Nyalandu aweka mambo hadharani

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

»Ni baada ya kuhusishwa na usaliti »Ataka haki itendeke kwa Tundu Lissu

A

MPANGO wa kumpeleka Lissu Marekani uko palepale, kilichotufanya tusitishe ni...

B

HAYO

ni maneno ya uongo, ndio maana kitabu kitakatifu Biblia inasema usimshuhudie jirani yako uongo.

MBUNGE wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu kwa mara ya kwanza amefanya mahojiano maalumu na RAI kwa njia ya simu na kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii yanayoendelea nchini pamoja na yale yanayomuhusu moja kwa moja.

Nyalandu amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wachache wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaoendesha siasa safi.

Hata hivyo, katika siku za karibuni baadhi ya makada wenzake ndani ya chama chake wamekuwa wakimtazama kama mtu anayejiimarisha kisiasa kwa masilahi yake ya baadae.

Hoja hiyo inabebwa na uamuzi wake wa kutoa misaada mbalimbali hasa ya kiafya kwa baadhi ya Watanzania.

Pia kitendo chake cha kuwa Mbunge wa kwanza wa chama tawala kwenda nchini Kenya kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ambaye yuko jijini Nairobi kwa matibabu baada ya kupigwa risasi Septemba 7, mwaka huu.

Mbali ya kwenda kumjulia hali Lissu, Nyalandu alikwenda mbali zaidi kwa kutaka kumhamishia mwanasiasa huyo nchini Marekani ili akapatiwe huduma bora zaidi za kiafya.

Pamoja na hilo, Nyalandu ambaye sasa baadhi ya watu wanamtazama kama mwanasiasa wa CCM anaekwenda kinyume na chama chake, amewataka wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla kumchangia na kumwombea Lissu.

Hoja ya Nyalandu kuhisiwa kwenda kinyume na chama na serikali inayoongozwa na chama chake, inachagizwa na kauli na maagizo ya hivi karibuni yaliyotolewa na viongozi wa wizara, idara na taasisi za Serikali ya kupiga marufuku mikusanyiko ya kumwombea Lissu, pamoja na kuwataka Watanzania kutoendelea kumchangia mwanasiasa huyo kwa madai kuwa Serikali inaweza kulipia matibabu yake popote pale duniani.

Hata hivyo, kwa upande mwingine mwanasiasa huyo ambaye sasa amekuwa gumzo nchini anatazamwa kama shujaa na mtu mwenye moyo wa upendo kutokana na matendo ya kibinaadamu anayoyafanya kwa watu mbalimbali kwa miaka mingi sasa.

Ukweli wa hoja hii unadhihirishwa na yeye mwenyewe kwa kusema kuwa yote anayoyafanya ni kwa sababu ya upendo wake na hofu aliyonayo kwa Mungu na kwamba hafanyi kwa masilahi yoyote.

AWEKA MAMBO HADHARANI

Akizungumzia hoja ya usaliti dhidi ya chama chake ambayo imenza kuelekezwa kwake Nyalandu alisema hajawahi kukisaliti chama chake na hata madai yanayosambazwa kuwa ameitwa na chama chake ili kuhojiwa hayana ukweli wowote.

“Si kweli kwamba nimeitwa na Kamati Kuu ya CCM, ni watu tu wanapenda kunichonganisha na chama changu.

“Tena niwaambie kuwa CCM kinafurahia haya ninayofanya kwa sababu mimi pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama Taifa hivyo najua ninachokifanya ni sawa na matendo ya huruma kwa Mwenyezi Mungu.”

KUHAMIA UPINZANI

Kuhusu madai ya dhamira yake ya kuhamia upinzani mwaka 2020, Nyalandu alisema hayo ni maneno ya uongo na kutaka yapuuzwe.

“Hayo ni maneno ya uongo, ndio maana kitabu kitakatifu Biblia inasema usimshuhudie jirani yako uongo, hivi majuzi niliwasaidia watoto wale waliopata ajali na hawa wengine vilevile nimewasaidia hakuna cha siasa pale kwa sababu hata wazazi wao sijui ni chama gani.

“Sifanyi hii kazi kwa ajili ya siasa, wala kujinufaisha mimi binafsi, ninafanya kwa ajili ya Utukufu wa Mwenyezi Mungu pekee kwa sababu sifa na utukufu ni wake.

“Ninachowaomba Watanzania wajielekeze kwenye maombi kwa sababu ndugu yetu Lissu ameumizwa vibaya, amedhulumiwa sana.

“Tukemee hali hii. Na wale wote waliohusika tunaiomba Serikali ihakikishe wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria bila kujali dini, kabila wala itikadi zao.”

