inadaiwa kupanga matokeo na JKT Kanembwa ya Kigoma hivyo kuutia doa mchezo huo ambapo hata hivyo iliibuka kashfa nyingine iliyodaiwa kuwahusisha baadhi ya viongozi wa TFF kushiriki kupanga matokeo.

Hayo ni mfano tu wa matukio ya uvunjifu wa amani yanayotokea mara kwa mara katika michuano hiyo kutokana na usimamizi duni. Udhaifu huo unatokana na ligi hiyo kutokuwa na mdhamini madhubuti pamoja na kutooneshwa ‘live’.

Hakuna Kampuni inayoweza kutoa fedha zake kisha anachokidhamini kisilete tija, hali ambayo itawafanya wasisimamizi wa mchezo huo kuamka na kuzidisha umakini katika usimamizi na uendeshaji wa ligi husika.

Msimu huu wa 2017/2018 michuano hiyo imeanza lakini kuna kila dalili ya kutokea matatizo hapo baadaye zaidi ikiwa ni kutokana na idadi ya timu zilizotangazwa kupanda daraja ambapo kila kundi kati ya matatu yaliyopo hivi sasa yatatoa timu mbili kila moja hivyo kufanya timu sita kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Kuna haja sasa ya TFF kuimulika ligi daraja la kwanza ili kuepuka vitendo kama hivyo lakini pia kuisimamia kikamilifu na kuipa sapoti ili kuwa na michuano yenye ubora ambayo itakuja kujenga ligi kuu bora.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.