LISSU NI LAZIMA APELEKWE MAREKANI

Nyalandu amesema mpango wa kumpeleka Lissu nchini Marekani kwa matibabu uko pale pale, hakuna kilichositishwa.

“Mpango wa kumpeleka Lissu Marekani uko palepale, kilichotufanya tusitishe ni kusubiri recommendation za madaktari ambao waliomba kukaa naye kwa muda mfupi ili awe vizuri kwanza na watakapokamilisha tutampeleka Amerika.

“Pia kilichotufanya tushindwe kumpeleka Lissu mapema ni sababu ya majeraha ambayo yalikuwa yanavuja damu na majeraha mengine ambayo kwa mujibu wa madaktari walituomba tuvute subira kwanza kutekeleza suala hilo.

“Niseme kwamba ulazima pia wa kumpeleka Lissu Amerika upo kwa sababu kwanza lazima afanyiwe matibabu ya ‘therapy’ ambayo ni ya utaalamu wa hali ya juu sana na unafanywa na madaktari bingwa duniani. Ndio maana nasema uamuzi wa kumpeleka Lissu Marekani uko palepale kama viongozi wa Chadema walivyozungumza hivi karibu kuwa macho na masikio yetu kwa sasa yapo kwa madaktari wanaomtibu,” alisema Nyalandu.

MTAJI WA KISIASA

Amesema mambo yote ya kusaidia jamii anayoyafanya kamwe hayana lengo au mtaji wa kisiasa bali anafanya kazi ya Mungu.

“Hakuna siasa katika suala la kutekeleza kazi ya Mungu. Hakuna siasa pindi mpinzani anapoumia. Mpinzani ameumia lazima niwajibike.

“Lissu ni ndugu yangu, ameumizwa vibaya sana pia ni sawa na ndugu yetu watanzania wote, tumeshuhuhudia namna alivyoumizwa. Ni vema Watanzania tukasimama katika maombi zaidi kumuombea ndugu yetu na kuweka pembeni tofauti zetu za kisiasa kwani hata kama angekuwa ni mtu mwingine ningewajibika vilevile kwa kadiri niwezavyo.”

UAMUZI WA SERIKALI

Akizungumzia uamuzi wa Serikali kutangaza kuwa na utayari wa kumtibu Lissu popote pale duniani, Nyalandu alisema hilo ni jambo jema.

“Kwa kuwa serikali ilisema ipo tayari kumpatia matibabu iwapo familia ikiwasilisha barua ya maombi yao ni jambo jema sana.

“Niseme wazi kuwa hili ni jambo ambalo nililifurahi sana. Nimpongeze rafiki yangu Ummy Mwalimu kwa kutamka kauli hiyo kwani nimefurahi kusikia kauli hiyo ya Serikali kwa sababu mipango ya kushirikisha wadau wote katika matibabu ya ndugu yetu ipo kwenye lengo ni kupigania afya ya Lissu.

“Hakuna sababu ya kurushiana maneno wala kuzusha ugomvi ili hali ndugu yetu anaumwa. Niweke wazi kwamba sina masilahi wala chochote katika hili ninalopigania sasa zaidi ya kutekeleza maandiko ya Mungu kwa kupigania afya ya ndugu yangu.”

HALI YA KISIASA NCHINI

Alisema kila kitu ni mipango ya Mungu na kwamba kwa sasa Mungu ameruhusu iwe hivi ilivyo sasa.

“Niseme kwamba Mungu anaruhusu majira na nyakati, kwa wakati huu Mungu ameruhusu Rais John Magufuli atuongoze sisi Watanzania. “Tumeona kabisa Rais Magufuli kuna vitu vingi anavirekebisha, anarudisha nidhamu anaipeleka Tanzania kuwa moja ya nchi ya uchumi wa viwanda. Ni mambo makubwa anaitendea Tanzania yetu hivyo ninawaomba Watanzania watulie, wamuunge mkono Rais Magufuli… kila mtu asimame katika nafasi yake kumuombea Rais wetu ili aendelee kuirekebisha Tanzania.

“Tuepukane na hali ya kutoelewana kwa tofauti zetu za kisiasa kwa sababu hakuna faida yoyote katika hali hiyo.”

MPANGO WA URAIS

Kuhusu dhamira yake ya kuutaka urais wa Tanzania, Nyalandu alisema kwa sasa jukumu lililombele yake ni kuwahudumia wapiga kura wake.

“Unajua wanasiasa wana mipango mingi, kwa sasa nitakosea sana nikisema nina mpango wa kugombea tena nafasi ya urais wakati mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu nilimpigia kura Magufuli, nilimuunga mkono kwa hali na mali hadi chama chetu kikashika madaraka.

“Kusema ukweli sasa nina kazi ya ubunge ambayo wanaSingida Kaskazini wamenipa na hata sasa ninapozungumza na wewe nipo jimboni kwangu natekeleza majukumu ya kuhakikisha miradi ya Singida inatekelezwa kwa usimamizi wa hali ya juu kwa faida ya wanaSingida na Watanzania wote kwa ujumla.

“Kwa maana hiyo nitaifanya hii kazi ya ubunge kwa moyo wangu wote bila kujali itikadi yoyote ya kisiasa ili kuleta maendeleo kwa Watanzania kama vile Rais wetu John Magufuli alivyodhamiria.”

SI MARA YA KWANZA KUTOA MSAADA MEI 2013:

Akiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Nyalandu alishiriki kuwajulia hali majeruhi wa mlipuko wa bomu kanisani wakati wa uzinduzi wa Parokia ya Olasiti, Jimbo Kuu la Arusha na kuwa waziri pekee aliyejitolea kutafuta ndege ya kuwapeleka Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.

MEI 2017:

Mei mwaka huu alishiriki kikamilifu, akishirikiana na taasisi ya Elimu ya Afya ya Sioux na Tanzania (Stemm) kutafuta msaada wa usafiri wa kwenda Marekani na matibabu kwa watoto watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent walionusurika katika ajali ya basi dogo iliyoua wanafunzi 29, walimu wawili na dereva.

Wanafunzi hao Doren Mshana, Wilson Tarimo na Sadya Awadh wamesharejea nchini wakiwa katika hali nzuri baada ya ajali hiyo kuwaacha

katika hali mbaya na wamesharejea shuleni.

SEPTEMBA 2017

Tangu Septemba 7 siku ambayo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi 32 na kujeruhiwa vibaya, Nyalandu amekuwa mbunge pekee wa CCM kumjulia hali, kumwombea na kuwaomba watanzania wamuombee Lissu pamoja na kujiandaa kumsaifirisha Lissu kwenda Marekani kwa matibabu zaidi.

Aidha, akiwa Mbeya katika moja ya harakati za kumuombea Lissu, Nyalandu alisema tukio hilo ambalo lilitokea nje ya majengo ya makazi ya Lissu mjini Dodoma, ni la kisiasa.

SEPTEMBA 7, 2017:

Aidha, Mbunge huyo pia usiku wa Septemba 7 aliwaokoa watoto wawili Nuru pamoja na Seif ambao walipata ajali na kuvunjika vibaya huku watu wengine saba wakipoteza maisha katika ajali iliyotokea mkoani Singida.

Nyalandu alifanya maamuzi hayo baada ya kupata taarifa kuwa watoto hao licha ya kuvunjika vibaya miguu lakini walipewa tiba za kijadi kwa kufungwa majeraha yake kwa njia za kijadi.

“Usiku wa kuamkia leo (Septemba 7), majira ya saa 6 usiku nilienda kijijini Ilongero na kuwachukua watoto wawili (Nuru na Seif) waliokuwa wamevunjika vibaya miguu kupitia ajali ya Lori la Mnadani wiki iliyopita. Watoto hawa walifungwa majeraha yao kwa njia za kijadi, ambako baada ya kuwafikisha hospitali ya Malkia wa Ulimwengu, Puma Wilaya ya Ikungi, sasa wamepangiwa kufanyiwa upasuaji kwa dharura” alisema Lazaro Nyalandu

SEPTEMBA 26:

Septemba 26 mwaka huu, Nyalandu alisaidia kumsafirisha kwa ndege mgonjwa Samson Mwanga, mkazi wa kijiji cha Mipilo, aishiye kijiji cha Gidika (Manyara) kutoka katika Hospitali ya Hyadom mkoani humo kuelekea katika hospitali ya KCMC Moshi.

Kwa mujibu wa Nyalandu mgonjwa huo alipasuka mshipa kichwani na kusababisha kuhitaji kile madaktari walichokiita ‘Immunogloblin Injections” ili kunusuru maisha yake.

“Tumempandisha ndege ya Shirika la “Flying Medical Doctors”, iliyotokea Nairobi na kuwasili hapa Hydom. Nawashukuru madaktari na wanafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Hydom kwa utumishi wao uliotukuka, na kwa kumhudumia mgonjwa hadi tukaweza kumpandisha ndege kwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Kilimanjaro mchana huu (juzi),” alisema.

Tundu Lissu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.